Maajabu ya Tanzania
- Rev. Godwin Chilewa
- Jul 7, 2015
- 4 min read

Tanzania inajulikana ulimwenguni pote kwamba ni nchi ya maajabu, ndio maana kila mwaka watu kutoka pande zote za dunia husafiri umbali mrefu, na kutumia fedha nyingi ili kuja kujionea maajabu mengi yaliyo sheheni nchini. Maajabu hayo ni pamoja na misitu, mbuga, na hifadhi kubwa za wanyama zilizojaa viumbe hai wengi ambao hawapatikani mahali pengine popote dunia, mabonde na milima mingi ya kushangaza ikiwa ni pamoja na mlima Kilimanjaro ambao pamoja na kuwa karibu na Ikweta huwa na theruji mwaka mzima.
Ipo pia mito mingi mirefu yenye maji matamu, na maziwa makubwa yanayo izunguka Tanzania na kuifanya ionekane kama mwanamwali anaelindwa na majemadari wa vita. Ndege, samaki, nyoka na viumbe vingine vya ajabu vyote vimeweka makazi yake nchini Tanzania kana kwamba ndio nchi pekee yenye rutuba. Tanzania imejaliwa pia kuwa na vito vya thamani ikiwa ni pamoja na almasi, dhahabu, yaspi, yakuti, yakuti manjano na zabarajadi. Vito vyote hivyo vimelundikana katika ardhi kubwa ya nchi hii kiasi cha kuwafanya wageni kutoka nje watamani kuinunua nchi yote na kuigeuza kuwa mgodi.
Si hivyo tu, Tanzania pia imejaliwa kuwa na mfumo wa siasa na uchumi wa ajabu kuliko nchi nyingine yoyote duniani. Mfumo unaotoa mwanya kwa wageni kuwa mamilionea kwa rasilimali za watanzania, huku wananchi wazawa wakiendelea kuwa maskini na serikali yao ikiendelea kuwa ombaomba kila kukicha. Si ajabu kwamba nchi hii ya ajabu inaongoza kwa kuwa na viongozi wa ajabu walio tayari kufanya lolote ili kulinda maslahi yao binafsi, lakini wasio tayari kufanya lolote la maana ili kuinua maisha ya wananchi wao japo kuwafanya wamudu kujipatia milo mitatu ya uhakika kwa siku.

Zaidi ya yote Tanzania imebarikiwa mno kuwa na wananchi (raia) wa ajabu sana, wasiojua kulalamika wala kupiga kelele wanapoonewa, au kudhulumiwa mali yao. Ni raia wa ajabu mno, wasiochukia wanapo tukanwa au kuambiwa maneno ya kejeli na viongozi. Ni wepesi wa kulaghaiwa kwa maneno matamu na walio tayari kuuza KURA zao kwa sahani za pilau, fulana zenye rangi ya kupendeza, doti za khanga na hata kwa burudani tu za wakata viuno na waimba taarabu. Ni raia wa ajabu ambao hufurahi na kupiga makofi hata pale wanapoambiwa kuwa “kila mtu atabeba msalaba wake mwenyewe” ilhali wakijua kuwa hawana nguvu za kubeba huo msalaba.
Acha wazungu walipe mamilioni ya dola kuja kuwaona watanzania maana kwa kusimuliwa tu hawawezi kuamini. Wakati wenzetu walioendelea walianzia chini na kujikokota taratibu kuelekea juu hadi kufika walipo leo hii, sisi tumeanzia juu na kujivurumisha kuelekea chini kwa kasi ya fataki.
Wenzetu (walio endelea) walianza na usafiri wa punda (zaidi ya miaka 3,500 iliyopita), wakaunda merikebu, magari ya stima, na baadae aeroplane na nyambizi (submarine); na sasa wanaenda kwenye mwezi na sayari ya Mars. Sie tumeanzia kwenye mabasi ya Icalus (UDA) tukaenda kwenye DCM, chai maharage, vipanya, bajaji na sasa bodaboda. Bila shaka tunaelekea kwenye punda. Naam! Maana magari na vyombo vingine vya moto vinaongeza uharibifu wa utando wa ozone.
Acha watalii wamiminike nchini kuja kujionea maajabu yetu. Wewe uliona wapi nchi iliyoendelea inatumia ‘ambulance’ za pikipiki? Hivi ukimpakia mama mjamzito kwenye hiyo ambulance ya pikipiki halafu ukafika muda wake wa kujifungua kabla hajafikishwa hospitali inakuwaje? Acha hiyo, mgonjwa akizidiwa wakati safari inaendelea huyo muuguzi (nurse) atamuhudumia vipi? Na mvua ikinyesha nani atakae mshikia mgonjwa mwamvuli ili asilowane? Halafu jambo la kushangaza zaidi ni kwamba bei ya kununulia ambulance hizo inakaribiana kabisa na gari aina ya Toyota Hiace ambayo kama ikifanyiwa ukarabati kidogo inaweza kuwa ambulance bora zaidi.
Hata kama ni msaada wa bure mimi ningeukataa. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba mtu akikupa ushauri wa kipumbavu, na wewe ukaukubali ushauri huo huku ukijua kuwa ni ushauri wa kipumbavu, mtu huyo (aliyekupa ushauri) anakudharau. Hivi kwa nini viongozi wasifikiri kupunguza posho zao na malulupu ya wanasiasa na kutumia fedha hizo kununulia ambulance za kweli?
Haishangazi kwamba Kenya inaongoza duniani kwa kuuza vinyago vya mpingo wakati mti huo haumei nchini kwao na wachongaji maarufu wa vinyago hivyo wamejaa Tanzania ambako mti huo unapatikana kwa wingi. Wakenya wanaongoza kwa kuuza vito aina ya tanzanites kwa wingi katika soko la dunia wakati mashimo ya vito hivyo yapo Tanzania tu. Wanasambaza duniani kahawa na chai ya Tanzania wakati mazao hayo yanalimwa nchini kwetu.
Si ajabu kwamba watu wengi ulimwenguni wanadhani mlima Kilimanjaro uko nchini Kenya maana wenzetu walisha uhodhi kibiashara siku nyingi wakati sie tunacheza dogoli. Na sasa nasiki wanataka kujenga uwanja wa ndege Taveta ili wafanye biashara ya utalii zaidi hivi KIA itapata mtu kweli?
Acha hayo, takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa Tanzania inashika nafasi ya tano ulimwenguni kwa kuwa na vivutio vizuri Zaidi na mazingira bora ya kuvutia watalii. Hata hivyo inashangaza kwamba nchi hii inashika nafasi ya 105 kati ya nchi 135 duniani kwa kuingiza mapato kutokana na utalii! Ajabu sana, tena ya kujisaidia hadharani bila aibu.

