Maboresho ya Majeshi ya Ulinzi na Usalama - Yaanzie TISS
- Rev. Godwin Chilewa
- Jul 23, 2022
- 10 min read
Updated: Jul 24, 2024

Nianze kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua udhaifu unaoyakabili majeshi yetu, na kuamua kwa dhati kuyafanyia kazi. Nampongeza pia kwa kulifanyia mabadiliko makubwa jeshi la Polisi kwa lengo la kuliboresha, na kuhakikisha linafanya kazi zake kwa haki na kuzingatia sheria zilizowekwa. Zaidi ya yote nampongeza sana kwa kuunda kamati maalum itakayozungukia majeshi yote kwa lengo la kuyafanyia uchunguzi/kuyakagua ili kutambua madhaifu mengine, na kupendekeza namna ya kuyaboresha.
Katika hotuba yake, mheshimiwa Rais alisisitiza kuwa, kamati aliyoiunda itafanya uchunguzi katika jeshi moja baada ya jingine hadi itakapomaliza majeshi yote na kutoa mapendekezo yake. Hata hivyo hotuba hiyo haikutaja kama idara ya Usalama wa Taifa (TISS) itakuwa miongoni mwa majeshi yatakayofanyiwa uchunguzi huo muhimu au la. Kwa jinsi utendaji wa idara hiyo ulivyo wa siri unafanya iwe ngumu kiasi fulani kuachia mtu yeyote kuichokonoa kwa undani kwa sababu za kiusalama. Ndiyo maana hata maafisa wenyewe hulazimika kufuata kanuni ya usiri sambamba (compatimentation/ need to know) katika utendaji wao. Hata hivyo, ni muhimu sana idara imulikwe ili mapungufu yake yaweze kujulikana na kushughulikiwa.
Pengine itakuwa vyema niweke bayana pia kwamba sina hakika kamati hiyo endapo ikipata nafasi ya kuifanyia uchunguzi idara itazingatia mambo gani zaidi. Nina hakika wanakamati walioteuliwa wana weledi wa hali ya juu na uzoefu utakaowawezesha kuangalia mambo ya msingi, na kutoa ushauri bila kupepesa macho. Hata hivyo, nikiwa mtu mwenye weledi kidogo na mambo ya intelijensia naona si vibaya nikigusia mambo ambayo mimi binafsi ningetamani sana kamati iyatazame, na kuishauri idara ili iweze kuyafanyia kazi kwa uhakika (seriously). Mambo haya, yote ni ya kiutendaji, na ya kuzingatia sana:

(a) Utendaji Katika Mfumo wa Vyama Vingi
Lengo la kuundwa kwa sheria ya Idara ya Usalama wa Taifa namba 15 ya mwaka 1996 ilikuwa kuiondoa idara katika mkanganyiko wa kuwa chini ya Ofis ya Rais ( ambaye ni Mwenyekiti wa CCM) na kuifanya kuwa chombo huru. Kabla ya mwaka 1995 kila aliyejiunga na idara hii alipaswa kuwa mwanachama wa CCM. Hivyo maafisa wa idara ya Usalama wa Taifa walijulikana kama vijana wa Chama. Ulipoanzishwa mfumo wa vyama vingi, ndoa kati ya idara na CCM ilisitishwa. Maafisa wote walitakiwa kurudisha kadi za CCM na kujitambua kuwa wao si wanachama wa chama chochote cha siasa.
Chini ya Uongozi wa marehemu Rais Benjamin Mkapa na DGIS Colnel Apson Mwang'onda idara ilifanya kazi kwa uhuru, kwa kufuata sheria ya vyama vingi. Maafisa wa idara walijitenga na siasa za vyama, na hivyo kuwatendea haki na usawa (kwa kiasi kikubwa) viongozi wa vyama vyote vya siasa. Hili lilibadilika wakati wa uongozi wa marehemu Rais, John Magufuli aliyelazimisha (kinyume cha katiba) idara zote za serikali kufanya kazi kana kwamba nchi iko katika mfumo wa chama kimoja. Hali hii imevuruga kwa kiasi kikubwa image na utendaji wa idara ya Usalama wa Taifa, na majeshi yote ya ulinzi na usalama.
Kwa kuwa mhe. Rais, Samia Hassan Suluhu amekusudia kufanya marekebisho ya dhati, ni vyema kamati iliyopewa jukumu la kuchunguza na kutoa mapendekezo iangalie jambo hili kwa kina, bila kuyumbishwa wala kupepesa macho, na kumueleza ukweli mheshimiwa Rais. Vinginevyo nchi itaendelea kuwa na katiba inayoruhusu mfumo wa vyama vingi, huku majeshi yake ya ulinzi na usalama yakitetea mfumo wa chama kimoja. Hii ni aibu kubwa. Majeshi yote yanapaswa kuwa vyombo visivyofungamana na siasa za chama chochote.
