Ongeza Marafiki Siyo Maadui
- Rev. Godwin Chilewa
- Feb 20, 2021
- 2 min read

Uongozi si lele mama! ni kazi kubwa inayohitaji hekima, busara, weledi, na uvumilivu wa hali ya juu. Unapokuwa kiongozi unalazimika kushughulika na watu wa aina zote, wenye uelewa, na wasio na uelewa; matajiri na maskini, wanaomwamini Mungu, na wasioamini wala kujali habari za Mungu, wanaokupenda na wasiokupenda.
Si ajabu kwamba viongozi wengi wanapotoka madarakani hujikuta wakiwa wametengeneza maadui wengi kuliko marafiki. Naam, kwa sababu wanapokuwa madarakani husahau kwamba siku moja wataondoka. Pengine hii ni mojawapo ya sababu zilizomfanya nabii Yeremia kusema "moyo ni mdanganyifu na tena una ugonjwa wa kufisha“ (Yeremia 17:9-10).

Ni ukweli usiopingika kwamba hakuna mtu asiyekuwa na maadui, na kamwe huwezi kuwalazimisha watu wakupende. Lakini pia uzoefu wa maisha umetufundisha kwamba matendo yetu huchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la marafiki au maadui katika maisha yetu. Maamuzi tunayoyafanya tukiwa katika hisia mbalimbali hututengenezea mazingira ya kupendwa, au kuchukiwa na watu wanaotuzunguka, na kama sisi ni viongozi basi watu walio chini yetu ambao kwa kiasi kikubwa ndio waathirika wa kila neno tunalotamka, au maamuzi tunayofanya.
Hivyo ukitaka kuwa na amani katika maisha yako, ni lazima uoneshe mapenzi ya dhati (yasiyo na unafiki) kwa wengine. Uoneshe kujali matatizo yanayowakabili na kuyashughulikia kwa moyo, pasipo chembe ya unafiki au dalili za kujisafisha na au kujipatia umaarufu..Zaidi sana ni lazima uwe mtu wa msamaha, asiyeendekeza kisasi, aliye tayari kusikiliza na kupokea ushauri na kujishusha.

Yesu Kristo alilisisitiza hili alipokuwa akizungumza na wanafunzi wake kwa kusema "Aliye mkuu kwenu awe kama mdogo na kiongozi awe kama mtumishi" (Luka 22:26).Bila shaka Yesu alisema maneno haya akijua umuhimu wa dhamana ya uongozi na mambo yanayoweza kutokea kiongozi anapojsahau dhamana yake na kuamua kujiinua.
Kumbe ni vema pale ulipo, kwa nafasi yako utafakari tabia na mwenendo wako kama kiongozi. Haijalishi kama nafasi yako ya uongozi ni kubwa au ndogo, ni ya kifamilia au kitaifa, ya kijeshi au kiraia ni vema ujitafakari. Zingatia kwamba maamuzi yako ya leo yana athari kubwa katika maisha yako ya kesho, duniani na mbinguni; kwa sababu hiyo unapaswa kuongeza marafiki na si maadui, kwani ya kesho ni fumbo.
Uwe na amani
Rev. Godwin Chilewa
Comentarios