top of page

Huisha Uwezo wa Kufikiri Kwako



Akili ni uwezo wa mtu kuelewa na kupambanua mambo, au kwa kifupi ufahamu. Akili humsaidia mwanadamu kujielewa yeye mwenyewe, wenzake, na mazingira yanayomzunguka kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali za maisha ili aweze kuishi vizuri. Mtu mwenye akili/ ufahamu mkubwa huweza kupata mafanikio makubwa katika jamii kuliko yule mwenye ufahamu duni. Hata hivyo mafanikio hayo hutegemea mazingira na aina ya watu anaoishi nao.


Kwa ujumla hakuna kipimo sahihi cha kupima akili. Wanasayansi hutumia vipimo mbalimbali kama Binet-Simon Scale, US Army Alpha na Beta Tests kupima uwezo wa kufikiri wa mtu yaani Intelligence Quotient (IQ) kwa kulinganisha na wastani wa watu wengine wa umri wake. Hata hivyo vipimo hivyo huwa havithibitishi kwa hakika uwezo wa akili ya mtu, na mara nyingine hutoa majibu yasiyo sahihi.


Katika maisha ya kawaida wengi wetu huona alama (marks) anazopata mwanafunzi darasani, au kiwango cha ufaulu wake katika mitihani kuwa ndicho kipimo cha uwezo wake wa kiakili. Japokuwa hoja hii ni ya msingi, upo ushahidi mkubwa unaonesha kuwa si wote wanaopata alama za juu darasani, au kusoma hadi kupata PhD wana uwezo mkubwa wa kiakili, na wale wanaopata alama za chini wana uwezo mdogo.



Kwa ujumla yapo mambo mengi yanayoweza kumfanya mwanafunzi kutofanya vizuri katika masomo. Mambo hayo ni pamoja na mazingira anayoishi na ya shuleni, uwezo wa walimu wanaomfundisha, interest ya mwanafunzi katika mada anayofundishwa, msongo wa akili unaomkabili, na mambo mengine yaliyoijaza akili yake.


Si ajabu tajiri Bill Gates amefanikiwa kujenga himaya kubwa ya biashara kiasi cha kuwa bilionea japokuwa alikatiza masomo yake mapema. Si ajabu pia kuwa bilionea huyo leo hii ndiye anayeongoza mkakati wa utengenezwaji chanjo ya ugonjwa wa COVID19 japokuwa hana shahada yoyote ya utabibu (udaktari). Kumbe kinachomfanya mtu kuwa na ufahamu mkubwa si alama alizopata darasani, au cheti alichonacho, bali uwezo wake wa kupokea elimu mpya, na mambo mapya, na kuyatumia kuboresha maisha yake kulingana na wakati na mazingira yake.


Ni kwa sababu hii Yesu aliwaambia wayahudi ”Watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; na wakifanya hivyo viriba hupasuka, divai ikamwagika, na viriba vikaharibika; bali hutia divai mpya katika viriba vipya, na vyote vikahifadhika salama” (Mathayo 9:17). Yesu alisema maneno haya kuwaonya mafarisayo, waandishi na walimu wa sheria waliokuwa wakimhoji na kukosoa mafundisho yake.


Kimsingi mafarisayo waandishi, na walimu wa sheria walikuwa ndio watu wanaoheshimika kwa kuwa na ufahamu mkubwa, na elimu ya juu kabisa katika dini na sheria ya Musa (torati) iliyokuwa ikitumika kuwaongoza waisraeli. Licha ya kuzishika amri kumi za Mungu kama zinavyotajwa katika sura ya 20 ya kitabu cha Kutoka, mafarisayo pia walizishika sheria nyingine 640 na mapokeo chungu mzima kutoka kwa baba zao.



Jambo la kusikitisha ni kuwa mlundikano wa mambo hayo katika akili na mioyo yao, uliwafanya kuzingatia zaidi mambo ya mwilini (sheria) na hivyo kushindwa kupokea mambo ya ROHONI na neno la uzima kutoka kwa Yesu kristo, aliyetumwa kuwakomboa kutoka katika laana ya torati (Warumi 10:4, Luka 24:44-49, Waebrania 8:10-13) Ni kwa sababu hiyo Yesu aliwafananisha na kiriba cha zamani kisichoweza kupokea mvinyo mpya.


Kumbe ili tuweze kuishi maisha mapya, ya wokovu, neema na baraka tele ni lazima tuzihuishe akili zetu na mioyo yetu, iwe mipya kama kiriba kipya kilicho tayari kupokea mvinyo mpya. Miaka mingi iliyopita mfalme Daudi alimwimbia Mungu zaburi akisema “Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu” (Zaburi 51:10). Mfalme Daudi alisema hayo akijua kuwa ili aweze kufanikiwa katika maisha ya kimwili, kiroho na kiakili, ni lazima awe na moyo safi, na roho mpya yenye utayari wa kupokea neema mpya.


Kumbe sisi pia tunapaswa kuihuisha mioyo yetu, roho zetu na akili zetu kwa kuzifanya mpya kila siku ili ziweze kupokea neema na rehema za BWANA ambazo ni mpya kila siku asubuhi (Maombolezo 3:22-25). Hebu zitafakari njia zako na mipango yako. Angalia unakwama wapi? Jiulize kwa nini mambo hayaendi sawa? Je wokovu wako una thamani ya upya au umechakaa kiroho?


Kama unajiona wokovu wako umefubaa jiulize ni kwa sababu gani. Pengine umeokoka siku nyingi kiasi cha kuuona wokovu kama kitu cha kawaida tu. Pengine hata toba unaifanya kwa mazoea, na kuwasamehe wengine kwako imekuwa msamiati. Pengine mazoea yamekukokota na kukurudisha kwenye tabia mbaya ulizokuwa umezizoea, na sasa huzioni kama ni tatizo tena kwa sababu unajiona umeokoka. Umekubali kuwa kiriba cha kale!



Tafakari pia maendeleo yako ya maisha ya kimwili na kiakili. Jiulize, Je! Maisha yako ni ya mafanikio? Unayapimaje mafanikio yako? Malengo yako yanatimia? Kama sivyo jiulize kwa nini hayatimii? Pengine ni kwa sababu bado umeng’ang’ana na ndoto za zamani, mipango ya zamani, na mitazamo ya kizamani isiyoendana na wakati tulionao. Kama ni hivyo badilisha namna yako ya kufikiri. Muombe roho mtakatifu akuongoze katika kujiwekea malengo mapya na ndoto mpya zinazotekelezeka.


Pengine umewahi kusikia kuwa Yesu ni yuleyule jana, leo na hata milele na hivyo ukadhani Yesu ni wa zamani. Si kweli! Yesu si wa zamani kwa maana yu hai (hachakai). Yesu ni yule yule kwa sababu ni MPYA kila siku, na neno lake ni jipya kila iitwayo siku.


Ni kwa sababu hii unapaswa usibweteke na wokovu wa zamani, ufanye mpya ili ukufikishe mbinguni. Usibweteke na ndoa yako ya miaka mingi, bali iboreshe ili kila siku ndoa yako iwe ya furaha na amani kama imefungwa leo. Tena usikubali maisha yako yachakae na kukosa thamani. Yaboreshe kwa kufanya mipango mipya, kuwa na ndoto mpya, na wekeza katika mambo mapya. Kuwa kiriba kipya kilicho tayari kupokea neema mpya kila siku kutoka kwa mfalme wa wafalme.


Mungu akubariki, uwe na amani.

Rev. Godwin Chilewa



Comments


bottom of page