(b) Kufanya Kazi kwa Kukera/Uchokozi (IOffensive)
Sheria ya Idara ya Usalama wa Taifa namba 15 ya mwaka 1996 inataja kazi za TISS ni kukusanya taarifa za kiusalama, kuzichambua, na kuishauri serikali hatua inayopaswa kuchukua kuhusiana na suala husika. Idara ina wajibu wa kubaini vitendo vyote vya kiadui ikiwa pamoja na ujasusi, uhaini, uhujumu uchumi, uzandiki, na vitendo vingine vyote vya kiadui vinavyopangwa kufanywa dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Idara inapaswa kuwatambua maadui wa ndani na wa nje, na kuwadhibiti.
Ili kufanikisha kazi hizi ni muhimu sana idara ifanye kazi kwa uchokozi (offensive), badala ya kufanya kazi ki zimamoto au postmoterm. Hii ina maana idara inapaswa kuwa ya kwanza kujua mambo muhimu yanayogusa maslahi ya Tanzania kitaifa na kimataifa, katika nyanja za uchumi, siasa, ulinzi na usalama, teknolojia, na masuala yote ya kijamii. Idara itaweza kufanya hivyo endapo itazingatia kuajiri, na kuwapenyeza watoa habari wenye uwezo kwenye sehemu zote muhimu ndani na nje ya nchi.
Kwa kifupi, TISS ni macho ya Rais na serikali kwa ujumla. Tanzania haiwezi kujua mataifa makubwa na nchi jirani zinatuwazia nini, na au zinapanga kutufanyia nini endapo TISS haina watoa habari wa uhakika kwenye balozi, na ndani ya nchi hizo. Hali kadhalika serikali haiwezi kujua yanayoendelea ndani ya mashirika ya umma, taasisi zisizo za kiserikali, balozi za nje zilizopo nchini, majeshi yote ya ulinzi na usalama, vyama vya siasa, na kila mtaa wa mji na kijiji nchini. Ni lazima TISS ifanye kazi ki offensive ili iweze kufanikiwa katika malengo yake.
Katika miaka ya nyuma Idara ya Usalama wa Taifa ya Tanzania ilikuwa ikiheshimika barani Afrika kwa weledi wake. Lakini hivi karibuni, TISS imeonesha udhaifu mkubwa katika ukusanyaji wa taarifa za kiusalama, na au uchambuzi na ushauri kwa serikali. Udhaifu huo umepelekea idara kujikuta ikifanya kazi za kufuatilia matukio yaliyokwishatokea (Postmoterm) badala ya kufanya kazi ya kuzuia matukio hayo kabla hayajatokea. Ukweli huu unajidhihirisha kwa kuangalia kila kinachoendelea nchini Tanzania kiuchumi, kisiasa, kijamii, kiulinzi na usalama, na kiutamaduni.
Hali hii huwenda imesababishwa na idara/maafisa wa idara kuajili watoa habari wasio na uwezo, au katika malengo yasiyo na uzito mkubwa. Vilevile inawezekana kuwa idara inasita kujipenyeza katika maeneo fulani kwa kuhofia kufanya uchokozi unaoweza kusababisha kutoelewana kati ya nchi majirani, au balozi. Hata hivyo ni ukweli usiopingika kuwa balozi zote za nje zimejaa majasusi na watoa habari wao wanaoendelea kukusanya taarifa za kiusalama za kila kinachoendeleza Tanzania. Hili ni jambo la kawaida lisilohitaji mjadala. Ni lazima TISS ijitahidi kufanya kazi offensive/aggressive ili nchi ipone. Nasisitiza Idara izingatie kuwa kazi yake ni kuzuia sio kutibu.

(c) Kufanya Kazi kwa Weledi (Profesionalism)
Idara ya Usalama wa Taifa ndiye mshauri mkuu wa rais na serikali kwa ujumla. Kwa sababu hiyo inapaswa kuwa na maafisa wenye taaluma mbalimbali. Katika hili TISS imefanikiwa kwa kiasi fulani kwa kuwasomesha baadhi ya maafisa wake ndani na nje ya Tanzania. Idara inao wachumi, wanadiplomasia, wanasheria, madaktari, na wataalam wengine wengi. Tatizo lililopo ni kwamba wengi wa wataalam hawa wamesoma katika vyuo vikuu vya kawaida vinavyofundisha masomo ya kawaida, na baada ya kuhitimu mafunzo haya wengi wao huwa hawafundishwi namna ya kutumia elimu waliyoipata katika tasnia ya intelijensia.
