top of page

Je, Serikali ya Tanzania Inalea Makundi ya Kigaidi?

Na. Rev. Godwin Chilewa




Kauli ya Shekhe Mwaipopo kwamba ana makundi mawili ya vijana, Mbwa Mwitu na Tiger waliopatiwa mafunzo ya kijeshi, na kwamba watatumika kuwaangamiza vijana watakaoandamana tarehe 7 Julai si kauli ya mzaha. Ni kauli nzito, ya kutisha, na yenye harufu kali ya ugaidi.


Ikiwa vyombo vya ulinzi na usalama vitakaa kimya na bila kumkamata shekhe huyo na majeshi yake, basi dunia itachukulia ukimya huo kama hatua ya kuhalalisha vurugu, umwagaji damu, na hofu kama mfumo wa utawala. Tena itaonekana sasa serikali imeamua kuunda na kutumia makundi ya ugaidi ili kuzima upinzani. Jambo baya kabisa!


Ugaidi ni nini? Kwa tafsiri ya jumla, ugaidi ni matumizi ya vitisho au nguvu za vurugu, mateso au mauaji dhidi ya mtu, kikundi cha watu, au raia kwa lengo la Kusababisha hofu, Kushinikiza itikadi ya kidini au ya kisiasa, na au kuzuia haki au uhuru wa watu


Ugaidi hauhitaji kuwa na sare za kijeshi wala kutambuliwa rasmi. Unaanza pale mtu au kundi linapotangaza au kutekeleza vitendo vya kutisha dhidi ya watu wasio na hatia.


Ugaidi umegawanyika katika makundi mawili: Ugaidi wa ndani na ugaidi wa kimataifa. Ugaidi wa kimataifa ni ule unaovuka mipaka ya nchi ambapo makundi husika hufanya mashambulizi katika nchi tofauti na huwa na mtandao wa kimataifa, na au kushirikiana na makundi mengine ya kigaidi yenye imani au itikadi zinazofanana.


Lakini hatari kubwa zaidi mara nyingi ni ugaidi wa ndani ambao huanzia ndani ya taifa, na kufanywa na raia au makundi ya ndani dhidi ya raia wenzao, mtu mmoja mmoja, au vikundi vya watu wa itikadi, dini, au imani tofauti, na au kabila na hadhi ya kijamii.


Mara nyingi ugaidi wa ndani hujificha kwa sura ya Vikundi vya “ulinzi” au wanamgambo, Makundi ya kisiasa yasiyo rasmi, Vikosi vya kujiteua na kadharika. Makundi haya mara nyingi huanza kwa kauli kama za vitisho kabla ya kumwaga damu.


Kwa maelezo haya bila shaka utaona kwamba makundi mawili ya shekhe Mwaipopo (kwa mujibu wa maelezo yake mwenyewe) yana sifa zote za kigaidi. Yana mafunzo ya kijeshi, uongozi, itikadi, malengo na yanatumia hofu, vitisho na mipango yote ya kigaidi kutekeleza malengo yao japokuwa malengo hayo yanashabihiana na lengo la serikali iliyoko madarakani.


Pamoja na hayo, Mwaipopo ametambulisha moja wapo ya kundi lake kama “Tigers” jina lililowahi kutumiwa na Kundi maarufu la kigaidi la Sri Lanka, Liberation Tigers of Tamil Eelam (LTTE), Kundi hili lilikuwa maarufu sana miaka ya 1976 hadi 2009. Haijulikani kama kundi la Mwaipopo au viongozi wake wana uhusiano na kundi hilo, au kuna nini kinachowaunganisha.


Aidha shekhe Mwaipopo alilitambulisha kundi la pili kwa jina la Mbwa mwitu, jina linaloeleza kwa kina aina ya utendaji wake. Katika mazingira ya ugaidi wa kisasa, hasa unaohusishwa na Islamic State, kuna dhana ya “lone wolves” (mbwa mwitu peke) mbinu ya mashambulizi  ya mtu mmoja anayejitegemea. Hii inaonesha shekhe Mwaipopo hakuwa akitania, alikuwa akieleza kitu anachokijua.


