top of page

Hali ya Kisiasa, Usalama wa Ndani, na Taswira ya Kimataifa ya Tanzania

Na Rev. Godwin Chilewa

Tarehe 10 August 2026



Tathmini ya sasa inaonesha kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko katika hatua ya shinikizo na msongo wa kisiasa wenye mwelekeo wa kuathiri uthabiti wa muda wa kati, lakini bado haijafikia kiwango cha mgogoro wa wazi (open conflict). Hata hivyo kama hatua za dhati hazitachukuliwa hali inaweza kudorora zaidi.


Viashiria vya msingi vinajumuisha kupungua kwa uhalali wa kisiasa (political legitimacy erosion) wa serikali iliyopo madarakani, kuongezeka kwa mgawanyiko wa kijamii (societal polarization), kuporomoka kwa taswira ya kimataifa, ikithibitishwa na mwelekeo hasi katika Global Peace Index, na kuongezeka kwa hasira ya wananchi na matamshi yanayoweza kuhamasisha hatua za umma zisizodhibitiwa.


Hali hii inaashiria uwezekano wa kutokuwa na utulivu mijini na machafuko ya mara kwa mara au vurugu zinazojirudia kwa vipindi, badala ya vita ya wenyewe kwa wenyewe au vurugu za kudumu kwa muda mrefu.


2. TATHMINI YA KIITELIJENSIA

2.1 Kupotea Kwa Udhibiti wa Simulizi

Serikali inapoteza udhibiti wa simulizi ya kitaifa. Vyanzo visivyo rasmi (hasa mitandao ya kijamii) vinatengeneza ( shape perception) ya umma. Hii inafanya mtazamo (Narrative) mbadala kuhusu dola na matumizi ya nguvu kuenea bila kupingwa kwa ushahidi unaoaminika.

Tathmini: Hatari kubwa kwa uhalali na uaminifu wa dola.


2.2 Kuporomoka kwa uhalali wa mamlaka

Kuna dalili za kuporomoka kwa uhalali wa mamlaka katika jamii. Mwelekeo wa wazi wa wananchi au makundi ya wananchi unaonesha kupungua kwa uhalali wa uongozi wa juu, na kukua kwa matumizi ya lugha ya kupinga mamlaka.

Tathmini: Kudhoofika kwa uhalali wa mamlaka. Dalili ya mwanzo ya kutokea kwa hali ya sintofahamu ya kisiasa. Hii ni mbaya kuliko maandamano ya kawaida


2.3 Kuongezeka kwa kasi kwa mgawanyiko wa kijamii na kisiasa

Mitazamo ya kisiasa inazidi kuwa na mgawanyiko kati ya upande unaoiunga mkono dola dhidi ya upande unaoipinga dola. Mgawanyiko huu mwanzo ulikuwa unaonekana zaidi nje , lakini sasa unajionesha hata ndani yako chama tawala na serikali.


Dalili za kuwagawa watu kwa misingi ya “sisi” na “wao” (kuona upande mwingine kama adui) zimezidi kukua kwa kasi. Kuna ongezeko la mgawanyiko wa kitaifa kati ya Watanzania bara (Watanganyika) na Watanzania visiwani (Wazanzibari).

Tathmini: Hatari ya juu. Kudhofika kwa uzalendo na umoja wa kitaifa, vita baridi kati ya Watanganyika na Wazanzibari. Muungano hatarini.


2.4 Viashiria vya uhamasishaji

Matumizi ya lugha inayochochea hatua yameongezeka. Wito wa kuchukua hatua na kuhamasisha ujasiri dhidi ya mamlaka iko katika kiwango cha juu. Sababu za wazi ni pamoja na uchungu wa matukio ya Oktoba 2025, kuendelea kushikiliwa kwa Tundulisu, na muendelezo wa matukio ya utekaji nyara au matumizi ya nguvu dhidi ya wapinzani.

Zingatia: Hii ni hatua ya mwisho kabla ya maandamano makubwa yasiyodhibitiwa.

Tathmini: Kuwepo kwa mazingira ya awali ya uhamasishaji wa umma. Kuna hatari ya kuibuka kwa matukio ya vurugu katika maeneo mahususi iwapo hali itaendelea hivi.


2.5 Kuporomoka kwa Taswira ya Tanzania Kimataifa

Tanzania imeanza kuonekana kama nchi yenye mgogoro wa ndani, na uwezekano wa kutokea kwa hali ya kutokuwa na utulivu. Ripoti kama Global Peace Index zinapotaja mgogoro wa ndani wawekezaji hujiondoa au kuacha kuwekeza, washirika wa kimataifa huongeza tahadhari, na mabenki husita kuipa nchi mikopo au hutoa mikopo yenye riba kubwa zaidi.