Jambo hili linaweza kuonekana si kitu. Lakini linafanya wengi wa wataalam hawa kufanya uchambuzi wa masuala wanayoyashughulikia kikawaida, badala ya kuyatazama ki intelijensia. Hii ni hatari sana kwa sababu mara nyingi uchambuzi wa kiitelijensia huwa unakuwa tofauti na uchambuzi wa mtaalam wa kawaida. Na hii ndiyo sababu inayomfanya kiongozi wa nchi kuhitaji ushauri wa idara katika masuala ya uchumi (kwa mfano) japokuwa amezungukwa na wachumi. Kumbe afisa wa idara anapaswa kuwa na elimu (shahada) ya kawaida na mafunzo tofauti ya uchambuzi wa uchumi kiitelijensia (analysis) ili weze kufanya kazi yake vizuri. Kinyume cha hapo mchumi wa idara anakuwa hana tofauti na mchumi wa kawaida.
Kwa mfano, wakati mchumi wa kawaida anapoona umuhimu wa kampuni fulani kuwekeza nchini ki uchumi, kisiasa na kijamii, mchumi mchambuzi wa idara (analyst) anapaswa kuona mambo ya ziada yaliyojificha katika uwekezaji huo. Ni lazima mchambuzi huyo aone malengo ya siri yaliyofichwa katika uwekezaji, au mkataba wa uwekezaji ili aweze kuionya serikali. Katika kutekeleza hili ni lazima afisa huyu/idara iwe na taarifa za ziada kutoka vyanzo mbalimbali, na kuzitumia katika uchambuzi huo. Hili ndilo linalofanya ushauri wa idara kuwa tofauti. Kumbe ni muhimu sana idara iwekeze katika kufundisha wachambuzi (analyst) wenye weledi, ari ya kutenda kazi, na wanaosikilizwa na serikali.
(d) Kupanua Mtazamo ili Kusaidia Uelekeo wa Nchi.
TISS ndicho chombo pekee kinachotarajiwa kuwa na taarifa za mambo yote yanayoendelea ulimwenguni, kuyafanyia uchambuzi, na kuishauri serikali kila hatua inayotakiwa kwa kufanya. TISS inapokuwa gizani kuhusiana na jambo lolote, nchi nzima huwa iko gizani. Ni kwa sababu hii, idara ya ujasusi ya Marekani (CIA) hutumia kauli mbiu ya Yesu Kristo katika kufafanua majukumu yake "Nanyi mtaijua kweli, na hiyo kweli itawaweka huru" (Yohana 8:32). Hii ina maana kubwa, kwani nchi isiyojua kinachoendelea duniani ni mfungwa/mtumwa wa wale wanaojua. Kumbe Tanzania inaweza kufikia mapinduzi ya juu kabisa ya kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia endapo TISS itatimiza wajibu wake kwa usahihi.
Tatizo lililopo sasa ni aina ya malengo, mtazamo na uelekeo wa TISS ukilinganisha na nchi nyingine. Ingawa si rahisi kwa mtu wa nje, asiye afisa wa idara kujua kwa usahihi malengo ya TISS, bado malengo na muelekeo huo hujidhihirisha wazi katika utendaji wa serikali. Pale serikali inapokosea katika maamuzi, kila mwenye akili timamu hutambua kuwa TISS imechemsha. Hii ni kwasababu idara ya usalama wa Taifa inayojitambua inapaswa kuwa na uwezo wa kumshawishi kiongozi wa nchi, kumsaidia katika kufanya maamuzi mazuri, kumshauri ili arekebishe pale anapokosea, na kama kiongozi atakuwa hafai idara inatakiwa kufanya mbinu ya kumuondoa (Kwa njia sahihi)
Ni kwa sababu hii idara ishauriwe kuwafunda maafisa wake na kupanua mtazamo wao ili kuweza kuishauri serikali kwa usahihi. Hii ina maana idara ijiikite zaidi katika ujasusi wa kiuchumi, kisayansi na tekonolojia ili kuifanya Tanzania isonge mbele ki uchumi. Nchi nyingi zilizoendelea zimefanikiwa kwa kuiba mipango mizuri ya kiuchumi ya nchi nyingine, kuiba teknolojia mpya, na kuzitumia katika maendeleo yao. Kumbe ni vyema idara iige mfano wa nchi ndogo ya Rwanda ambayo imeweza kujipenyeza kiasi cha kuweka mizizi yake katika nchi nyinginezo kwa manufaa ya nchi na watu wa Rwanda. Huu ni ujasili unaopaswa kuigwa, na hii ndiyo maana halisi ya idara kuwa offensive. Ni muhimu sana idara iende na wakati. Ki msimgi, ni kosa la kiufundi kwa maafisa wa idara kuendelea kufanya kazi kwa mtazamo wa siasa ya ujamaa na kujitegemea, na kutumia mbinu zilezile, wakati dunia imebadilika sana, na inaendelea kubadilika kwa kasi.
