“Heri Mwisho wa Jambo Kuliko Mwanzo Wake”: Uchambuzi wa Utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan
- Rev. Godwin Chilewa
- May 22, 2025
- 4 min read

“Heri mwisho wa jambo kuliko mwanzo wake” (Mhubiri 7:8). Maneno haya ya Mhubiri yamebeba uzito mkubwa kwa viongozi – hasa katika kipindi cha mpito au uchaguzi. Hii ni methali inayomuweka kwenye mizani mhe. Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na timu yake ya uongozi.
Rais SSH alipochukua uongozi wa Tanzania Machi 2021 baada ya kifo cha Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, taifa lilikuwa katika hali ya sintofahamu. Hata hivyo, mwanzo wake ulitafsiriwa na wengi kuwa wa matumaini, maridhiano na mageuzi ya kidiplomasia. Lakini pengine swali wanalojiuliza watu wengi hivi leo ni kama matumaini hayo bado yapo, au yameyeyuka kama samli kwenye kikaango?
Rais Samia Suluhu Hassan aliingia madarakani akiwa na maono chanya ikiwa pamoja na mtazamo wa kupunguza misuguano ya kisiasa na kuboresha uhusiano wa kimataifa. Alifungua milango ya mazungumzo na viongozi wa upinzani, akaruhusu mikutano ya hadhara, na kuchukua hatua za kurejesha taswira njema ya Tanzania kimataifa baada ya kipindi cha kutengwa kidiplomasia. Hii ilileta matumaini mapya kwa Watanzania na jumuiya ya kimataifa.
Katika sekta ya uchumi, alizindua Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 (Tanzania COVID-19 Socio-Economic Response Plan), alifanikisha kupatikana kwa fedha kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF), na alisafiri mara nyingi nje ya nchi ili kutafuta wawekezaji. Mwanamama alipambana kurudisha heshima ya Tanzania na yamkini alifanikiwa kuteka mioyo ya watu.
Kadri muda ulivyokuwa ukienda mtazamo wa Rais Samia ulianza kubadilika, hali iliyofanya wananchi waanze kujiuliza maswali. Licha ya misaada kutoka kwa wahisani, hali ya maisha imezidi kuwa ngumu kwa wananchi hasa wa hali ya chini. Gharama za bidhaa zimepanda, thamani ya shilingi imeshuka, huku tozo na kodi zikiwa zimeongezeka kwa kiwango kinachotishia uhai wa biashara ndogo ndogo. Wananchi wanalalamikia matumizi yasiyo na tija ya fedha za walipa kodi na mikopo huku miradi mingi ikionekana kuchelewa au kutokuwa na athari za moja kwa moja kwa maisha ya wananchi.
Mbaya zaidi ni pale yalipoanza kujitokeza matukio ya mara kwa mara ya mauaji ya kutatanisha, utekaji, na ongezeko la uhalifu usio wa kawaida. Wananchi wakaingizwa katika sintofahamu kwa wasiwasi kwa kuona hali ya usalama imeyumba ukilinganisha na kipindi cha nyuma cha uongozi wa SSH ambapo utulivu ulitawala. Ukosefu wa mawasiliano ya wazi kutoka serikalini kuhusu matukio hayo umeongeza sintofahamu hiyo kwa kiasi kikubwa.
Hali ya siasa nayo imezidi kuwa mbaya. Licha ya kuanza kwa mikutano ya hadhara, matumaini ya mageuzi ya kweli ya kisiasa yamefifishwa tena. Viongozi wa upinzani wamejikuta wakikumbana na vitisho na vizuizi. Mchakato wa katiba mpya – uliokuwa kiini cha matumaini kwa wengi – umetumbukia kwenye ukimya, huku uchaguzi wa Serikali za Mitaa ukisheheni malalamiko ya uvunjaji wa haki. Watanzania wanahoji uhuru wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwani bado hakuna mabadiliko ya kisheria yaliyofanyika kuhakikisha uhuru wactume hiyo. Mchakato wa uchaguzi unaonekana kutayarishwa katika mazingira yanayolenga kuipa ushindi CCM.
Si hivyo tu bali pia kiongozi wa chama kikuu cha upinzani CHADEMA wamekuwa wakisumbuliwa na kupigwa bila sababu za msingi. Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani mhe. Tundu Lisu amekamatwa na kutupwa gerezani kwa mashtaka yanayotafsiriwa kuwa ya kisiasa. Tukio hili limetikisa imani ya wapinzani na wanaharakati wa haki za binadamu kwani Lissu alikuwa mfano wa maridhiano ya kisiasa, hivyo hatua dhidi yake imetafsiriwa kama “kujenga daraja kwa upande mmoja tu.”
