Sakata la Mkataba wa Bandari - Tatizo ni Misingi Mibovu
- Rev. Godwin Chilewa
- Jul 12, 2023
- 3 min read
Updated: Jul 14, 2023

Ameandika mwandishi wa kitabu cha Zaburi akisema "Kama misingi ikiharibika, Mwenye haki atafanya nini?" (Zaburi 11:3). Hili ndilo ninaloliona kwenye sakata la mkataba wa bandari. Tumesahau ushauri wa wahenga waliosema "Aliyeshika mpini akivuta makali yatakuadhiri" Tukaamua kuwapa vichaa marungu kwenye jumba la vioo." Ni kwa sababu hii namkumbuka sana Bob Marley wa Tanzania, al maruhum Ramadhani Mtoro Ongala, maarufu kama Dr. Remmy, aliyeimba akisema "Ubaya tumeukaribisha wenyewe sasa tumebaki tunalaumiana." Kama hujawahi kusikia maneno haya yenye hekima tafuta wimbo wake uitwao MREMA labda utanielewa.
Kwa kifupi misingi ya utawala na mfumo mzima wa uendeshaji wa nchi yetu una mushkeli, na kama usipofanyiwa marekebisho basi Tanzania itaendelea kufanywa shamba la bibi huku wananchi wakibaki maskini milele. Kwa kifupi mfumo huu unatoa mwanya kwa watu wachache kujijengea himaya imara na dola zisizovunjika ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Watu wa hovyo, wasio waaminifu wanaweza kujipenyeza na au kubebwa kiasi cha kuweza kushika nyadhifa za juu ya kufanya maamuzi makubwa kwa niaba ya watanzania. Kwa kifupi hatuangalii kwa dhati uwezo na usafi wa maadili ya mtu kabla ya kumpa nafasi kubwa. Tunafanya mambo kimazoea.
Miaka michache iliyopita tulishuhudia majambazi, na hata wezi wa kutumia silaha wakipewa madaraka makubwa kiasi cha kupigiwa saluti na IGP au CDF (mkuu wa majeshi). Watu hao walifanya uhalifu waziwazi, walihujumu nchi na kutesa wananchi bila woga. Hakuna aliyewajibishwa wala kushitakiwa kwani walilindwa vilivyo na namba 1 wa wakati huo. Ashukuliwe mwenyezi Mungu mara tu rais Samia alipoingia madarakani aliamua kuwashughulikia vilivyo, japo baadhi yao tu. Hivi sasa wapo waliolipa gharama za makosa yao, wapo wanaosubiri muda uamue hatima yao.
Waswahili husema "pema usijapopema, ukijapema si pema tena" Pamoja na mama kusifiwa 'kwa kuupiga mwingi' bado kwenye serikali yake kuna wengi wanaotuhumiwa kuwa ni wevi na matapeli. Tena wengine hata kwa kujisifu wenyewe, hadharani kwamba pesa walizonazo ni za damu. Wapo waliothubutu hata kutoa uhai wa watanzania kwa kuwauzia/kuwalisha vyakula vyenye sumu ili wao na familia zao watajirike. Hawa tunao kwenye mifumo yetu ya utawala. Wengine wabunge, wanasheria, na wanasiasa maarufu. Halafu eti ndio tuliowapa dhamana ya kuamua hatima ya maisha ya watoto na wajukuu zetu, ikiwemo suala la uidhinishaji mkataba wa uendeshaji bandari. Halafu tunalalamika!
Naam! Watetezi watasema hao ni watu wachache tu katika mfumo mzima wa uongozi na utawala wa serikali yetu. Naam, inawezekana ni kweli. Wapo maafisa, makamanda, waheshimiwa na viongozi wengi wazuri tu. Wanaojua wajibu wao na kuutenda. Lakini kama yasemavyo maandiko matakatifu "Chachu ndogo huharibu donge zima" (Wagalatia 5:9). Inawezekana hao wachache wabovu ndio waliotufikisha hapa tulipo, wakisaidiwa na mfumo mzima tuliojiwekea.
Ukweli ni kwamba viongozi wabovu, hata wakiwa wachache kiasi gani, wanaweza kuangamiza nchi kabisa. Hili si la kusema kwa kunong'ona wala kuficha, maana juzi tu tumeadhimisha siku ya kupiga vita rushwa. Tunapaswa kuwa na viongozi waadilifu, wanasheria wenye weledi, nidhamu ya kimaadili na kiu ya haki. Tena tunapaswa kuwa na wanasiasa wanaojua wajibu wao na haja ya kujenga heshima ya nchi na heshima yao binafsi. Tunahitaji wabunge wenye elimu, weledi, na uchungu wa nchi yetu. Wanaoenda bungeni kwa lengo la kutetea haki, ustawi, na amani ya watanzania, si kutafuta posho na umaarufu tu.
Tatizo leo hii uchama umezidi utanzania. Hili linafanya hata wale wabunge wazuri wachache wakubali kuburuzwa kwa kisingizio cha uchama. Tena suala la kukosoa au kuionya serikali limegeuzwa kuwa dhambi, badala ya kuwa wajibu wa bunge. Remmy Ongala alituonya akisema "Ubaya tumeukaribishe wenyewe sasa tumebaki tunalaumiana na kutukanana" Badala ya kusikia maonyo yake wanasiasa wakamchukia, mpaka uhamiaji wakakataa kumpa uraia wa Tanzania! Nasikia walimpa akiwa anakaribia kufa. Misingi ya nchi yetu imeharibika sana! Yamkini kama tusipoamua kuijenga upya, na kuweka viongozi na wabunge wa kueleweka, nchi hii itageuka kuwa jehanam.
Ni lazima tufanye mapinduzi ya fikra yenye kulenga kurejesha moyo wa kizalendo ulioporwa na ufisadi. Tujifunze wenyewe na kuwafundisha watoto wetu kuipenda Tanzania kwa dhati badala ya kuigeuza shamba la bibi. Kila mtu afikirie kutanguliza utanzania wake mbele badala ya tumbo, uchama, au umaarufu. Tusipofanya hivyo hakuna kiongozi atakayetufaa wala katiba itakayoturidhisha.
Ustawi wa Tanzania - Jukumu letu sote
Rev. Godwin Chilewa
____________
Comentários