Mabadiliko ya Mara kwa Mara ya Mawaziri na Wakuu wa Idara: Yanaongeza Tija au Mzigo?
- Rev. Godwin Chilewa
- Dec 11, 2024
- 6 min read
Updated: Jan 9

Jana, tarehe 10 Desemba 2024, Rais wa JMT mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliwaapisha mawaziri wapya aliowateua hivi karibuni kuongoza wizara mbalimbali. Hii si mara yake ya kwanza kufanya hivyo, alishafanya mara kadhaa na upo uwezekano mkubwa akafanya tena kabla ya uchaguzi mkuu wa mwakani.
Kimsingi wizara na idara za serikali ni moyo wa utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo ya taifa. Pasipo uongozi thabiti nchi haiwezi kupiga hatua za maendeleo. Ni kwa sababu hii na kwa unyenyekevu mkubwa nimeona haja ya kuungana na wananchi, wengine waliosikika wakihoji umuhimu wa mabadiliko haya ya baraza la mawazili na idara mbalimbali. Naamini hoja hii ni ya msingi na inapaswa kujadiliwa kwa heshima kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa taifa letu
Ni ukweli usiopingika kwamba mabadiliko ya aina hii yamekuwa yakifanyika mara kwa mara lakini hakuna utofauti mkubwa unaoonekana katika utendaji wa serikali. Hii ni kwa sababu watu wanaozungushwa katika nafasi hizo ni walewale, na wote huwa wakisifiwa kwa kazi nzuri walizofanya kule wanakoondolewa na kutakiwa kupeleka uzoefu huo kwenye wizara au idara mpya. Hapo ndipo wananchi wanapojiuliza “kama mtu anafanya vizuri kuna haja gani ya kumhamisha?”
Kimsingi, mheshimiwa Rais ana haki ya kikatiba ya kumteua mtu yeyote anayeona anafaa, kushika wizara au idara yoyote, mahali popote, muda wowote, na kwa namna yeye anavyoona inafaa. Hili ni haki yake ya kisheria, na haiingiliwi. Lakini pia ustawi na maendeleo ya taifa hutegemea sana uongozi imara. Kwahiyo wananchi pia wana haki ya kuhoji sababu zinazofanya kuwa na mawaziri au wakuu wa idara wasioaminika, au wasio na uwezo wa kuongoza wizara au idara zao kwa kipindi chote cha miaka mitano, au walau robo tatu ya kipindi hicho.
Ni jambo lisilopingika kuwa mabadiliko ya uongozi wa juu wa wizara au idara kuu si kitu kidogo. Kila mabadiliko huja na athari nyingi ambazo zisipodhibitiwa huweza kuyumbisha utendaji wa wizara au idara husika. Ni kwa sababu mheshimiwa Rais anapaswa kuwa na sababu za msingi kuwahamisha au kuwaondoa wateule wake. Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na:
(a) Kutoridhishwa na utendaji wa mteule wake.
Rais, kama mkuu wa nchi, ana jukumu la kuhakikisha watendaji wake wanatimiza malengo ya serikali. Ikiwa waziri au mkuu wa idara anashindwa kufanikisha malengo aliyowekewa au anaonyesha utendaji dhaifu, ni wajibu wa rais kuchukua hatua ya kumwondoa, kumhamisha au kumshusha cheo.
(b) Shinikizo la kisiasa na maslahi ya chama
Kwa kuwa chama tawala ndicho kinachoendesha serikali Rais anaweza kufanya, mabadiliko ya mawaziri hutokana na shinikizo kutoka kwa wanasiasa wengine au mahitaji ya kusawazisha nguvu za kisiasa ndani ya chama tawala. Rais anaweza kubadilisha mawaziri ili kulinda mshikamano wa kisiasa ndani na nje ya chama.
(c) Kashfa za kiutendaji na maadili pia ni sababu tosha kwa Rais kumuondoa mteule wake madarakani. Waziri au kiongozi anayehusishwa na kashfa za ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka, au migogoro ya kimaadili anaweza kuondolewa haraka ili kulinda taswira njema ya serikali na kuboresha utendaji.
(d) Serikali inapobadilisha vipaumbele vya sera, wizara mpya huundwa au kuunganishwa, na hivyo kusababisha mabadiliko ya mawaziri. Hata hivyo hili hupaswa kufanywa kwa umakini mkubwa zaidi kuepusha mabadiliko ya mara kwa mara yanayopelekea serikali kutokuwa na sera au mipango ya muda mrefu inayotekelezeka. Wakuu wengi wa idara hutumia kifuniko cha mabadiliko ya sera na mipango kufunika udhaifu wa utendaji wao.
