top of page

JE, TISS INAHUSIKA KWELI? Uchambuzi wa Kiitelijensia Kuhusu Tukio la Nyumbani Kwa John Heche

Updated: 1 day ago

Na. Rev. Godwin Chilewa



Katika mazingira ya kisiasa yenye joto, matukio yasiyoeleweka mara nyingi hugeuzwa haraka kuwa ushahidi wa njama kubwa. Tukio la gari jeupe lililoripotiwa kuonekana likiulizia na hatimaye kufika nyumbani kwa John Heche, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, limezua mjadala mkali. Wapo waliokimbilia kuhusisha TISS na kile kinachodaiwa kuwa jaribio la kumdhuru mwanasiasa huyo.

Hata hivyo, uchambuzi wa kitaalamu wa kiintelijensiau unaonesha kuwa hitimisho hilo linaweza kuwa la haraka.


Kwanza, ieleweke kwamba mfumo wa utendaji wa TISS (modes operandi) unafanana kwa kiasi kikubwa na taasisi nyingine za kijasusi duniani kama CIA ya Marekani au MI6 ya Uingereza. Taasisi hizi zote hukusanya na kuhifadhi taarifa (intelligence) kuhusu watu wote maarufu au wenye hadhi ya juu. Kazi hii hufanyika kwa muda mrefu na kwa kina (long-term profiling). Hivyo, haiingii akilini kwamba TISS, chombo chenye uwezo huo kushindwa kujua anuani ya John Heche na badala yake kuanza kuulizia hadharani.


Pili, kanuni za operesheni za siri (covert operations doctrine) zinaeleza wazi juu ya umuhimu wa plausible deniability, yaani uwezo wa chombo au mhusika kuweza kukataa kuhusika bila ushahidi wa moja kwa moja. Taasisi kama Mossad na FSB zimekuwa zikihusishwa na operesheni za hali ya juu ambazo haziwachi alama za wazi. Hata TISS huko nyuma imewahi kuhusishwa katika operesheni kadhaa za siri, bila uwepo wa ushahidi. Kwa hiyo tukio la aina hii, la watu kuuliza mitaani linapingana na utendaji wa idara, na pia hata kanuni hizi za msingi.


Tatu, kwa mujibu wa tafiti za RAND Corporation kuhusu intelligence tradecraft, operesheni zisizo na usiri wa kutosha huongeza “operational risk” na uwezekano wa kufichuliwa. Taasisi yenye utaalamu kama TISS haiwezi kuchagua mbinu yenye hatari kubwa ya kuonekana na kurekodiwa kirahisi na CCTV.


Nne, nadharia ya “cost-benefit analysis” inayotumika katika intelijensia inaeleza kuwa kabla ya operesheni yoyote, faida lazima izidi gharama. Katika kesi hii, gharama za kisiasa, kijamii na kidiplomasia kwa TISS zingekuwa kubwa sana ikilinganishwa na faida yoyote inayoweza kupatikana. Hii inapunguza uwezekano wa uhusika wake.


Tano, vitabu na tafiti za intelijensia kama zile za Michael Herman (mwandishi wa Intelligence Power in Peace and War) zinaonesha kuwa operesheni nyingi za kisasa hutegemea teknolojia (signals intelligence, cyber surveillance) badala ya mbinu za moja kwa moja zinazoonekana kirahisi. Hivyo, tukio hili linafanana zaidi na mbinu za watu wasio na utaalamu wa hali ya juu.


Sita, dhana ya false flag operations imeelezewa katika tafiti nyingi za kimataifa, ikiwemo zile za Brookings Institution, ambapo tukio linaweza kupangwa kwa makusudi ili kumhusisha mhusika mwingine na kuathiri taswira yake. Hii ina maana kuna uwezekano wa kuwepo kikundi cha mauaji (kama kile kilichoelezwa na Sativa) lakini kinajificha au kutumia jina la TISS. Katika mazingira ya ushindani wa kisiasa, uwezekano huu haupaswi kupuuzwa.


Saba, kwa kuzingatia mifumo ya kimataifa ya uchambuzi wa vitisho (threat assessment models), kama zinazotumika na Interpol, tukio hili linaashiria zaidi “low sophistication actors”—yaani wahusika wenye uwezo mdogo wa kitaalamu kutokana na makosa ya wazi ya kioperesheni. TISS ina maafisa, japo wachache wenye uwezo wa hali ya juu, waliofundishwa ndani na nje ya nchi ambao wangeweza kutumika kwa operesheni ya aina hii kama ni lazima.


Nane, ushahidi wa CCTV unaonesha tukio lakini hauoneshi nia (intent) wala utambulisho (attribution). Katika taaluma ya intelijensia, attribution problem ni mojawapo ya changamoto kubwa na mara nyingi hitimisho la haraka bila ushahidi thabiti husababisha makosa ya kimkakati.


Upo uwezekano mkubwa wa kuwepo kundi linalofanya kazi chafu ya kuua na kutishia wanasiasa. Hata hivyo kwa kuangalia modes operandi yake kundi hili si TISS. Maelezo ya Sativa na watu wengine waliowahi kukutana ana kwa ana na kundi hili yanaonesha udhaifu mkubwa wa kioperesheni. Hii ni dalili ya deep state.


Kwa kuhitimisha, ingawa tukio hili linapaswa kuchunguzwa kwa kina, kulihusisha moja kwa moja na TISS bila ushahidi wa kiwango cha juu wa kiintelijensia kunapingana na misingi ya uchambuzi wa kitaalamu. Ulinganisho wa utendaji wa TISS na hata mifumo ya kimataifa unaonesha wazi kuwa tukio hili halifuati alama za operesheni za taasisi za juu za ujasusi.


Katika ulimwengu wa intelijensia, ukweli mara nyingi hufichwa chini ya kelele za hisia. Ni wajibu wa wachambuzi na jamii kwa ujumla kuchagua ushahidi badala ya hisia, na mantiki badala ya tuhuma. Ni muhimu sasa kwa TISS kujisafisha kwa kufanya uchunguzi na kuiamuru Polisi kuwakamata wahalifu hao. Aidha ni wajibu wa TISS kuhakikisha viongozi wa kariba ya John Heche wanalindwa na kuwa salama kwa faida na usalama wa taifa.


Uwe na amani.

 
 
 

Comments


bottom of page