Suleiman Mombo Atadumu Nafasi ya DGIS?
- Rev. Godwin Chilewa
- Aug 8, 2024
- 5 min read
Updated: Sep 17, 2024

Anaitwa Suleiman Abubakar Mombo, mzaliwa wa Tabora, lakini majasusi wenzie, hususan wanaomjua vyema kule mjengoni humwita “Mzee wa shoka” jina alilopewa alipokuwa mafunzoni kwenye chuo cha maafisa usalama wa Taifa Malindi. Wanaojua kwanini alipewa jina hilo yamkini hawatasita kuungana nami kwa kusema bwana Mombo ni mtu sahihi kabisa kwa nafasi ya DGIS, ataitendea haki nafasi hiyo, na kama lisipotokea la kutokea basi ndiye mtu atakayeshika wadhifa huo mpaka Rais Samia Suluhu atakapomaliza muda wake.
Kwa kifupi Mombo au Mzee wa shoka (kama nitakavyoendelea kumwita hapa) alifaa kupewa nafasi hii miaka mingi iliyopita. Huyu ni mmoja wa maafisa wachache wenye uwezo mkubwa katika kusimamia operesheni za kijasusi, kuchambua mambo, kufanya uamuzi wa haraka na sahihi na kutoa ushauri unaofaa bila hofu, unafiki au kupindapinda mambo.
Mombo anayajua vyema majukumu na matatizo ya maafisa wa medani kwa kwani yeye mwenyewe amekulia ndani ya idara, na kupitia hatua zilezile wanazopitia maafisa wengine katika kupanda ngazi ndani ya idara. Hili limemfanya awe mahili katika uongozi wa kiutawala na kioperesheni. Anawajua vyema watu wa chini yake tofauti na ma DG wengine waliokuwa wakiletwa toka nje ya idara.
Kuhusu elimu, bwana Mombo ni msomi aliyehitimu shahada yake ya kwanza nchini India, na akajiendeleza katika masomo ya juu. Alipokuwa masomoni nchini India miaka ya mwanzoni mwa 1990 Bwana Mombo ndiye mwanafunzi pekee wa kundi lake aliyefanikiwa kupata shahada ya daraja la kwanza (Summa Cum Laude). Aidha afisa huyo anazungumza kwa ufasaha lugha ya kihindi. Kabla ya kupanda ngazi bwana Mombo aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya idara ikiwa pamoja na DSO, RSO, afisa wa ubalozi, na nyadhifa nyingine za siri ndani ya idara.
Pengine utafikiri nimeamua kummwagia sifa hizi bwana Mombo kwa kuwa tayari ameshateuliwa kuwa mkurugenzi mkuu wa idara. Hiyo si kweli. Kama utakumbuka huko nyuma niliwahi kuandika makala iitwayo TISS MLINZI ANAYESINZIA. Kwenye makala hiyo iliyochapishwa tarehe 6 April 2022 kwenye tovuti hii nilieleza kwa kina changamoto zinaoikabili idara kwa kadri zinavyoonekana kwa jicho la nje, na kushauri mambo yanayotakiwa kufanyika ili kuiokoa idara hiyo.
Mojawapo ya mambo niliyoshauri ilikuwa kumuondoa DGIS wa wakati huo bwana Diwani Msuya na kumpa nafasi hiyo mmojawapo kati ya maafisa watatu niliowataja. Maafisa hao ni James Kaji aliyekuwa mkuu wa kikosi cha kupambana na madawa ya kulevya, Suleiman Abubakar Mombo aliyekuwa afisa mwandamizi kwenye ubalozi wa Tanzania nchini Brazil na Makungu Msalika aliyekuwa Katibu Tawala wa mkoa (RAS) Tabora wakati huo.
ingawa sina hakika kama mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alipokea ushauri huo na kuufanyia kazi, au la, jambo moja nina hakika nalo, kwamba jinsi nilivyokuwa nikimuona afisa huyo kati ya mamia ya maafisa waandamizi wa idara hiyo, ndivyo pia mheshimiwa rais alivyokuwa akimuona. Kwa kifupi mawazo yetu hayakupishana. Kwa mtazamo huohuo nabashiri bwana Mombo atadumu kwenye nafasi hiyo.
Pengine utajiuliza Mombo, au Mzee wa shoka kama ninavyomwita hapa atafanya lipi jipya ambalo wakurugenzi wengine hawakulifanya? Jibu ni kwamba ataleta ari mpya na nguvu mpya ya utendaji ndani ya idara, atainua heshima ya idara, na kumfanya rais kujenga imani na idara hiyo. Tutarajie mabadiliko makubwa kwenye utendaji na hata utamaduni (culture) ya idara. Mombo ana uwezo wa kushawishi, kusimamia mabadiliko, na kuboresha idara kwa kila hali.