(e) Aidha Rais anaweza kufanya mabadiliko kwa sababu za kibinafsi au kiafya, matatizo ya kifamilia, au maamuzi yao binafsi ya kuacha nafasi zao. Mara nyingi hili huhusisha kuondolewa katika majukumu ya uwaziri au ukuu wa idara . Kumhamishia mgonjwa kwenye wizara nyingine ni kuidhoofisha.
Ukiangalia kwa kina sababu hizi, bila shaka utashindwa kuelewa sababu hasa za mawaziri wetu kuhamishwa hamishwa. Kwani ingekuwa suala la udhaifu wa kiutendaji, basi wote walipaswa kuwa wametolewa kwenye nyadhifa zao maana wameshazunguka sana, wengi wizara zaidi ya tatu. Isitoshe wote huwa wanasifiwa kwa kazi nzuri. Na kama suala ninkuwa na kashfa, kwa nini wanaendelea kubaki madarakani? Mtu mwenye kashfa anapaswa kuondokewa ili kulinda usafi wa serikali, kumuhamisha kunafaa nini?
Sasa, ukiondoa hayo mawili kinalobaki kuwa na nguvu ni lile la shinikizo la chama tawala. Kwamba huwenda wazee wa CCM wanataka mabadiliko ya uongozi wa serikali. Lakini hili nalo linaleta ukakasi. Maana baadhi ya mawaziri wamerudishwa kwenye wizara zao za zamani. Kama chama kilimuona muhusika hafai kuongoza wizara hiyo jana, ni nini kimempa uwezo wa kuongoza wizara hiyo leo? Isitoshe Rais ndiye kiongozi mkuu wa chama tawala, kuna mtu mwenye mbavu za kumshinikiza kwe? Hapa tunapata jibu, hata hili inawezekana silo. Kumbe tatizo ni nini!?
Mabadiliko ya mara kwa mara yana madhara makubwa kwa ustawi wa wizara na watendaji kwa ujumla. Baadhi ya madhara hayo ni kupoteza mwendelezo wa kazi, kuathiri utekelezaji wa sera na miradi ya muda mrefu. Mawaziri wapya hutumia muda mwingi kujifunza majukumu na changamoto za wizara, hali inayochelewesha utekelezaji wa mipango.
Watumishi wa wizara wanapobadilishiwa viongozi mara kwa mara, huathirika kisaikolojia na mara nyingine hupoteza mwelekeo kuhusu matarajio ya uongozi mpya. Ari ya kazi hushuka, na watumishi huanza kujipanga upya namna ya kushughulika na utawala mpya.
Pamoja na hayo, mabadiliko husababidha gharama kubwa za kiutawala hasa yanapohusisha uundaji wa wizara mpya au kugawa zilizopo, serikali hutumia fedha nyingi kuanzisha miundombinu mipya, kubadilisha vitengo, na kuajiri wafanyakazi wa ziada. Mbaya zaifi eizara hizi hudumu kwa muda mfupi tu na kuundwa upya tena. Kwa mfano hivi sasa imebakia miezi michache tu kuingia kwenye uchaguzi mkuu. Ni dhahiri mabadiliko mengine yatafanyika mwakani mara tu baada ya uchaguzi huo.
Vilevile, mabadiliko hushusha imani ya wananchi. Wananchi wanaweza kuanza kuhoji ufanisi wa serikali ikiwa mawaziri wanabadilishwa mara kwa mara, hasa ikiwa mabadiliko haya hayaonyeshi maboresho ya wazi ya utendaji. Wengi juishia kuamini kwamba hii ni njia mojawapo ya watawala kuwapatia nafasi za kula watu wso, jambo ambalo si sahihi.
Kubwa zaidi ni kwamba mabadiliko huathiri usimamizi thabiti wa sera. Mawaziri wapya mara nyingi huja na vipaumbele tofauti, hali inayoweza kuathiri usimamizi wa sera za wizara husika, na mara nyingine huanza kutengeneza makundi yasiyo ya msingi.
