Mabadiliko Ya Mfumo Wa Elimu Nchini - Tumemuiga Nani?
- Rev. Godwin Chilewa
- Jun 20, 2022
- 5 min read
Updated: Jun 19, 2023

Mabadiliko ni kitu cha kawaida, na tena cha lazima katika maisha. Yamkini pasipo mabadiliko hakuna mtu, jamii, wala nchi yoyote inayoweza kupiga hatua. Mabadiliko ndiyo yanayofanya nchi ya wenye ufahamu kusonga mbele, na ile ya wasiojitambua kuachwa palepale au kurudishwa nyuma kwa kasi. Ni kwa sababu hii mataifa yaliyoendelea hufanya mabadiliko ya kila aina, na mara kwa mara katika mifumo yake ili kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Katika kufanikisha hilo mataifa yenye kujitambua hufanya kila liwezekanalo kuiga teknolojia mpya. Nchi kama China, Russia, India na nyinginezo hupenyeza maelfu ya raia zake nchini Marekani na Ulaya kujifunza elimu mpya na kuiba siri za maendeleo. Raia hao huingia katika nchi hizo wakiwa wanafunzi wa kawaida katika vyuo vikuu, au wahamiaji wanaotafuta kazi katika viwanda na taasisi za uchunguzi (research) wanazozikusudia. Hawa wote huwa na lengo moja tu, kuiba siri za sayansi na teknolojia na kuzipeleka kwao.
Si hivyo tu, bali kila mwaka serikali ya Marekani hutumia mamilioni ya fedha kwa ajili ya mambo ya kiusalama, hususani kuwasaka majasusi wa kigeni wanaojipenyeza nchini humo kwa lengo la kuiba siri za biashara na uchumi, sayansi na teknolojia, na zile za ulinzi na usalama. Hili huenda sambamba na kuwatafuta wadukuzi (hackers) wa nchi mbalimbali wanaojaribu kuingia ndani ya mifumo mbalimbali ya nchi hiyo. Haya yote husababishwa na kiu waliyonayo wenzetu katika kukuza na kulinda ufahamu wao wa sayansi na teknolojia. Kwa ufupi wanajua thamani ya ELIMU, wanaitafuta kwa bidii na kulinda hazina yao isichukuliwe hovyo hovyo tu.
Nimeyasema haya kwa sababu bado naendelea kujiuliza sisi tuna ugonjwa gani? Hivi hawa wataalam wetu waliotuletea hii Sera mpya ya elimu nchini wameitoa wapi? wamechukua mfano wa nchi gani? na wametumia vigezo gani? Nani aliyewaambia kwamba kufupisha elimu ya msingi toka madarasa saba hadi sita itasaidia kuboresha elimu? Kama hayo madarasa saba yaliyokuwepo bado hayakutosha kuwasaidia wanafunzi wengi hasa wa vijijini kupata elimu bora, je madarasa sita yatawaokoa kweli? Kigezo gani kilichotumika kufanya uamuzi huu? Au ni kwa sababu wataendelea moja kwa moja tu hadi kidato cha nne?

Tena huu mpango wa kuondoa mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi utasaidiaje kuwafanya wanafunzi wasome kwa bidii? Utafiti gani ulioonesha mtihani wa darasa la nne utasaidia wanafunzi kujiandaa vyema kwa elimu ya juu kuliko wa darasa la saba? Kama matokeo ya mtihani wa taifa wa darasa la saba uliokuwa ukiheshimiwa kwa kulindwa na maafisa wa idara ya Usalama wa Taifa, Polisi (na wajumbe wengine wote wa kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya) haukutosha kuwatikisa wanafunzi, wala kuishitua serikali kuwa elimu ya Tanzania ina matatizo makubwa; Je! mtihani wa darasa la nne utasaidia kweli? Utamshitua nani? Tena ukizingatia mwanafunzi anaufanya akiwa bado mtoto zaidi?
Kwa maoni yangu nadhani mtu aliyetoa pendekezo la kubadilisha sera ya elimu hakufanya uitafiti wa kutosha, au maelezo yake hayakueleweka na wale waliolifanyia kazi suala hili. Au pengine wahusika wamechukua mfano wa nchi moja iliyofanikiwa bila kujua undani wa mfumo huo. Nakumbuka hata Zanzibar walikuwa wana mfumo wa aina hii pia. Kwa kifupi mfumo huu unafanana sana na ule unaotumika nchini Marekani na nchi nyingine zilizoendelea, Ni mfumo wenye gharama kubwa, na unafaa kwa nchi inayojiweza. Hauko rahisi kama wataalam wetu wanavyofikiri.
Kwa mfano, mwanafunzi wa Marekani huanza elimu ya awali (Elementary education) darasa la chekechea (Kindergarten) na kuendelea hadi darasa la nne. Anapoingia darasa la tano hupelekwa shule ya kati (Middle School) ambapo husoma hadi darasa la nane. Hapo huwa ndiyo mwisho wa elimu ya awali, mtoto hupelekwa shule ya upili (High school) ambako husoma darasa la tisa hadi la kumi na mbili. Akimaliza (na kufaulu vyema) huenda moja kwa moja chuo kikuu.