Kwa mfano, miezi michache iliyopita nilizungumza na mtu mmoja ninayemfahamu kuwa ni afisa wa TISS. Katika mazungumzo hayo, nilimuuliza kwanini hakuwa na akaunti yoyote ya mtandao wa kijamii kama instagram, facebook, au twitter. Bila kusita alinijibu kuwa hawezi kuwa na akaunti ya aina hiyo kwa sababu yeye ni mtumishi wa serikali. Nilicheka sana! Kwa sababu maafisa wa counter intelligence katika nchi zilizoendelea wanafahamu kuwa katika dunia ya leo mtu asiye na akaunti ya mtandao wa kijamii ni yule tu anayejaribu kujificha (suspect). Kwa kifupi mtu huyo anaweza kuwa gaidi au wakala wa idara ya Usalama wa Taifa ya nchi nyingine. Kwa lugha nyingine kutokuwa na akaunti ya social media ni kitambulisho tosha kuwa wewe ni jasusi, bali kuwa nayo kunasaidia kujificha katika kivuli cha mamilioni ya watu wa kawaida. Mfano huu mdogo unaonesha jinsi mtazamo na fikra za maafisa wetu zisivyobadilika kuendana na wakati.
(e) Kuwepo Kila Mahali (Own the street)
Idara itaweza kufanya kazi nzuri za kiintelijensia endapo itafanikiwa kujipenyeza, kuwepo kila mahali, na kutumia uwepo wake vyema kwa manufaa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuwepo kila mahali maana yake kuwashawishi wananchi kuiamini idara ya Usalama wa Taifa, na kuwa tayari kuipa taarifa muhimu. Ingawa idara inao watoa habari wengi, si rahisi hata kidogo kwa watoa habari hao kuwepo kila mahali. Hata hivyo, ni rahisi kuwafanya wananchi wote kuwa watoa habari wasio rasmi kwa kuwajengea imani na chombo hiki ambacho wengi bado hawakijui vyema Uwepo wa idara kila mahali unaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa uhalifu unaoendelea.
Kwa mfano, wakati wa uongozi wa mhe. Rais John Magufuli wananchi walio wengi walikuwa na hofu ya kuongea mambo ya siasa hadharani kwa kuamini wanaweza kusikiwa na maafisa wa idara, na kukamatwa au kupotezwa. Hii ilikuwa ni sifa nzuri kwa idara yenye matokeo mabaya (Kwa kawaida wananchi wanapaswa kufurahia uwepo wa vyombo vya ulinzi na usalama mahali walipo, si kuogopa). Hata hivyo imani ya uwepo wa idara kila mahali ulisaidia sana kujenga nidhamu ya kazi, uaminifu, kujituma, na uwajibikaji. Katika mahospitali wagonjwa walihudumiwa kwa wakati, na kwenye viwanja vya ndege wasafiri hawakusumbuliwa. Kwa bahati mbaya baada ya kifo cha Magufuli hili limeanza kutoweka, na ndiyo tafsili ya kauli zinazoendelea kuwa "Bora alipokuwepo mwendazake...."
Kumbe ni muhimu sana idara iendelee kutawala mitaa kwa kuwepo kila mahali. Ni vizuri watendaji wa vyombo vingine vya ulinzi na usalama wajue kuwa idara ipo, inawaangalia, na kuwa watumishi wasio waaminifu wanaweza kushughurikiwa muda wowote ule. Aidha, watu wa idara zote za serikali kwa mfano, TRA, Mahakama na kadharika waone matokeo ya idara kuwepo kila mahali, na hivyo wasithubutu kuchukua rushwa au kufanya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu. Zaidi sana, majasusi ,magaidi na maadui wote wa Taifa waone hofu ya kujipenyeza nchini kwa kujua idara ipo kila mahali.

(f) Uteuzi wa Maafisa na Mafunzo.
