MAKONDA na Kisa cha Mfalme Nebukadreza
Na Rev. Godwin Chilewa

Kama wewe ni msomaji wa Biblia bila shaka unakifahamu kisa cha Mfalme Nebukadreza (Danieli 5), Mfalme huyu kwa kiburi cha mamlaka aliyokuwa nayo alitumia vibaya vyombo vya dhahabu vilivyotolewa katika madhabahu ya Mungu, akavifanya kuwa chombo cha kujitukuza mbele ya wageni wake. Kitendo hicho hakikuwa kosa la kawaida; kilikuwa ni kuvuka mipaka ya mamlaka, kuchukua kilicho kitakatifu na kukigeuza kuwa nyenzo ya utukufu wa kisiasa. Ndipo maandishi ya hukumu “Mene, Mene, Tekel, na Pelesi yalipojitokeza ukutani, ishara kwamba mamlaka inapovuka mipaka ya maadili, hujikuta katika hatari ya kuanguka ghafla.
Katika muktadha wa sasa wa Tanzania, kauli ya Waziri Paul Makonda dhidi ya Kanisa la KKKT akilitaka kuacha “kuinyooshea serikali kidole” na kujikita katika maombi pekee inaakisi kwa namna ya kisasa simulizi hilo la Nebukadreza. Siyo kwamba kauli hiyo ni sawa moja kwa moja na tendo la kale, bali inabeba mantiki ile ile: jitihada ya kupunguza au kudhibiti mamlaka ya kiroho (moral authority) na kuiweka chini ya matakwa ya mamlaka ya kisiasa. Kwa lugha ya kiintelijensia, hili ni jaribio la “reframing institutional roles” ili kuondoa ukosoaji unaoweza kuathiri simulizi rasmi ya dola.
Katika namna isiyokuwa ya kawaida Makonda aliwataka viongozi wa kanisa kuacha kulaumu au kukosoa serikali na badala yake wazidishe maombi, akisisitiza kuwa kanisa “halina sifa ya kunyoosha kidole.” Kauli hii, kwa uchambuzi wa kina, si tu mjadala wa kidini bali ni hatua yenye athari za kisiasa, kijamii na kidiplomasia.
Kihistoria, Biblia haijaweka kanisa au manabii kuwa watazamaji kimya wa mamlaka. Kinyume chake, maandiko yanathibitisha wajibu wa kinabii wa kukemea uovu. Nabii Nathani alimkemea Mfalme Daudi (2 Samweli 12), Eliya akasimama dhidi ya Ahabu (1 Wafalme 18), na Yohana Mbatizaji akamkosoa Herode hadi kufa kwake. Hii inaweka kanuni isiyopingika: mamlaka ya kisiasa hayako juu ya maadili. Hivyo, kudai kuwa kanisa lina wajibu wa kuomba tu bila kukemea ni kupunguza nusu ya wito wake wa msingi.
Kwa mtazamo wa ndani ya nchi, kauli hii inaweza kuzalisha athari kadhaa za kimkakati. Kwanza, inaweza kuongeza ufa kati ya dola na taasisi za dini, ambazo kwa muda mrefu zimekuwa nguzo ya utulivu wa kijamii. Pili, inaweza kuchochea “silent resistance” yaani upinzani wa kimya unaojengeka ndani ya jamii na ambao mara nyingi hulipuka ghafla bila tahadhari. Tatu, inahatarisha mfumo wa uangalizi wa kijamii (informal oversight) unaotolewa na taasisi za dini, hasa pale ambapo mifumo rasmi ya uwajibikaji haijakomaa kikamilifu.
Zaidi ya hayo, historia ya kauli za viongozi wa umma inaonesha kuwa matamshi yana uzito wa kisiasa na kijamii. Vyombo vya habari vimekuwa vikionya kuwa kauli za Makonda katika nyakati tofauti zimekuwa zikizua mijadala na athari pana kwa jamii, zikionesha nguvu ya “neno la mamlaka” katika kuunda au kuvunja mshikamano wa kitaifa. Hivyo basi, kauli dhidi ya kanisa haiwezi kuchukuliwa kama maoni ya kawaida bali kama ishara ya mwelekeo wa sera na mtazamo wa dola.
Katika ngazi ya kimataifa, athari ni pana zaidi. Tanzania imejijenga kwa muda mrefu kama taifa lenye uvumilivu wa kidini na utulivu wa kisiasa. Hata hivyo, ishara zozote za kubana uhuru wa taasisi huru ikiwa pamoja na dini huweza kufasiriwa kama dalili ya “authoritarian drift.” Aidha, katika mazingira ya baada ya matukio ya Oktoba 29, 2025, ambapo kumbukumbu za mvutano wa kisiasa bado ziko hai, kauli ya aina hii inaweza kuibua tahadhari kwa washirika wa maendeleo, wawekezaji na taasisi za haki za binadamu.
Kimkakati, taasisi za dini hufanya kazi kama “early warning systems” katika jamii. Zinapotoa kauli au tahadhari, mara nyingi zinakuwa zimechunguza hisia za wananchi kwa kina zaidi kuliko taasisi za serikali. Kuzinyamazisha ni sawa na kuzima kengele ya tahadhari kabla ya hatari haijatokea. Hili linaweza kusababisha serikali kukosa taarifa muhimu za mapema kuhusu hali halisi ya jamii.
Kwa kurejea simulizi ya Nebukadreza, somo kuu halikuwa tu adhabu ya kifalme, bali ni onyo la kudumu: mamlaka inapochanganya mipaka ya kiroho na kisiasa kwa faida yake, hujenga mazingira ya anguko lake lenyewe. Vivyo hivyo, jaribio lolote la kulinyamazisha kanisa au kulipunguza jukumu lake linaweza kuzaa matokeo kinyume na yaliyokusudiwa kuongeza mvutano badala ya kuupunguza.
Kwa ujumla, kauli ya Makonda inapaswa kuangaliwa si kama tukio la mtu mmoja, bali kama dalili ya mvutano mkubwa kati ya dola na dhamiri ya taifa. Biblia, historia na siasa za kisasa zote zinakubaliana katika jambo moja: jamii yenye afya ni ile ambayo mamlaka ya kisiasa na sauti za maadili zinakaa katika uwiano, badala ya ukimya wa kulazimishwa. Pale ambapo uwiano huo unapovunjika, maandishi huanza kuandikwa ukutani na mara nyingi, huchelewa kusomwa.
Sambamba na hilo pia tuwakumbushe wale waliompa Bw. Makonda nafasi ya kulidharilisha kanisa wazingatie umuhimu wa kulinda utakatifu wa nyumba ya Bwana. Ni dhahiri kwamba anguko la Nebukadreza halikuwaacha salama wale waliomuandalia vinono na divai kwenye vyombo vya madhabahu. Halikadhalika ukengeufu wowote unaoweza kuipa mamlaka utukufu kuliko Mungu ni hatari kwa viongozi wa kanisa na taifa zima.
Tunawakumbusha viongozi wetu kuzingatia mipaka yao na kuacha kulidhibiti kanisa. Katika lugha ya kiintelijensia: unapodhibiti dhamiri ya taifa, huchezi tu na dini unacheza na uthabiti wa mfumo mzima wa dola.






Comments