top of page

Kama Rais Wetu Angekuwa Pilato - Angemsulubisha Yesu?


Watu wengi wanapozungumzia Kifo cha Yesu hukitazama kwa jicho la kiroho tu. Husema Yesu alisulubiwa kwa sababu ya dhambi zetu, kwa maana imeandikwa “Kwa kupigwa kwake sisi tumepona” (Isaya 53:5 Soma pia Yohana 3:16) Ni kweli kwamba kiimani Yesu alisulubiwa ili kutuletea ukombozi. Hata hivyo, ni muhimu pia kuitazama hali ya kisiasa na mazingila yaliyochangia kuhukumiwa kifo kwa mtu huyu mwenye haki. Na hapo ndipo tunapopaswa kujiuliza swali hili “Kama Rais wetu angekuwa ndiye Pontio Pilato, Je, naye angeamtoa Yesu auawe japokuwa hakuwa na hatia?


Yesu aliishi kipindi ambacho Taifa la Israel lilikuwa chini ya ukoloni wa Warumi kama Tanzania ilivyokuwa chini ya ukoloni wa Wajerumani. Warumi waliitawala Israeli kwa mkono wa chuma wakilinda na kutetea ustawi wa dola yao. Kipaumbele chao kikuu kilikuwa pax Romana (amani ya Kirumi), yaani kudumisha utulivu wa kisiasa na kijamii. Mtu yeyote aliyeonesha kudai haki iliyo kinyume cha maslahi ya dola ya kirumi, aliyejiinua au kujipa mamlaka bila ya ruhusa ya Kaisali, na aliyepinga maamuzi ya Warumi, alionekana kuwa muasi au mhaini.


Yesu alipokamatwa na Wayahudi, alipelekwa kwa Pilato aliyekuwa Gavana wa Yudea (Judea) wakati huo. Yudea ilikuwa mkoa wa Dola ya Kirumi ulioko katika eneo la sasa la Israel na Palestina. Pilato aliteuliwa na Warumi kusimamia eneo hilo kama mwakilishi wa Kaisari, mtawala wa Roma. Pilato alikuwa na mamlaka ya kuamua kesi na kutoa hukumu ya kifo—ndiyo sababu viongozi wa Wayahudi walimpeleka Yesu kwake kutaka amhukumu kifo.


Ukweli ni kwamba Pilato hakuona hatia yoyote juu ya Yesu. Baada ya kusikiliza ushahidi, kumhoji Yesu na kupima maelezo ya wote Pilato alibaini kwamba mashitaka juu ya Yesu yalikuwa ya kubambikiza. Kisheria alipaswa kumuacha huru. Hata hivyo hali ya kisiasa na mazingira ya tukio lenyewe yalimbana kiasi cha kuondoa uadilifu wake. Wayahudi walileta mashitaka yaliyogusa maslahi ya dola ya Kirumi wakidai Yesu anajiita mfalme wa Wayahudi na anawazuia watu kulipa kodi kwa Kaisari.


Maneno haya japo yalikuwa ya uongo yalikuwa na uzito mkubwa kiasi cha kumtisha Pilato. Kitendo cha kujiita Mfalme wa Wayahudi na kuzuia watu wasilipe kodi kwa Kaisali kiliashiria kutangaza uasi dhidi ya dola ya kirumi, jambo ambalo lilikuwa halivumiliki. Wakuu wa Makuhani waliongezea uzito mashitaka haya kwa kumuonya Pilato kwa kumwambia “Ukimwachilia huyu, wewe si rafiki wa Kaisari; kila mtu ajifanyaye mfalme humpinga Kaisari.” (Yohana 19:12)


Japokuwa Pilato alijua mashitaka yale yalikuwa ya uongo, aliogopa kujenga uadui na Wakuu wa Makuhani ambao walikuwa na nguvu kubwa ya ushawishi kwa Wayahudi. Maneno ya Viongozi hao yalimlazimisha Pilato amhukumu Yesu ili kulinda nafasi yake kisiasa. Ingawa mwenyewe hakuona kosa lolote la kweli kwa Yesu (Luka 23:4). Shinikizo la kisiasa, hofu ya ghasia za Wayahudi na kiu ya kulinda nafasi yake ya kiutawala vilimfanya Pilato aidhinishe hukumu ya kifo.


