top of page

Je, Tutabaki Watazamaji Wakati Dunia Inasonga Mbele?

Na Rev. Godwin Chilewa



Dunia inakimbia kwa kasi isiyokuwa ya kawaida kuelekea mapinduzi ya teknolojia yanayobadili maisha ya mwanadamu kila siku. Hata hivyo, bara la Afrika linaonekana kubaki nyuma, likikumbwa na changamoto ambazo za kiuchumi, za kiakili na kimfumo. Sababu kuu zinazotajwa mara kwa mara ni tamaa ya madaraka, ubinafsi wa viongozi, na hali ya “usingizi wa kimkakati” miongoni mwa taasisi na jamii kwa ujumla.


Tamaa ya madaraka imegeuza siasa kuwa uwanja wa kulinda maslahi binafsi badala ya kuwa chombo cha maendeleo ya taifa. Badala ya kuwekeza kwenye elimu ya sayansi, teknolojia na ubunifu, rasilimali nyingi hutumika katika siasa za muda mfupi zisizo na matokeo ya kudumu. Ubinafsi nao umeua roho ya ushirikiano. Taifa badala ya kujengwa kwa pamoja, linavunjwa na makundi yenye maslahi binafsi. Hali ya usingizi wa kimkakati inaonekana pale ambapo viongozi na taasisi wanashindwa kuona mabadiliko makubwa yanayotokea duniani na kujipanga kuyakabili.


Wakati Afrika ikiwa katika mzunguko huu wa changamoto, dunia nyingine inaendelea mbele kwa kasi ya ajabu. Mfano hai ni mkakati wa kampuni ya teknolojia ya kimataifa, Meta Platforms, inayolenga kubadilisha kabisa namna binadamu wanavyotumia teknolojia.

Meta, chini ya uongozi wake, imeanza safari ya kuondoka kwenye utegemezi wa simu za mkononi (smartphones) na kuelekea kwenye kile kinachoitwa “next computing platform.”


Hii ni hatua kubwa inayolenga kubadilisha simu kuwa kifaa cha zamani, na kuanzisha matumizi ya miwani ya kisasa yenye uwezo wa hali ya juu (smart glasses na augmented reality glasses).

Tayari Meta imeanza na bidhaa kama Ray-Ban Meta Smart Glasses, ambazo zina uwezo wa kupiga picha, kurekodi video, kusikiliza sauti, na hata kutumia akili bandia (AI) kama msaidizi binafsi. Huu ni mwanzo tu. Lengo kuu ni kuunda miwani ambayo itaonyesha taarifa moja kwa moja machoni mwa mtumiaji kama ujumbe, ramani, mikutano, na hata mazingira ya kidigitali yatakayochanganyika na ulimwengu halisi.


Kupitia vifaa kama Meta Quest 3, Meta tayari inaweka msingi wa kile kinachoitwa metaverseulimwengu wa kidigitali unaoruhusu watu kufanya kazi, kujifunza, na kuwasiliana kwa njia ya kuzama kabisa (immersive experience). Hapa ndipo dunia inaelekea: mahali ambapo mipaka kati ya halisi na kidigitali inafutika.


Tofauti kubwa kati ya Afrika na mataifa yanayoongoza katika teknolojia si ukosefu wa rasilimali, bali ni ukosefu wa maono na uwekezaji wa kimkakati. Wakati Meta inawekeza mabilioni ya dola katika tafiti za teknolojia ya baadaye, nchi nyingi za Afrika bado zinahangaika na masuala ya msingi kama miundombinu duni, sera zisizotekelezeka, na mifumo ya elimu isiyozalisha wabunifu.


Hata hivyo, mapinduzi haya ya teknolojia hayaji bila changamoto. Moja ya hofu kubwa inayojitokeza ni suala la faragha (privacy). Miwani hii ya kisasa ina uwezo wa kurekodi kila kinachoonekana mbele ya mtumiaji, jambo linaloweza kusababisha watu kurekodiwa bila ridhaa yao. Aidha, ikiwa teknolojia ya utambuzi wa nyuso (facial recognition) itaunganishwa kikamilifu, inaweza kufungua mlango wa ufuatiliaji wa watu kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.


Zaidi ya hayo, data binafsi itakusanywa kwa kiwango kikubwa zaidi, kuanzia unachoangalia, unakoenda, hadi watu unaowasiliana nao. Hii inaleta maswali makubwa kuhusu nani anamiliki taarifa hizo na zinatumika vipi. Hatari ya udukuzi (hacking) pia inaongezeka, kwani mtu anaweza kuvamia mfumo na kuona au kusikia kupitia kifaa cha mtumiaji.


Licha ya changamoto hizi, ukweli unabaki kuwa dunia haiwezi kusimama. Mataifa na makampuni yanayowekeza leo katika teknolojia ndiyo yatakayodhibiti uchumi wa kesho. Hii ndiyo sababu kampuni kama Apple na Google pia zinawekeza katika teknolojia mbadala wa simu za mkononi.


Swali tunalopaswa kujiuliza Waafrika ni kama bara letu litakuwa sehemu ya mapinduzi haya au litaendelea kuwa mtazamaji na mtumwa wa nchi za magharibi kama karne zilizopita. Bila mabadiliko ya fikra, uwekezaji katika elimu ya sayansi na teknolojia, na uongozi unaoweka mbele maslahi ya taifa, bara hili litaendelea kubaki nyuma huku dunia ikiendelea kusonga mbele kwa kasi.


Ni wakati wa Afrika kuamka. Ni wakati wa viongozi wetu kujitafakari na kuacha ubinafsi. Ni wakati wa kuwaamsha watu wetu. Dunia inasonga mbele, na haingoji mtu yeyote. Tusipochukua tahadhari tutakuwa watumwa kuliko wale wa karne zilizopita.


Uwe na amani.

 
 
 

Comments


bottom of page