Ukiangalia kijuujuu unaweza kudhani huu ni mfumo usio na maswali mengi, lakini sivyo. Katika kipindi chote mwanafunzi anapokuwa shuleni hufanyaishwa mitihani mingi kupima uwezo wake. Baadhi ya mitihani hiyo hutungwa katika shule anayosoma, na mingine huwa ya kiwilaya (School district) na kitaifa (State exams). Mwanafunzi anayeshindwa kufikia alama ya ufaulu iliyowekwa hulazimika kurudia darasa. Kwa mfano, katika jimbo la Texas wanafunzi hulazimika kufanya mitihani ifuatayo:
Mtihani wa Vipaji Maalum (Gifted Talented Students Test)
Mtihani huu ndiyo wa kwanza kabisa anaopewa mwanafunzi katika jimbo la Texas. Mtoto hufanyishwa mtihani huu (kupima IQ yake) akiwa shule ya chekechea (Kindergarten) au darasa la kwanza. Huu ndiyo mtihani unaoamua kama mtoto husika anafaa kuingizwa katika madarasa ya watoto wenye vipaji maalum (Gifted talented) au la. Mtoto akifaulu moja kwa moja huingizwa katika madarasa ya watoto wenye vipaji maalum ambayo utaratibu wake wa masomo ni tofauti. Kama akishindwa huwekwa katika madarasa ya watoto wa kawaida.
Hata hivyo wakati wowote ule (kati ya darasa la kwanza na la pili) mwalimu akimuona mtoto ana ufahamu usio wa kawaida hupendekeza afanyiwe mtihani huo .Mtoto aliyefaulu kuingia madarasa ya watoto wa vipaji maalum (GT) hutakiwa kuendelea kuonesha uwezo wake darasani kipindi chote anachokuwa shuleni; kama akionesha kutomudu madarasa ya vipaji maalum (GT) hurudishwa katika madarasa ya wanafunzi wa kawaida. Mtoto anayermalkiza elimu ya awali katika madarasa ya vipaji maalum hupelekwa Middle school na High school za watoto wa vipaji maalum.
2. Mitihani ya Wilaya (School District)
Kila mwaka wanafunzi wa shule ya awali (elementary school) hufanya mtihani wa wilaya (school district test). Mitihani huu hufanywa mara moja kwa mwaka, kutegemea ratiba ya wilaya husika. Lengo la mitihani hii ni kumhakikishia mzazi kuwa maendeleo ya mtoto wake ni mazuri au mabaya kama yanavyooneshwa katika taarifa (report card) ya matokeo ya majaribio na mitihani inayotungwa na mwalimu wa darasa lake. Hii huondoa utata kuwa walimu wanawafundisha watoto majibu badala ya kuwafundisha waelewe. Pia huondoa malalamiko au hisia ya mzazi wa mtoto asiyefanya vyema darasani kuwa mwanawe anakatwa alama zake au hatendewi haki.
3. Mtihani wa Taifa (Texas STAAR Test).
Huu ni mtihani wa taifa (State Exam) unaofanywa kila mwaka na wanafunzi wa shule ya awali (Elementary school) na wale wa shule ya Kati (Middle School) kuanzia darasa la tatu (third grade) hadi darasa la nane (eighth grade). Mtihani huu huhusisha masomo ya Hesabu, Sayansi, kusoma na kuandika. Mwanafunzi asiyefaulu mtihani huu hulazimika kuurudia mara ya pili (wakati mwingine) asipofaulu tena hulazimika kurudia darasa.
4. Mitihani ya Mwisho (Final Exams).
Ili mwanafunzi atambulike kuwa amehitimu shule ya upili katika Texas Public Highschools ni lazima afaulu masomo matano katika mtihani wake wa mwisho. Masomo hayo ni English - Reading, Mathematics (Algebra), Historia (U.S History), na English - Writing. Mwanafunzi asiyefaulu hutakiwa kurudia darasa.
Kama unavyoona huu si mfumo rahisi kama watengeneza sera wetu wanavyofikiria. Unahitaji maandalizi, usimamizi wa hali ya juu, na fedha nyingi za uendeshaji. Ni mfumo mzuri lakini una gharama isiyokwepeka. Kwani ili uwe na wahitimu bora ni lazima wajaribiwe na kuthibitishwa kwa mitihani. Je tuko tayari kubeba mzigo huo? Kama hatuna uwezo wa kufanya hivyo kwa nini tunataka kuchukua mfumo tusiouweza? Huu tuluionao tunashindwaje kuusimamia hadi uoneshe mafanikio? Je tatizo ni sera au usimamizi? Je! hiyo sera mpya itaongeza uwezo wa walimu wetu kufundisha? Au utamfaidisha nani?
Kumbe ni vyema serikali iangalie upya marekebisho ya sera ya elimu kabla ya kukurupuka na utekelezaji wake. Kitendo cha kuondoa mtihani wa darasda la saba ni dalili tosha kuwa sera hiyo itawaathiri zaidi wanafunzi kimasomo. Mtihani huo licha ya kuwa kipimo cha uelewa wa mwanafunzi, ndiyo pia uliokuwa kigezo cha kuwepo kwa Qualifying Test, mtihani uliokuwa ukifanywa na watu waliotaka kufanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne kama Private Candidate. Kuondolewa kwa mtihani wa dsarasa la saba moja kwa moja kunafuta Qualifying Test. Je wanafunzi binafsi watapimwaje? Tusipoziba ufa tutajenga ukuta.
Ustawi wa Tanzania - Jukumu letu sote.
Uwe na amani.
Rev. Godwin Chilewa
Comments