Kwa ujumla Pilato aliona – mtu anayevuta umati mkubwa na kuitwa “Mfalme wa Wayahudi” alikuwa hatari kwa utawala wa Roma, na hatari zaidi kwa maslahi yake binafsi kama Gavana. Jambo ambalo huwenda hakulijua, ni kwamba Makuhani walikusudia kumuua Yesu ili kulinda maslahi yao binafsi, si ya dola ya Kirumi. Yesu alikuwa akipora wafuasi wao, na kufungua ufahamu wa watu. Wayahudi walianza kujitambua. Kwa ujumla Yesu alikuwa tishio kwa dini ya kiyahudi kuliko dola ya Kirumi.


Sasa hebu simama hapa kidogo. Tafakari na kujiuliza kama Rais wetu ndiye angekuwa kwenye nafasi ya Pilato wakati huo angemuachia huru Yesu au naye angemsulubisha? Angekuwa tayari kuwafukuza Wayahudi waliokuwa wakipiga kelele kutaka Yesu asulubiwe? Tena angekuwa tayari kuhatarisha maslahi yake binafsi (kupoteza nafasi ya utawala) kwa ajili ya haki na uhai wa mtu mmoja?


Kesi ya Yesu inatufundisha kutambua unafiki wa wanasiasa na watawala. Watu wanaojifanya waungwana, na wenye huruma lakini walio tayari kupindisha haki na hata kutoa uhai wa mtu asiyekuwa na hatia ili kulinda maslahi yao. Pilato alijua ukweli, alijua Yesu hakuwa MHAINI, wala hakuwa akiongoza UASI. Yesu alikuja kuwakomboa Waisrael kutoka katika utumwa wa dhambi, utumwa wa fikra na vifungo vya dini.


Ni ajabu kwamba Pilato alikuwa na askari, wapelelezi na majeshi ambayo angeweza kuyatumia kujua ukweli zaidi kabla ya kumhukumu Yesu kifo. Lakini hakufanya hivyo kwa sababu alitaka kuwaridhisha Wakuu wa Makuhani na Wayahudi waliokuwa wakipiga kelele kutaka Yesu asulubiwe. Hakutaka kupoteza muda kuitafuta haki ambayo ingemtia matatani. Aliamua kufanya maamuzi rahisi kwa kesi ngumu iliyohusu UHAI wa mtu.


Natamani sana viongozi wetu hasa mheshimiwa Rais ajifunze kutokana na makosa ya Pilato. Natamani viongozi wetu wajiepushe na shinikizo la watu wanaotaka watu fulani au kikundi cha wanasiasa fulani wafungwe magerezani, watekwe nyara au wapotezwe kwa kisingizio cha UHAINI au kuhatarisha usalama wa Taifa. Uko uwezekano mkubwa kwamba wanaoleta mashitaka hayo wanafanya hivyo kwa maslahi yao binafsi. Si maslahi ya nchi wala Kaisari (Mwenye ufahamu na afahamu).


Zingatia kuwa Yesu hakuwa na hatia lakini alihukumiwa kifo. Inawezekana hata wanasiasa wanaokamatwa, kutekwa nyara, au kufunguliwa mashitaka ya Uhaini leo ni watu wasio na hatia. Pengine ni waungwana tu waliojitolea kutetea haki na kufungua fikra za wananchi kama Yesu alivyofanya lakini Wayahudi wa wakati wetu (nchi yetu) wameshaona hatari ya kupoteza maslahi yao binafsi kiasi cha kumshawishi Pilato wetu kutoa hukumu. Ni vyema viongozi wetu walinde haki na uhai wa mtu mmoja kwa gharama yoyote.


Tunapokumbuka mateso ya Yesu, tukumbuke pia kwamba Pilato alikuwa na nafasi ya kutenda haki, na kuokoa maisha ya Yesu. Hakufanya hivyo kwa sababu ya hofu, kutaka kuwaridhisha Wayahudi na tamaa ya kulinda nafasi yake. Leo hii dunia inamhukumu Pilato kwa kumwaga damu isiyokuwa na hatia kwa sababu ambazo angeweza kuzizuia. Kumbe , kama usipokuwa mwangalifu iko siku NAWE dunia itakuhukumu kwa kumwaga damu isiyo na hatia kama Pilato.


Uwe na Pasaka njema Yenye Baraka

Rev. Godwin Chilewa

 
 
 

Comments


bottom of page