Tanzania: Kutoka Taifa la Maono Hadi Maandamano na Mauaji. Tumefikaje Hapa?
- Rev. Godwin Chilewa
- 1 day ago
- 4 min read
Na. Godwin Chilewa

Kwa miongo kadhaa baada ya uhuru, Tanzania ilisimama kama taa ya matumaini barani Afrika. Chini ya uongozi wa Julius Nyerere, taifa lilijijengea heshima kubwa kimataifa kwa misingi ya siasa za ujamaa, mshikamano wa kijamii, na mchango wake katika harakati za ukombozi wa bara la Afrika. Tanzania ilikuwa nchi, wazo, mfano wa maadili, utu, na uongozi wenye dhamira.
Leo, taswira hiyo imechakaa. Malalamiko yameongezeka: rushwa imekithiri, pengo kati ya matajiri na maskini limepanuka, na wananchi wengi wanahisi kutengwa na matunda ya uchumi. Wimbo umebadilika toka taa ya matumaini hadi maandamano ya risasi. Swali linabaki: nini kimeifikisha Tanzania hapa? Je, ni hujuma za nje, ubovu wa viongozi, au uzembe wa wananchi wenyewe?
Chanzo kikuu kinachoonekana wazi ni mmomonyoko wa maadili ya uongozi. Tofauti na kizazi cha mwanzo cha viongozi waliotanguliza taifa mbele ya maslahi binafsi, sehemu ya uongozi wa sasa imejikuta ikiendeshwa na tamaa ya mali, madaraka, na ushawishi. Rushwa haionekani tena kama aibu bali kama “njia ya mkato” ya mafanikio.
Tatizo hili si la mtu mmoja bali mfumo mzima. Tangu pale viongozi walipoamua kutupilia mbali Miiko ya Uongozi, na kuleta Azimio la Zanzibar nchi ikawa kama imeingia kwenye laana.Taasisi zinazopaswa kusimamia uwajibikaji zimekuwa dhaifu au zimetekwa na maslahi ya kisiasa. Ufisadi umekuwa mtindo wa maisha. Pale ambapo sheria haifanyi kazi kwa usawa, haki hupotea na taifa huanza kudorora.
Ni ukweli usiopingika kwamba hatua ya kutoka ujamaa kwenda uchumi wa soko huria ilikuwa muhimu, lakini utekelezaji wake haukujengwa juu ya misingi thabiti ya kulinda maslahi ya wananchi wote. Ubinafsishaji wa mali za umma mara nyingi haukuleta tija iliyotarajiwa; badala yake, ulihamisha utajiri mikononi mwa wachache.
Matokeo yake ni uchumi unaokua kwa takwimu, lakini usiogusa maisha ya wananchi wengi. Vijana wanahitimu bila uhakika wa ajira, wakulima wanabaki maskini licha ya kufanya kazi kwa bidii, na huduma za kijamii zinakuwa ghali au duni. Maisha ya mwananchi wa kawaida yamekuwa magumu mno.
Mara nyingine ni rahisi kulaumu viongozi pekee, lakini ukweli ni kwamba jamii nzima imeathirika. Uzalendo uliowahi kuwa nguzo ya taifa umedorora. Wananchi wengi wamezoea kukubali hali ilivyo badala ya kudai mabadiliko. Wengine wanashiriki moja kwa moja katika vitendo vya rushwa kutoa au kupokea—kwa sababu ya tamaa au kukata tamaa. Vijana wanapoteza muda kwenye kubeti na kuangalia tamthiria badala ya kufuatilia haki zao kwa umakini.
Ukweli mchungu ni kwamba demokrasia haiwezi kufanya kazi bila wananchi wenye uelewa, ujasiri, na maadili. Pale wananchi wanaponyamaza au kushiriki katika uovu, wanachangia kuendeleza tatizo. Wananchi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kukataa maovu kwa vitendo.
Lipo pia tatizo la shinikizo la nje na mwelekeo wa kimataifa. Katika ulimwengu wa leo, nchi haziishi peke yake kama kisiwa cha Kusadikika. Mashinikizo ya kiuchumi na kisiasa kutoka nje yanaathiri maamuzi ya ndani. Mikopo, misaada, na mikataba ya kimataifa mara nyingine huja na masharti yanayoweza kudhoofisha uhuru wa sera za kitaifa.
Hata hivyo, hoja ya “hujuma za nje” haiwezi kuwa kisingizio cha kudumu. Nchi yenye taasisi imara na uongozi thabiti inaweza kujilinda na kusimamia maslahi yake ipasavyo. Tatizo ni pale misaada na mikopo inayotolewa kutumika kwa malengo yasiyokusudiwa, kisiasa, na kwa maslahi binafsi. Aidha uingiaji wa mikataba mibovu limekuwa donda ndugu kwa taifa.
Pengine utajiuliza’ “Nani wa kulaumiwa? Jibu la kweli haliegemei upande mmoja. Ni mchanganyiko wa mambo: Viongozi waliokosa maadili na dira, mfumo usio na uwajibikaji wa kutosha, wananchi waliopoteza nguvu ya kudai haki na kushiriki kikamilifu, na mazingira ya kimataifa yanayoongeza changamoto. Kwa ujumla, lawama ni ya pamoja. Hata hivyo si kwa kiwango sawa. Uongozi una nafasi kubwa zaidi kwa sababu una mamlaka ya kufanya maamuzi na kuweka mwelekeo. Hivyo unapaswa kubeba lawama kubwa zaidi.
Je, nini kifanyike ili kurejesha hadhi ya Tanzania? Hili si jambo la siku moja, bali ni safari inayohitaji dhamira ya kweli. Ni lazima kubomoa na kujenga upya misingi ya maadili.Uongozi lazima urejee kwenye misingi ya uwajibikaji, uadilifu, na huduma kwa umma. Sheria dhidi ya rushwa zitekelezwe bila upendeleo. Na hapa ndipo linapokuja suala la Katiba mpya.
Katiba mpya ni muhimu katika kuimarisha uhuru wa Mahakama, vyombo vya uchunguzi, na taasisi za usimamizi zenye nguvu ya kuwajibisha hata walio madarakani. Mfumo uliopo sasa unampa madaraka makubwa rais wa nchi na kulipunguzia bunge uwezo wake.
Ni muhimu pia kutengeneza Sera za uchumi zinazolenga kupunguza umaskini kwa vitendo, kuwezesha wakulima, kukuza viwanda vya ndani, na kuunda ajira kwa vijana. Hivi sasa Sera nyingi zinatengenezwa kisiasa ili kuandaa majimbo na wapiga kura wa chama tawala.
Pamoja na hayo yote ni muhimu pia kufufua uzalendo na elimu ya uraia. Wananchi wafundishwe haki zao na wajibu wao. Taifa linajengwa si na viongozi pekee, bali na kila raia. Sambamba na hili mfumo wa kisiasa utoe nafasi ya ushindani wa haki, uwazi, na sauti za wananchi kusikika bila hofu.
Tanzania haijapoteza kila kitu, ila imepoteza mwelekeo. Na mwelekeo unaweza kurejeshwa. Historia ya taifa hili inaonyesha uwezo wake wa kusimama imara hata katika nyakati ngumu. La muhimu ni Watanzania kuwa tayari kufanya maamuzi magumu ili kufika huko. Bila hatua za makusudi, malalamiko yataendelea. Lakini kwa maono sahihi, katiba mpya, uongozi sahihi, taasisi imara, na wananchi wenye ujasiri, taifa linaweza tena kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika.
Uwe na amani.






Comments