top of page

Mgogoro wa Congo: Funzo Kubwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki

Mgogoro unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hasa kati ya serikali na kundi la waasi la M23, umeibua maswali makubwa kuhusu uwezo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika kusimamia amani na usalama wa eneo lake. Pamoja na juhudi kadhaa za kidiplomasia na kijeshi, bado mgogoro huu unaendelea, ukionyesha udhaifu wa jumuiya hii katika kushughulikia migogoro ya aina hii.


Ziko sababu nyingi zinazofanya Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) ilegelege, kuwa ya kisiasa zaidi na kushindwa kutatua migogoro yake. Sababu ya kwanza, kama ilivyojionesha hivi karibuni ni kuwa haina jeshi la pamoja lenye mamlaka ya moja kwa moja kushughulikia migogoro ya kivita ndani ya nchi wanachama. Ingawa lipo Jeshi la Jumuiya ya Afrika (African Standby Force - ASF) lenye dhamana ya ulinzi wa amani barani, halina muundo thabiti wa utekelezaji ndani ya EAC. Hii ndiyo sababu iliyofanya kikosi cha EAC kilichopelekwa DRC kushindwa kuleta suluhu ya haraka kutokana na changamoto za kisera na ukosefu wa rasilimali za kijeshi na kifedha.


Pili, kuna mgongano mkubwa wa maslahi kwa nchi wanachama wa EAC . Baadhi ya nchi zinashutumiwa kwa kuwa na maslahi yanayokinzana katika mgogoro wa DRC, na hata kuchochea vurugu. Kimsingi EAC haina nguvu ya kiitikadi wala malengo ya pamoja yanayolenga kuzifanya nchi washirika kujitambua kama wamoja. Tofauti za kiasili, kikabila na kimtazamo bado ziko palepale. Kwa ujumla kila nchi mwanachama inaangalia jinsi itakavyojinufaisha binafsi kutokana na EAC badala ya kuimarisha undugu, umoja na ustawi wa jumla.


Kwa mfano, Rwanda inatajwa mara kwa mara kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na kundi la M23, huku Uganda na Burundi zikiwa na majeshi katika DRC kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kupambana na waasi wa ADF. Nchi hizi zinafanya hivi kwa malengo ya ustawi binafsi badala ya kujenga EAC. Migongano hii inafanya iwe vigumu kwa EAC kuwa na msimamo mmoja wa pamoja wa kumaliza mgogoro.


Tatu, ni ukosefu wa mifumo imara ya kushughulikia matatizo na majanga. EAC haina chombo madhubuti cha utatuzi wa migogoro ambacho kinaweza kushughulikia migogoro kama huu wa DRC kwa haraka na kwa njia za kina. Juhudi za kidiplomasia, kama zile zilizokuwa zikiongozwa na Angola na Kenya, zimekuwa na mafanikio madogo kutokana na ukosefu wa uwezo wa utekelezaji wa maazimio yanayofikiwa.


Pamoja na hilo, EAC haina ushirikiano thabiti wa kijasusi na mfumo wa udhibiti silaha. Jumuia inakabiliwa na changamoto kubwa ya kudhibiti mtiririko wa silaha haramu, hasa kupitia mipaka inayopenyeka kwa urahisi. Eneo la Maziwa Makuu lina historia ndefu ya usambazaji wa silaha haramu, hali inayochangia kuendeleza mizozo ya waasi kama M23. Ukosefu wa ushirikiano wa kijasusi kati ya mataifa ya EAC unafanya iwe vigumu kudhibiti makundi yenye silaha na hata wanajeshi wa kukodi.


Sambama na hili EAC inakabiliwa na changamoto ya kuwa na taasisi za kiuchumi zilizo imara. Kwa kiasi kikubwa, migogoro ya eneo la Maziwa Makuu, ikiwa ni pamoja na DRC, inachochewa na mifumo dhaifu ya kiutawala, rushwa, na ukosefu wa maendeleo ya kiuchumi. Nchi nyingi za EAC bado zinakabiliwa na changamoto ya usimamizi mbovu wa rasilimali, hali inayosababisha baadhi ya makundi kutumia vurugu kudai haki zao au kushindania utajiri wa rasilimali za DRC kama madini.


Ili kuimarisha Jumuia na kuondoa matatizo yanayoikabili, EAC inapaswa kuunda jeshi la pamoja lenye mamlaka ya haraka ya kuingilia kati migogoro ndani ya nchi wanachama. Jeshi hili linapaswa kuwa na ufadhili wa moja kwa moja kutoka kwa nchi wanachama na liwe na mfumo wa maamuzi wa haraka ili kuepuka ucheleweshaji wa operesheni kama ilivyoshuhudiwa DRC.


EAC inapaswa kuwa na chombo madhubuti cha utatuzi wa migogoro chenye mamlaka ya kisheria ya kusimamia migogoro kati ya nchi wanachama na ndani ya nchi husika. Hii inajumuisha kuunda mahakama au jopo la waamuzi wa kimataifa ambalo litashughulikia malalamiko ya nchi wanachama na pande zinazozozana.


Ni muhimu pia nchi wanachama zijenge imani na kupunguza migongano ya kimaslahi. Viongozi wa jumuia wanapaswa kuwa na lengo la dhati la kuimarisha umoja na undugu, na kuondoa dhana za kibaguzi zilizojengwa na wakoloni. Ni muhimu nchi wanachama kuwa na mazungumzo ya wazi kuhusu maslahi yao katika eneo la Maziwa Makuu na kuondoa uhasama wa chinichini. Diplomasia ya kisiri na ushawishi wa moja kwa moja wa baadhi ya mataifa makubwa nje ya Afrika unapaswa kudhibitiwa ili kuhakikisha kuwa suluhisho linatokana na Waafrika wenyewe.


Ili kuimarisha usalama wake, ni muhimu sana EAC iunde mfumo thabiti wa ushirikiano wa kijasusi, na udhibiti wa silaha . EAC inapaswa kuwekeza katika mifumo ya pamoja ya kijasusi inayohusisha teknolojia ya kisasa, na ili kudhibiti biashara haramu ya silaha katika eneo lake. Hii inajumuisha kuimarisha ulinzi wa mipaka na kushirikiana kwa karibu na mashirika ya kimataifa yanayohusika na udhibiti wa silaha.


Haya yote yanapaswa kwenda sambamba na uwekezaji katika elimu, afya, na miundombinu ili kupunguza umasikini, ambao mara nyingi ni kichocheo cha migogoro. Pia, zinapaswa kuhakikisha kuwa rasilimali za asili, hasa madini, zinawanufaisha wananchi wa kawaida badala ya kuwanufaisha wachache.


Hitimisho


Mgogoro wa DRC ni onyo kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu udhaifu wake katika kusimamia amani na usalama wa eneo lake. Bila maboresho katika mifumo ya kijeshi, kidiplomasia, kiuchumi, na kijasusi, EAC itaendelea kuwa taasisi dhaifu isiyoweza kutatua migogoro inayozidi kuongezeka. Ni wakati sasa kwa viongozi wa EAC kuungana kwa dhati ili kujenga jumuiya imara inayoweza kukabiliana na changamoto za usalama na maendeleo kwa ufanisi.

 
 
 

Comments


bottom of page