Sambamba na hilo DGIS huyu atapunguza sana msululu wa watu wanaojifanya washauri wa hiari wa rais. Ingawa mheshimiwa rais ana haki ya kumteua mtu yeyote kuwa mshauri wake, wakurugenzi waliopita waliruhusu watu wengi kujipenyeza, kumfikia rais na kumpa ushauri usio rasmi. Hili litapungua sana kwa DGIS huyu. Mombo hapendi watu wanaojipendekeza na au kumpandia kichwani. Anajiamini na kutambua kuwa ushauri wa idara unapaswa kuwa wa mwisho, na hata ushauri wa wataalam unapaswa kuangaliwa na idara kwanza kama hauna ajenda ya siri. Huyo ndiye Mombo.
Kwa sababu hizo huko mbeleni tutegemee kuona idadi ya chawa ikipungua sana, viongozi wazembe wakiondolewa haraka, na wapiga majungu kukosa nafasi. Hii ni kwasababu mojawapo ya mambo yanayomkera Mzee wa shoka ni wapiga majungu, chawa , na watu wanaojaribu kujipatia nafasi kwa kujipendekeza. Mombo hana tabia ya kuendekeza urafiki unaoweza kumuharibia kazi.
Pengine utarudia kuuliza swali lilelile. Je! atadumu ofisini kwa muda gani? Atamaliza miaka mitano au naye ataondolewa baada ya muda mfupi tu? Jibu ni kwamba upo uwezekano mkubwa wa Mombo kudumu kwenye nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka mitano ingawa hilo linategemea mapenzi na uamuzi wa mheshimiwa rais. Mombo ni diplomat mzuri, anajua kujenga mahusiano na watu na kudumisha uhusiano huo.
Si hivyo tu, bali pia Mombo ni mtu anayejiamini na asiyeogopa kusema kweli. Kama mheshimiwa rais anataka mtu anayeweza kumwambia ukweli bila kutia sukari, mtu anayeweza kusema mbili jumlisha mbili ni nne na si tano basi sasa amepata mtu wa aina hiyo. Lakini kama hapendi mtu anayeweza kumwambia ukweli na kwa heshima, basi Mombo hatadumu kwenye hiyo nafasi. Kwa kifupi Mombo hana tabia ya kupindisha mambo.
Kuhusu siasa na upinzani, Mombo ni muumini mkubwa wa demokrasia, uhuru na siasa za vyama vingi nchini. Tutegemee kuona wapinzani wakipewa uhuru zaidi wa kujieleza na kufanya mikutano yao bila kusumbuliwa kama zamani. Hii ni kwa sababu Mombo ni mmojawapo wa maafisa wanaojua maana halisi ya mfumo wa vyama vingi. DGIS huyu aliingia kwenye idara katika kipindi ambacho kuwa askari au afisa wa idara ni lazima uwe na kadi ya Chama Cha Mapinduzi.
Kwa bahati nzuri wakati Mombo akiwa mafunzoni kwenye chuo cha Usalama wa Taifa Malindi, ndipo yalipotokea mapinduzi ya Ulaya mashariki (perestroika) yaliyoisukuma Tanzania kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi. Tukio hili lilisababisha maafisa wote, pamoja na wale waliokuwa mafunzoni kurudisha kadi zao za CCM na kula kiapo cha kuilinda Tanzania mpya chini ya mfumo wa vyama vingi. Mombo pamoja na maafisa wanafunzi wenzake wote walirudisha kadi zao zilizokuwa zimegongwa muhuri wa "Chama Cha Mapinduzi - Tawi la Ofisi ya Rais, Ikulu Dar es Salaam" na kuwa maafisa wapya wa kwanza nje ya mfumo wa na kivuli cha chama tawala. Kama hunielewi fuatilia msimamo wa kisiasa wa katibu mkuu wa CCM wa sasa Bwana Nchimbi.
Pengine utajiuliza tena, kitu gani kinaweza kumuharibia kazi DGIS huyu? Jibu ni biashara! Bwana Mombo ni mtu anayechukia umaskini kama ukoma. Anapenda kujishughulisha, kufanya biashara, na kuwekeza. Tabia hii alikuwanayo tangu akiwa afisa mwanafunzi na mlinzi wa 'Vituo Muhimu" pale kijitonyama. Mombo na rafiki yake marehemu Shomari Bakari Monela (PKA) walikuwa na kawaida ya kununua soda (enzi hizo) kwenye duka la maafisa wa idara (Base Store) na kwenda kuziuza uraiani.
Biashara hiyo halali iliyokuwa wazi kwa maafisa wote haikupata mashabiki wengi kwa sababu ilikuwa na usumbufu mkubwa, na faida kidogo sana. Lakini Mombo na rafiki zake waliifanya kwa bidii kiasi cha maafisa wengine kuwapachika jina la "wazee wa base store". Tangu kipindi hicho Mombo hajawahi kuacha kufanya biashara na kuwekeza kwa njia halali ili kujiongezea kipato. Ni matumaini yangu kuwa jambo hili halitamuingiza kwenye ukakasi kiasi cha kuharibu kazi zake.
By. Rev. Godwin Chilewa
Comments