Wakati wenzetu wanalinda rasilimali zao (za kipekee) zisihamishiwe katika nchi nyingine (ughaibuni) siye tunaongoza kwa kugawa Simba wetu, Tembo, Chui na hata Twiga bila kujali kwamba waungwana tunaowagawia wanakwenda kutengeneza Zoo katika nchi zao na hivyo kupunguza idadi ya watalii watakaokuja katika nchi yetu. Wewe uliona wapi nchi inayokubali kumpa ruhusa mkandarasi kuchukua udongo wenye dhahabu ghafi (usiochekechwa) ili akauchekechee kwao (ughaibuni) na kisha kumpa taarifa mwenye mali kiasi na thamani ya dhahabu iliyopatikana?
Si ajabu kwamba tumeamua kugawa shahada za udaktari kwa kila mtu bila kujali mchango na kipimo halisi cha utendaji wake katika kuelimisha, kuboresha au kufanikisha maendeleo ya watanzania na watu wengine duniani. Naam, pengine hatuoni haja wala umuhimu wa kusoma tena. Kwanza nani kasema mtu akienda shule ndiyo anaelimika? Shauri yao hao akina Dr Salim Ahmed Salim walio uhangaikia na kuupata udaktari kwa kuutolea jasho.
Kizazi chetu sie ukipata udiwanitu na udaktari unakufuata nyuma kama kazi. Hapa nilipo nasubiria ‘Ankal’ apewe udaktari wake. Ndio, nani asiyejua kuwa blog yake ina mafanikio kuliko blog nyingine yoyote nchini Tanzania? Kwa nini nae tusimpe udaktari wa kublog? Kwani tumewapa wangapi? Tumejidai kuwakataza kina Profesa Vulata, Profesa Maji marefu na Dr Remmy wasijiite maprofesa eti kwa sababu wanaharibu sifa na heshima ya wadhifa huo kumbe na sie pia tunautamani. Ajabu sana.
Zaidi ya yote inachekesha kwamba baada ya miaka mingi ya kuishi kwa amani na furaha viongozi wa dini nao wameanza kuchochea vurugu, kutukana dini za watu wengine, na hata kuchoma makanisa na misikiti ili kumfurahisha mwenyezi Mungu. Hivi dini kazi yake ni kuleta amani au kuvuruga amani?
Wakati watu wengine duniani wanaitafuta amani kwa kila namna sie tunatafuta namna ya kuipoteza! Ajabu sana, tena ya Mwajabu kuolewa na Rajabu. Namuomba sana mwenyezi Mungu anipe uhai na kuendelea kulilinda Taifa hili la ajabu na watu wake, na hasa kipindi hiki tunapoelekea katika uchaguzi mkuu wa rais na wabunge. Nina hakika huu nao utakuwa uchaguzi wa AJABU sana.
Uwe na amani
Rev. Godwin Chilewa
_______
Comments