Kidiplomasia, ingawa serikali ya SSH ilianza na diplomasia ya kuifungua Tanzania na kuikaribisha dunia, hali imebadilika. Tukio la kuwazuia kuingia nchini wanasheria kutoka Kenya waliotaka kuhudhuria kesi ya Tundu Lissu limeibua taharuki kubwa. Mataifa ya nje na hasa watetezi wa haki za binadamu wanaona kama ishara ya hofu ya wazi na kudhoofisha taswira ya Tanzania kama taifa linaloheshimu uhuru wa mahakama na sheria.
Nazo ziara nyingi za Rais Samia, nje ya nchi ambazo mwanzoni zilionekana kuwa za matumaini, sasa zimeanza kuonekana kama mzigo kwa mlipa kodi. Matokeo ya kidiplomasia yanayoonekana kuwa haba ukilinganisha na matumizi makubwa. Baadhi ya wawekezaji wanaeleza kukatishwa tamaa na urasimu na ukosefu wa uwazi.
Ili kulinda heshima, jina lililotukuka, historia njema na kuhakikisha mwisho wa utawala wake hauharibu matumaini aliyojenga mwanzoni, Rais Samia anapaswa kuchukua hatua za haraka kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza. Hatua hizo ni pamoja na kusikiliza malalamiko ya wananchi na kuyatatua kwa haki na uwazi.
Hivi sasa wananchi wana malalamiko mengi hususan kuhusu usalama wao. Watu wanatekwa, kupotea na kuuawa katika mazingira yasiyo ya kawaida. Pamoja na kujua hili mhe. Rais ameelekea kulipuuza tatizo hili hali inayofanya wananchi waamini yeye ndiye yuko nyuma ya utekaji huo. Jambo hili linamfanya afananishwe na Idd Amin na madikteta wengine waliotsngulia. Ni muhimu sana Rais achukue hatua kukomesha matukio haya kurejesha matumaini ya wananchi na kulinda amani na usalama wa Taifa.
Rais pia anapaswa kufanya mageuzi katika vyombo vya usalama. Kuongeza uwazi, uadilifu na mawasiliano ya haraka kuhusu masuala ya usalama wa taifa. Hivi sasa idara ya Usalama wa Taifa inaongozwa na mkurugenzi mwenye uwezo mkubwa, maono na mtazamo chanya. Hata hivyo zipo taarifa kwamba ushauri wake haisikilizwi na badala yake watu wasio na taalumavya intelijensia ndio wamekuwa washauri wakuu. Jambo hili ni hatari na huwenda ndilo linalosababisha watumishi wa serikali wenye hasira kuvujisha taarifa nyeti mitandaoni. Hali hii iliyoshamiri katika kipindi cha Rais Magufuli imeanza kujirudia na ni dalili ya kukata tamaa kwa watendaji wa serikali.
Rais anapaswa kuwawajibisha viongozi wanaochafua jina la serikali kwa ubadhirifu na rushwa. Uwajibikaji wa kweli utarejesha imani. Zipo tuhuma nyingi zenye ushahidi zinazothibitisha ubadhirifu, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. Mheshimiwa Rais anapaswa kuchukua hatua za haraka na sahihi kukomesha hali hii.
Ni muhimu pia mhe. Rais alipe kipaumbele suala la kufufua mchakato wa Katiba mpya. Huu ni msingi wa umoja wa kitaifa na maridhiano ya kisiasa. Katiba iliyopo inawapa watawala mwanya wa kutumia madaraka vibaya bila kudhibitiwa, na pia inabana baadhi ya haki za msingi za watanzania.
Pia kuna umuhimu mkubwa kwa mhe. Rais kupunguza safari zisizo za lazima na kuweka vipaumbele vya maendeleo ndani ya nchi. Hili linapaswa kwenda sambamba na kupunguza matumizi ya serikali na udhibiti wa wizi wa kodi za wananchi. Dunia inaheshimu nchi inayojiheshimu kwa nidhamu ya matumizi. Katika miaka ya karibuni CAG amekuwa akitoa taarifa zinazoonesha udhaifu mkubwa katika udhibiti wa mapato ya serikali. Rais anapaswa kuchukua hatua kudhibiti hali hii.
Ni jambo lisilopingika kwamba , “heri mwisho wa jambo kuliko mwanzo wake,” Mtu anaweza kuanza vizuri lakini akamaliza vibaya, au akaanza vibaya na kumaliza vizuri. Mahali Tanzania ilipofikia si pabaya sana, lakini si pazuri kiuchumi, kidiasa, kiusalama na kijamii. Mabadiliko chanya yanahitajika haraka. Lakini hilo linawezekana tu kwa uongozi unaotathmini njia yake na kufanya marekebisho. Rais Samia bado ana nafasi ya kurekebisha hali. Historia itamhukumu kwa namna atakavyoshughulikia changamoto hizi na kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa nchi ya amani, umoja, maendeleo na haki.
Rev. Godwin Chilewa






Comments