Tanzania ina sheria wazi inayopinga ugaidi. Sheria hiyo The Prevention of Terrorism Act inakataza kuunda au kushiriki katika kundi la kigaidi. Kutoa mafunzo ya kijeshi kwa raia bila mamlaka. Kutishia au kupanga mashambulizi dhidi ya raia. Kwa mujibu wa sheria hii, hata kauli ya kupanga au kutangaza matumizi ya nguvu dhidi ya raia inaweza kuchukuliwa kama kitendo cha ugaidi.


Ukiangalia vitendo na kusikiliza kauli ya Mwaipopo utaona vipengele vyote vya ugaidi: Kwanza, ametangaza uwepo wa makundi yenye mafunzo ya kijeshi. Hii peke yake ni tishio kwa usalama wa taifa. Pili makundi haya hayako chini ya mamlaka ya serikali. Hayatambuliki kama jeshi, polisi, au chombo chochote halali.


Tatu lengo lao ni kushambulia raia wanaotumia haki yao ya kikatiba, hata kama bado hawajaruhusiwa na serikali. Maandamano ya amani ni haki, kuwatisha au kuwashambulia ni uhalifu mkubwa. Nne, ametumia lugha ya vitisho na kuangamiza. Hii si siasa, si hoja, ni sura ya wazi ya ugaidi wa ndani.


Kwanini serikali haijachukua hatia ya kumkamata shekhe Mwaipopo na makundi yake? Hapa ndipo penye hatari kubwa zaidi. Kwasababu kimya hicho kinaashiria aidha kuunga mkono uwepo wa makundi hayo, na au kutojali kwa sababu Mwaipopo anafanya kile ambacho serikali inatamani kifanyike. Yaani ridhaa ya kimya kimya. Kama ni hivyo, basi taifa linaelekea kwenye hali ya kutisha sana.


Historia ya dunia inatoa onyo kali sana kuhusu uzembe wa aina hii. Serikali zinapoanza kuvumilia au kuunga mkono vikundi visivyo rasmi kwa sababu vinawalinda au vinawasaidia kisiasa, matokeo huwa mabaya. Nchini Colombia, makundi ya paramilitary yaliyoanza kama “ulinzi” yaligeuka kuwa mashine za mauaji


Nchini Sudan, makundi ya Janjaweed yalipopewa nafasi yalihusika katika mauaji ya halaiki na kuwa tishio kubwa. Nchini Libya, makundi ya wanamgambo yaliyoachwa yakue yalivunja kabisa utawala wa taifa. Haya yote yanatupa fundisho moja. Ukilea chatu, siku moja atawameza hata waliomlea.


Ikiwa leo vijana watafundishwa kuua wenzao kwa sababu ya tofauti za mawazo, kesho taifa halitakuwa na msingi wa haki, bali wa hofu. Wamarekani husema “What goes around, comes around.”


Kama serikali haitachukua hatua leo kumkamata Mwaipopo na kundi lake, basi itaonekana dhaifu mbele ya sheria. Itazidi kuondoa imani ya wananchi. Itakuwa inajenga msingi wa machafuko ya baadaye. Amani haijengwi kwa vitisho, bali kwa haki.


Ni muhimu sana serikali ichukue hatua kusimamia sheria, kukamata wahusika, na kulinda haki za raia. Kukaa kimya kutachochea ugaidi wa ndani na kufungua mlango wa machafuko yasiyodhibitika. Kauli ya Mwaipopo si jambo la kupuuzwa. Ni jaribio la kupima mipaka ya sheria na ujasiri wa serikali.


Mchelea mwana kulia, hulia yeye!


Uwe na amani.

 
 
 

Comments


bottom of page