Vita Vinavyoendelea DRC: Nani Anatawala?
- Rev. Godwin Chilewa
- 5 hours ago
- 3 min read
Na. Godwin Chilewa

Mgogoro unaoendelea mashariki mwa DRC umeingia hatua mpya ya hatari, ambapo vita vya wazi, siasa za kimataifa, na maslahi ya rasilimali zimeungana kuunda mgogoro tata zaidi barani Afrika kwa sasa. Licha ya juhudi za kimataifa hususan zile zilizoongozwa na Rais Donald Trump hali ya amani bado ni tete na inazidi kudhoofika.
Kwa sasa, hali ya kijeshi mashariki mwa DRC imegawanyika katika makundi kadhaa: Waasi wa M23, wanaoungwa mkono na Rwanda, bado wanadhibiti maeneo makubwa ya Kivu Kaskazini na Kusini. Ikumbukwe kuwa mwaka 2025, M23 waliteka miji muhimu kama Goma — kitovu kikuu cha biashara na usafirishaji wa mashariki.
Majeshi ya serikali ya DRC (FARDC) yamefanikiwa kurejesha baadhi ya maeneo kama Uvira, lakini bado kuna uwepo wa waasi pembezoni mwa mji huo, huku makundi ya wanamgambo wanaoiunga mkono serikali kama Wazalendo na FDLR pia yanahusika moja kwa moja vitani.
Kwa ujumla, hakuna upande wenye udhibiti kamili kwani hali ni ya “vita vya kusukumana” ambapo maeneo hubadilika mara kwa mara. Ripoti za karibuni zinaonyesha kuwa mapigano yanaendelea licha ya makubaliano ya kusitisha vita. Aidha, pande zote mbili, serikali, M23, na washirika wao zinatuhumiwa kukiuka makubaliano ya amani.
Kuna ushahidi wa uwepo wa wanajeshi wa Rwanda kati ya 14,000 hadi 18,000 ndani ya DRC, wakisaidia M23. Hali hiyo inafanya mashambulizi ya anga (drone strikes), mauaji ya raia, na uporaji wa rasilimali kuendelea. Hii inaonyesha wazi kuwa vita hivi vina sura ya vita vya kikanda (proxy war).
Juhudi za Donald Trump zimeleta mikataba miwili mikuu ya amani (Juni na Desemba 2025), ikiwa ni pamoja na kusitisha vita, na ushirikiano wa kiuchumi (hasa madini muhimu kama cobalt na coltan). Hata hivyo waasi wa M23 wanadai Marekani si mpatanishi wa haki na Rwanda inaendelea kushukiwa kuunga mkono waasi licha ya makubaliano.
Kimsingi makubaliano hayo yanaonekana kuhusisha maslahi ya rasilimali (“peace for minerals”). Kwa maneno mengine, diplomasia imechanganyika na maslahi ya kimkakati ya kiuchumi. Hii inafanya mambo yawe tata zaidi kwani waasi wa M23 na washirika wao wanachotaka ni kutambuliwa kisiasa, kushirikishwa kwenye utawala, na wanapinga baadhi ya makubaliano ya Washington.
Mbaya zaidi ni kwamba waasi hawa Wanaendelea kujipanga kijeshi na hata kuajiri wapiganaji wapya. Hii inaashiria kuwa hawako tayari kwa suluhisho la haraka la kisiasa.
Wakati haya yote yakiendelea jina la Joseph Kabila linaendelea kutikisa siasa za DRC. Ingawa rais huyo wa zamani wa DRC amewekewa vikwazo na Marekani kwa madai ya kuunga mkono M23 bado anaendelea na mikakati yake. Ikumbukwe kuwa miezi michache iliyopita Mahakama ya kijeshi ya DRC ilimhukumu Joseph Kabila kifo kwa tuhuma za uhaini na uhalifu wa kivita
Bwana Kabila anadaiwa kuwa na ushawishi mkubwa kisiasa na kijeshi, hasa mashariki
Ingawa yeye mwenyewe anakanusha, wachambuzi wengi wanaamini bado ana mtandao mkubwa unaochochea mgogoro.
Swali wanalojiuliza wengi kwa sasa ni hili: Je, amani iko karibu? Kwa hali ilivyo sasa hali ni tete na vikwazo ni vingi. Vikwazo hivyo ni pamoja na mzozo wa kumiliki maeneo ya rasilimali (madini ya thamani), ushiriki wa mataifa jirani (hasa Rwanda), uwepo wa makundi zaidi ya 100 ya wanamgambo, na kukosekana kwa imani kati ya pande husika
Ukweli huu unajionesha wazi kwani makubaliano ya amani yanakiukwa mara kwa mara, mapigano yanaendelea, huku wakimbizi na mateso ya raia yanaongezeka. Kwa tathmini ya sasa, amani ya kudumu bado iko mbali.
DRC imekuwa uwanja wa mgongano wa maslahi ya ndani na ya kimataifa kwa zaidi ya miongo mitatu. Vita vya sasa vinaonyesha serikali dhaifu inayopambana kurejesha mamlaka, huku waasi wenye nguvu wanaoungwa mkono nje wakikaidi makubaliano ya amani na mataifa makubwa yakivutiwa zaidi na rasilimali kuliko amani halisi ya DRC.
Bila mabadiliko ya kimsingi hasa kuondoka kwa ushawishi wa nje na suluhisho la kisiasa linalojumuisha pande zote mgogoro huu utaendelea kuwa “vita visivyoisha” badala ya safari ya kuelekea amani.
Uwe na amani






Comments