top of page

Serikali Ibuni Vyanzo Vipya Vya Mapato

Updated: Nov 1, 2024


Miaka michache iliyopita nilitembelea miji ya Spring, na Denver iliyoko katika jimbo la Colorado nchini Marekani. Nikiwa huko nilipata wasaa wa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii ikiwa pamoja na sehemu maarufu ijulikanayo kama Bustani ya Miungu (Garden of the Gods), Mlima wa Mawe Mekundu (Red Rocks Mountain) na eneo maarufu la michezo ya kutereza kwenye theruji (Ski Cooper). Pamoja na kufurahia mandhari ya vivutio hivyo, niliguswa sana na ubunifu wa wenzetu katika kutengeneza ajira kwa wananchi, na kuweka misingi bora ya vyanzo vya mapato ya serikali.


Ili uweze kunielewa vyema, labda niweke bayana kuwa umbali wa kutoka Texas ninapoishi hadi Spring Colorado ni maili 958 sawa na kilometa 1548. Hivyo ukiendesha kwa gari inaweza kukuchukua masaa kati ya 15 hadi 17 kama hutapoteza muda njiani. Umbali huu ni mkubwa kuliko safari ya Dar es salaam - Mwanza ambapo ni kilometa 1129 tu. Sasa jiulize. Ilikuwaje hata nikashawishika kumbeba mke wangu na familia nzima, na kuendesha umbali huo wote kwenda kutazama mawe tu? Tena ukizingatia mtu mwenyewe niliwahi kuishi wilayani Magu, mkoa wa Mwanza ambako kuna majabali makubwa na ya ajabu kuliko sehemu nyingi za Tanzania?

Jibu ni nguvu wanayotumia wenzetu katika kuwekeza, na kutangaza vivutio vyao. Hawa ni watu wasiofanya kitu kwa kubahatisha. Kila wanachofanya huhakikisha kinalipa, tena kwa faida kubwa. Kwa hiyo wanapoanzisha mradi, au kivutio hufanya kila linalowezekana kuhakikisha wateja wanapatikana, na wakishakuja, watakapoondoka watapeleka sifa njema huko walikotoka. Tena wanajua namna ya kumvuta mtu kwa maneno matamu. Hebu fikiria mtu akikwambia ametembelea "Bustani ya Miungu" unapata picha gani? Kumbe hii ni milima na majabali yaliyojipanga katika bonde tu.



Si jimbo la Colorado pekee linaoingiza pesa kiulaini kupitia vitu vya kawaida kabisa. Kila jimbo la Marekani lina vivutio lukuki vinavyosaidia kuiingizia mapato serikalini, aidha moja kwa moja au kwa mlango wa nyuma. Huku kila ziwa, kila mto, kila bonde la kupendeza au msitu, hicho ni chanzo cha mapato ya serikali. Viko vituo vya makumbusho ya kila kitu. Kuanzia vifaa vya anga, bahari, sayansi, sanaa, jeshi na silaha zake (manoali, vifaru na mizinga) na hata ujasusi (Spy Museum). Hivi vyote ni vyanzo vya mapato yasiyo na kelele kabisa. Serikali hutoza fedha za kiingilio kwenye baadhi ya vivutio hivyo ambapo wananchi hulipa bila kulalamika; na au hupata fedha kwa kuuza vinywaji, vyaakula, nguo na zawadi za ukumbusho.

Mapato haya, yakichanganywa na kodi mbalimbali zinazokusanywa, huiwezesha serikali kugharimia miradi mikubwa, na kuondoa tozo katika vitu visivyo vya lazima. Kwa mfano, serikali hutoa kompyuta mpakato bure kwa wanafunzi wote wa shule za msingi na upili, pamoja na huduma za internet kwa wale wasiokuwanazo majumbani kwao. Serikali pia kwa kutumia program zake huwapa simu bure, na kuwalipia bili zao wale wote wasio na uwezo, ambao pia hupewa chakula bure (Food stamps). Hii ni pamoja na kuwalipa mishahara watu wasio na kazi (unemployed).

Nimeelezea haya yote ili kuonesha haja ya serikali ya Tanzania kufikiria na kubuni vyanzo vipya vya mapato, badala ya kuwatoza wananchi maskini fedha kidogo walizonazo kwenye vijiakaunti au miamala ya simu. Tanzania inavyo vivutio vingi ambavyo kama vikihuishwa vinaweza kutoa ajira kwa wananchi na kuwafanya wao wazirudishe serikalini kwa furaha kupitia matumizi yao. Wananchi wa Tanzania ni watumiaji wazuri sana wa fedha, na kama huamini angalia idadi ya watu waliotembelea viwanja vya sabasaba mwaka huu, na wale wanaohudhuria viwanja vya mpira kuangalia soka.


Kama watu wanaweza kutembelea mabanda ya sabasaba, si ajabu kuwa wanaweza kutembelea vivutio vingine vya ndani kama vikijengwa, na wakihamasishwa kufanya hivyo. Leo hii mtu akitembelea jijini Dar es Salaam, hana sehemu nyingi za kutembelea kwa kujifunza. Zamani kila mtu alikwenda soko la Kariakoo maana lilionekana ndiyo muujiza. Leo hii limekuwa kitu cha kawaida sana. Kwa ujumla hakuna vivutio vya maana.


Ndiyo maana huwa najiuliza sana, kwa nini jeshi la Wananchi wa Tanzania hawafungui eneo kubwa la makumbusho jijini Dar es Salaam kuonesha silaha mbalimbali zilizotumika kumng'oa nduli Iddi Amini. Nina hakika huo ungekuwa mradi mkubwa wa kuliingizia mapato jeshi, kuwafundisha vijana wetu historia, na kuwajaza uzalendo na kiu ya kulitumikia Taifa kwa dhati.