Kutokana na athari hizo, ni muhimu sana mheshimiwa Rais apunguze mazoea ya kubadilisha baraza la mawaziri. Ni dhahiri kwamba nia yake ni njema, hasa kuboresha utendaji wa mawaziri. Lakini hii ni njia yenye utata, na isiyopenda kutumiwa na mataifa yaliyoendelea. Badala yake Rais, ikimpendeza anaweza kufanya mambo yafuatayo
Kuteua Viongozi Wenye Weledi
Rais anapaswa kuhakikisha uteuzi wa mawaziri unazingatia uwezo, weledi, na uzoefu wa kiongozi husika katika sekta inayohusiana na wizara. Uteuzi ufanyike baada ya TISS kufanya upekuzi wa kina kuthibitisha sifa na uwezo wa mteule. Yapo malalamiko mengi kuwa baadhi ya viongozi wanapewa nafasi wasizostahili wala wasixoweza kuziongoza. Ni muhimu sana uteuzi uzingatie sifa na upekuzi sahihi.
2. Kutoa Mafunzo Maalum.
Rais Jakaya Kikwete alipoingia madarakani alianza na utaratibu wa Semina Elekezi. Semina hizi ziliwapa mafunzo viongozi kabla ya mawaziri kuanza kazi. Ni muhimu sana utaratibu huu kuwapa mafunzo viongozi kuhusu majukumu yao, changamoto za wizara, na mipango ya serikali uendelezwe Hii itawasaidia kuwa tayari kwa kazi na kupunguza muda wa kujifunza.
Pamoja na hili ni muhimu mawaziri, makatibu wakuu na wakuu wa idara wapewe muda wa kujifunza kazi zao kwa vitendo, kuzizoea na kuwa wabobezi katika wizara husika. Waziri anayepewa wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga, Wizara ya Afya, au Wizara ya Mambo ya Ndani Taifa hawezi kuimudu wizara kwa kukaa miezi sita tu. Anahitaji kujifunza, kujenga mahusiano na makamanda au wakuu wa idara za chini yake’ na ndipo anapobobea.
3. Utendaji wa Mawaziri Upimwe
Rais anapaswa kuwa na vigezo maalum vinavyotumika katika kupima ubora wa watendaji wake. Ni muhimu utendaji wa mawaziri usipimwe kwa kusikiliza malalamiko ya wananchi tu. Kwanza mengi ya malalamiko hayo hutokana na uzembe wa watu walio chini ya waziri husika. Kumbe waziri anapaswa kuziba mianya inayosababisha malalamiko, sio kusikiliza malalamiko na kesi zilizosababishwa na uzembe wa watu walio chini yake.
Pili, malalamiko mengi huanzia ngazi ya chini, na yanapofika ngazi ya taifa (wizarani) maana yake wakuu wa wilaya na mikoa wameshindwa kufanya wajibu wao. Mawaziri wanapaswa kupimwa kwa usimamizi wa utekelezaji wa sera za seriksli katika wizara zao. Kumbe badala ya kufanya mabadiliko mara kwa mara, rais anaweza kuweka viwango na malengo ya utendaji kwa mawaziri na kufanya tathmini ya mara kwa mara ili kubaini changamoto na kusaidia kutatua matatizo, au kuwaondoa kabisa mawaziri wasio na uwezo
4. Kuboresha ushirikiano wa kiutendaji
Rais anapaswa kujenga utamaduni wa mawasiliano na ushirikiano wa karibu kati ya mawaziri na ofisi yake, ili kuondoa changamoto za utendaji kabla ya kufikia hatua ya mabadiliko makubwa. Pamoja na hili Rais anapaswa kuepuka uteuzi wa mawaziri kwa misingi ya kisiasa tu na badala yake kuweka mkazo kwenye uwajibikaji na utendaji wa hali ya juu.
Hitimisho
Ingawa mabadiliko ya mawaziri yanaweza kuwa muhimu wakati mwingine, yanapofanyika mara kwa mara yanaweza kusababisha madhara makubwa ya kiutendaji. Rais anapaswa kuimarisha mifumo ya tathmini, mafunzo, na uteuzi wa viongozi ili kuhakikisha wizara zinaongozwa kwa ufanisi. Ni muhimu pia kudumisha mwendelezo wa kazi ili kuleta maendeleo endelevu kwa taifa. Tanzania itafaidika zaidi ikiwa uongozi wa serikali utazingatia umakini, uthabiti, na weledi wa hali ya juu.
Rev. Godwin Chilewa
Comments