Suala la kufanya kazi kwa weledi na taaluma linakwenda sambamba na suala la uteuzi wa maafisa, mafunzo na uajiri. Idara inapaswa ifanye marekebisho makubwa katika utaratibu wake wa ajira na mafunzo ili kupata maafisa bora, wenye nidhamu, na watakaozingatia kanuni na miiko ya utendaji wa idara. Katika kutimiza hili idara inapaswa kuondoa ubinafsi unaopelekea kuajiriwa kwa ndugu na jamaa wa maafisa wa idara, hata kama watu hao hawana sifa stahiki za kuwa maafisa wa idara. Ni muhimu kurugenzi ya uajiri na mafunzo katika idara (DRRT) ihakikishe wote wanaoomba nafasi hizo wanapitishwa katika chekeche la kuwachuja bila kujali wanahusiana na nani.
Pamoja na hilo idara iboreshe mafunzo ya awali ya vijana wanaojiunga na idara ili maafisa wapya waweze kuwa na sifa stahiki za kuitwa maafisa wa idara. Miaka ya nyuma (1980s) idara ilikuwa ikisifika kwa kuwa na mafunzo magumu, na ya uhakika kiasi cha maafisa wake kuheshimika kila kona. Kadri miaka ilivyosonga mbele mafunzo hayo yameelekea kulegezwa kiasi cha kuidharilisha idara. Ni muhimu sana maafisa wafundishwe mafunzo ya kijeshi, mbinu za kujilinda kwa mikono mitupu, na mengine yote yanayopaswa afisa wa idara hiyo kujua kwa undani, sio kubabaisha tu.
(g) Usimamizi wa Maafisa (Supervision)
Mojawapo ya mambo yanayoweza kukwamisha utendaji wa idara ni usimamizi wa maafisa wake, hasa walioko mikoani na mawilayani. Mikoa na wilaya nyingi hudumaa kiutendaji kutokana na kuteuliwa kwa watu wasiokuwa na uwezo wa kuongoza vituo hivyo. Miaka ya nyuma jambo hili lilisababisha migomo baridi kila ilipoonekana afisa aliyepewa wadhifa ana cheo cha chini (junior), na elimu ndogo kuliko aliowakuta kituoni. Idara ilijaribu kurekebisha hili kwa kuweka utaratibu uliotaka afisa anayeteuliwa kupewa wadhifa fulani awe na shahada ya chuo kikuu, na apandishwe cheo mara mbili ili kufikia ngazi inayohitajika kushika wadhifa ule.
Utaratibu huu umesababisha matatizo makubwa zaidi. Kwanza, vijana wengi walipandishwa vyeo kwa kasi na kupewa nafasi za juu bila kuzingatia uwezo wao wa utendaji. Pili, vijana hao waliposhindwa majukumu hayo mazito, walibadilishiwa kazi (kupewa kazi nyepesi) bila kupunguzwa vyeo walivyopewa kwa mkurulo na hivyo kuendelea kulipwa mishahara mikubwa wasiyostahili. Matokeo yake ni uwepo wa maafisa wengi, vijana wenye vyeo vikubwa, lakini wasioisaidia idara ki utendaji. Vijana hao wamekuwa kero kwa maafisa wa muda mrefu (seniors) wenye weledi na uzoefu wa kazi, ambao wamejikuta wakiwa chini ya vijana waliopandishwa vyeo kwa mkurulo.
Kumbe Idara inapaswa kuangalia sana utaratibu wake wa uteuzi wa viongozi, na upandishaji vyeo. Idara iangalie kwa makini na kujiridhisha uwepo wa haja ya kumpandisha cheo kwa mkurulo afisa yeyote kabla ya kufanya hivyo. Aidha, iweke utaratibu wa mafunzo maalum kwa wale waliopandishwa vyeo na kupewa nyadhifa nzito. Ni muhimu pia mafunzo hayo yanaendane na aina ya kazi wanayokwenda kuifanya, badala ya kuwapatia mafunzo ya jumla tu. Nasisitiza kuwa idara izingatie mafunzo yanayowaandaa maafisa kuendana na changamoto za dunia ya leo hususani katika habari, tekonolojia, na kadhalika.
Ni imani yangu kuwa makala hii itasaidia kutoa mwanga kidogo wa jinsi wananchi wa kawaida wanavyoitazama idara ya Usalama wa Taifa, na mabadiliko wanayotarajia.
Ustawi wa Tanzania - Jukumu letu sote.
Uwe na Amani.
Rev. Godwin Chilewa
Komentarji