top of page

Serikali Inaogopa Maandamano au Mabadiliko?

Na. Godwin Chilewa



Je, serikali inaogopa maandamano—au inaogopa mabadiliko yanayobisha hodi?

Hili ni swali ambalo kila anayefuatilia siasa na mustakabali wa Tanzania anapaswa kujiuliza. Hata hivyo kabla ya kutoa jibu rahisi ni muhimu kuangalia mambo kadha wa kadha.


Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), zaidi ya asilimia 26 ya Watanzania wanaishi chini ya mstari wa umaskini. Vijana ambao ni zaidi ya asilimia 60 ya idadi ya watu wanaendelea kukumbwa na ukosefu mkubwa wa ajira rasmi.


Wakati huo huo, gharama za maisha zimepanda kwa kasi. Bei za vyakula muhimu kama unga, mchele, na mafuta ya kupikia zimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 20 katika baadhi ya maeneo ya mijini ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita. Hizi si namba tu ni maisha ya watu wanaolazimika kuchagua kati ya kula na kulipia mahitaji mengine muhimu. Katika mazingira haya, maandamano si uchochezi ni matokeo ya maumivu.


Si hivyo tu, ukweli ni kwamba mpaka sasa hakuna Mtanzania aliyesahau matukio ya Oktoba 29, 2025, siku iliyogubikwa na umwagaji damu, ukamataji wa kiholela, na hofu iliyoenea katika maeneo mbalimbali ya nchi wakati wa uchaguzi mkuu. Ripoti za ndani na nje ya nchi zilieleza vifo vya maelfu ya raia wasio na hatia, huku wengine wakipotea au kukamatwa bila maelezo au sababu zinazoeleweka.


Matukio haya yameacha majeraha ya kimwili na hofu ya kudumu katika nafsi ya taifa. Hofu ya kuhoji. Hofu ya kukosoa. Hofu ya kudai haki.

Tatizo ni kwamba historia ina tabia moja: haiwezi kufutwa. Inaweza kunyamazishwa kwa muda, lakini wakati wowote huweza kuibuka tena kwa nguvu zaidi.


Pamoja na hilo, miaka ya karibuni, kumekuwa na hatua za wazi za kuzuia mikutano ya kisiasa, hasa kwa vyama vya upinzani. Hoja ya “usalama wa taifa” imetumika mara kwa mara kuhalalisha hatua hizi. Hata hivyo ukweli ni kwamba hoja hiyo imetumika kama sababu tu ya kuvidhibiti vyama vya siasa na kukipa ahueni chama tawala.


Wengi wamekuwa wakihoji kama kweli amani, utulivu na usalama wa taifa hujengwa kwa kuwanyamazisha wananchi wanapodai haki zao za kikatiba. Si ajabu ripoti za mashirika ya kimataifa kama Human Rights Watch na Amnesty International zimekuwa zikionya kuhusu kupungua kwa uhuru wa kujieleza na kukusanyika nchini Tanzania. Hizi si propaganda ni tahadhari kutoka kwa macho ya dunia.


Mkusanyiko wa mambo yote hayo umefanya baadhi ya wananchi na hasa viongozi wa vyama vya upinzani kuilalamikia Idara ya Usalama wa Taifa. Kimsingi Idara hii inapaswa kuwa tegemeo la mwisho la wananchi wote. Lakini pale taarifa za kiintelijensia zinapolenga zaidi kufuatilia wapinzani wa kisiasa kuliko kushughulikia changamoto halisi za kiusalama inakuwa tatizo. Watu wanajiuliza kama TISS inalinda taifa au inalinda mfumo wa kisiasa uliopo?


Matharani, kama kweli kulikuwa na onyo la vitendo vya kiadui kabla ya matukio ya Oktoba 29, kwa nini jitihada hazikufanyika kuzuia maafa? Mbona miaka ya 1980 TISS ilifanikiwa kuzima jaribio kabambe la kumpindua Rais Julius Nyerere? Tena ilifanya hivyo bila kumwaga damu wala kuleta taharuki?


Hapa ndipo baadhi ya wachambuzi hurejea kwenye kauli za tahadhari zilizotolewa na askofu Josephat Gwajima. Kwamba TISS inafanya kazi yake ipasavyo lakini ushauri wake hautiliwi maanani au unapuuzwa kwa malengo maalum, aidha baadhi ya machawa wamepora hadhi ya ushauri wa Rais hata katika mambo yanayohitaji taaluma ya ndani ya uchambuzi wa kiitelijensia.


Kwa sasa watanzania wengi, hasa vijana wa Gen Z wanapiga kelele kudai mabadiliko na kuhamasisha maandamano ya amani. Hata hivyo baadhi ya wananchi hasa wanachama wa chama tawala wako kimya. Lakini ukimya huu si ridhaa ni matokeo ya mazingira ya hofu. Hofu ya kupoteza kidogo walichonacho na kudhibitiwa na polisi. Hata hivyo, historia ya dunia inaonyesha wazi: pale wananchi wanapochoka, huamka, huungana, na kuwa na kauli moja. Na wanapoamka, hakuna nguvu inayoweza kuwazuia kwa muda mrefu.


Hasira ya wananchi ni kama moto uliofukiwa, hauonekani, lakini unaendelea kuwaka. Viongozi wanapaswa kuelewa kuwa kuzuia maandamano si suluhisho la kudumu. Ni kuchelewesha mlipuko. Taifa haliwezi kuendeshwa kwa hofu ya mtutu milele.


Kumbe suluhisho si nguvu, ni hekima. Wananchi wanataka mabadiliko ya kiuchumi na uhuru wa kisiasa bila masharti Ni vyema viongozi wawe wasikivu na kukubali kubomoa ili kujenga upya taasisi zinazojitegemea na zenye uwajibikaji. Fungueni milango ya majadiliano ya kitaifa. Wekezeni katika ajira na ustawi wa vijana. Heshimuni katiba na utawala wa sheria. Toeni nafasi kwa utawala wa haki na sheria.


Kwa sasa Tanzania iko katika wakati ambao historia itaandika kwa herufi nzito. Ama itaandikwa kama taifa lililopuuzia sauti za wananchi wake hadi likajikuta kwenye msukosuko, au kama taifa lililochagua kusikiliza, kubadilika, na kujijenga upya kwa amani.

Mabadiliko hayazuiliki. Aidha yatakuja kwa hekima au kwa gharama kubwa.


Uwe na amani

 
 
 

Comments


bottom of page