Tathmini: Hatari ya kiuchumi yenye athari za kimkakati


3. CHANZO CHA MSUKUMO (ROOT CAUSES)

Uchambuzi unaonesha sababu kuu ni pamoja na kuzorota kwa imani kati ya serikali na wananchi, kuendelea kushikiliwa kwa mwenyekiti wa CHADEMA, Mhe.Tundu Lissu, serikali kushindwa au kuchelewa kutoa taarifa wazi na zinazoaminika hasa kuhusu miili ya waliofariki Oktoba 2025, shinikizo kutoka kwa vijana (GenZ) wanaotaka uwajibikaji wa haraka, kuminywa kwa vyama vya upinzani na kukosekana kwa nafasi ya wazi ya ushindani wa kisiasa


3.2 Kushindwa kwa Mfumo wa Taarifa na Mawasiliano

Ukosefu wa taarifa wazi na zinazoaminika unasababisha uvumi kuchukua nafasi ya ukweli, na propaganda (kutoka pande zote) kupata nguvu


3.3 Shinikizo la Vijana na Mienendo Yake

Kundi la vijana (urban, digitally connected) lina uwezo mkubwa wa kuhamasisha kupitia mitandao. Vijana hawa wana uvumilivu mdogo kwa mifumo ya jadi, wengi wao ni wasomi na wanaojitambua. Hili linaongeza kasi ya mabadiliko ya kisiasa.


3.4 Kubanwa kwa Nafasi ya Kisiasa

Kukosekana kwa nafasi ya wazi ya kisiasa :kunasababisha ongezeko la msongo wa kisiasa, kuzalisha hisia za kutengwa, na kusukuma baadhi ya makundi kuelekea njia zisizo rasmi za kujieleza.


4. UTABIRI WA HATARI (RISK FORECAST)

Ndani ya miezi 6 hadi 18 ijayo, hali inaweza kuelekea kama ifuatavyo:


Hali inayowezekana zaidi:

Maandamano ya hapa na pale hasa katika miji mikuu, na maeneo yote ambako vijana wana ushawishi mkubwa. Kuongezeka kwa mvutano wa kisiasa


Hali ya hatari ya kati:

Machafuko makubwa ya mijini. Hatua kali za usalama zinazoongeza hasira ya umma


Hali mbaya (uwezekano mdogo lakini athari kubwa):

Migogoro ya muda mrefu kati ya dola na makundi ya kiraia. Mvutano mkubwa kati ya Watanzania bara na Wazanzibari (kiasi cha kufikia kushikana mashati)


5. MAPENDEKEZO YA KIMKAKATI

Hatua zifuatazo zinapendekezwa:

5.1 Kurejesha Uaminifu wa Umma

Mhe. Rais afanye mawasiliano ya wazi, ya ukweli na yenye ushahidi. Epuka majibu ya kukataa bila uchunguzi


5.2 Kuruhusu Uchunguzi Huru

Ruhusu uchunguzi huru na wa haki kuhusu matukio ya Oktoba 2025 na tuhuma zote za matukio ya utekaji nyara na ukiukaji wa haki za binadamu. Matokeo yawekwe wazi kwa umma


5.3 Kufungua Nafasi ya Kisiasa kwa Udhibiti

Ruhusu maoni tofauti ndani ya mfumo wa sheria. Punguza presha inayoweza kulipuka


5.4 Kushirikisha Vijana

Anzisha majukwaa ya mazungumzo kwa vijana. Jibu hoja zao kwa ukweli na uwazi, na wajumuishe katika mipango ya kiuchumi na kisera


5.5 Kurekebisha Taswira ya Kimataifa

Mwachie mwenyekiti wa CHADEMA, mhe. Tundu Lissu bila masharti. Kuendelea kumshikilia ni kujitia doa kimataifa. Jenga msingi wa uwajibikaji wa ndani na diplomasia kueleza hali halisi. Jenga tena imani ya washirika wa kimataifa



6. FINAL INTELLIGENCE JUDGMENT

Tanzania haiko kwenye hatari ya kuanguka mara moja, lakini iko kwenye critical transition phase yenye hatari ya kupoteza uhalali wa kisiasa na kuchochea mgogoro wa ndani hususan kati ya Watanganyika na Wazanzibari. Hatari kuu si maandamano wala upinzani, bali ni kuporomoka kwa imani ya wananchi, kumong’onyoka kwa umoja wa kitaifa, kushindwa kwa serikali kudhibiti simulizi


Endapo hatua za kurekebisha hazitachukuliwa mapema: hali inaweza kuingia kwenye mzunguko wa mzunguko wa kutokuwa na utulivu → ukandamizaji → kuongezeka kwa kutokuwa na utulivu.”


ANGALIZO

Tathmini hii imejengwa kutokana na viashiria vinavyopatikana katika vyanzo vya wazi, dalili za kitabia, pamoja na mifumo linganishi ya tathmini ya hatari za kisiasa. Inashauriwa hali hiyo iendelee kufuatiliwa kwa karibu na kwa utaratibu.


Uwe na Amani

 
 
 

Comments


bottom of page