Au kwa nini chuo kikuu cha sayansi na Tiba Muhimbili hakijengi makumbusho ya sayansi na tiba kwa ajili ya kuwaonesha vijana na wazee wetu mfumo wa mwili wa binadamu ulivyo, na kuelekeza jinsi madaktari wanavyotumia sayansi katika kuokoa maisha ya watu? Haya si ndiyo huwa wanayaonesha kwenye mabanda ya sabasaba? kwa nini kisijengwe kituo ambapo wanafunzi wanaotamani kuwa madaktari toka kila kona ya Tanzania wanaweza kutembelea kwa kulipa kiasi fulani cha pesa? Tunashindwa nini? Mbona wenzetu wanafanya na wanaingiza pesa?

Si hivyo tu, huwa najiuliza sana ni wanafunzi wangapi wa sekondari, na hata chuo kikuu waliowahi kutembelea makumbusho ya Taifa? Kwa nini makumbusho hiyo haijitangazi kiasi cha kumfanya kila mwanafunzi awe na kiu ya kuitembelea? Tena kwa nini wizara ya Elimu haishirikiani na vituo vya makumbusho kwa kuweka program zinazohimiza wanafunzi hasa wa shule za msingi na sekondari kwenda kwenye makumbusho au vituo vingine vya aina hiyo?


Na kwanini vivutio kama Mapango ya Amboni Tanga yanafutika kwenye midomo ya watanzania? Wizara ya Utalii inafanya jitihada gani kuboresha vivituo hivi, kuvitangaza, na kuhakikisha watu wanakwenda? Ni ukweli usiopingika kuwa hivi leo Amber Rutty anajulikana zaidi kuliko Mapango ya Amboni, achilia mbali Diamond. Wizara husika haijiulizi tu?

Ni jambo la kushukuru kwamba mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alipata maono ya kutengeneza Royal Tour ili kuutangaza utalii wetu nje. Nina imani hiyo itasaidia mamilioni ya watalii kumiminika nchini kuzitembelea mbuga zetu na vivutio vingine. Lakini hiyo haitoshi. Ni lazima serikali ijikite katika kutengeneza, kuboresha, na kutangaza vivutio vya utalii wa ndani vitakavyowafanya wananchi wa kawaida pia wajenge utamaduni wa kutalii ndani ya nchi yao.


Ziko wilaya kama Rushoto na Tukuyu zenye mazingira na uoto wa asili mzuri, lakini hakuna anayekwenda. Yapo maporomoko ya maji, bustani za maua mazuri ajabu, na hata miamba ya kuvutia kama ile ya bustani ya miungu (Garden of Gods) lakini hatujaipa thamani. Hii ndiyo sababu inayofanya serikali ihangaike na tozo za miamala ya simu.

Tujifunze kwa wenzetu. Nchini Marekani mamlaka za mashule hushirikiana kwa kila hali na vituo mbalimbali vya elimu na uwekezaji kuhakikisha mwananchi anatumia fedha yake kwa furaha ili nchi iingize mapato. Ndiyo maana mtoto wa darasa la kwanza hadi la nne akifanya vizuri darasani hupewa cheti (Honor Roll) na kupuni inayomruhusu kujipatia mlo wa bure McDonard au mgahawa mwingine wowote.


Kupuni hiyo pamoja na kuwa ni zawadi ya bure, humfanya mzazi ajikute akilazimika kwenda kwenye mgahawa huo ili mtoto apate chakula chake. Hiyo humfanya mzazi kushawishika naye kujinunulia chakula chake hata kama hakuwa amepanga. Si hivyo tu, kupuni hiyo humfanya mtoto aanze kujenga mapenzi na mgahawa uliompa zawadi na hivyo kujikuta akiwa mteja wa sasa, au mteja mtarajiwa.

Kumbe ni muhimu sana Tanzania ijue mbinu za ushindani wa kibiashara hasa katika sekta ya utalii. Hilo litnawezekana kama wataalam wetu watajifunza toka kwa wenzetu. Kwa mfano, ziko hoteli kadhaa nchini Marekani, Uturuki, Thailand, na Dubai ambazo mteja anapotaka kuzitembelea hulipa pesa ya package nzima inayojumlisha usafiri wa ndege toka anakotoka, chumba cha kulala, vyakula na vinywaji, na maeneo atakayotembelea kwa siku husika.


Mapango ya Amboni

Hii humsaidia sana muhusika kujua bajeti yake na kuondoa hofu ya kuishiwa ugenini kwani malipo hayo humuwezesha kukaa akiwa huru mpaka siku atakayoondoka. Kwa nini serikali isiyaunganishe mahoteli, na wadau wengine wa utalii ili watumie ndege za Air Tanzania kutoa huduma za aina hii? Naamini utaratibu huu unaweza kusaidia kuondoa changamoto ya kuwa na ndege nyingi zisizoingiza mapato.

Nimalizie kwa kusisitiza kuwa haya niliyoyaorodhesha humu nimeyatumia kama mfano tu. Serikali inaweza kubuni mambo makubwa, na ya maana zaidi kwa kufuata mifano ya wenzetu. Lakini kama itsipolichukulia jambo hili kwa uzito, na kutotafuta vyanzo mbadala vya mapato, itajikuta kila wakati ikirudia kupandisha bei za kodi na tozo zilizokwishawekwa kwenye vinywaji, petroli, miamala ya simu, na vitu vingine vinavyogusa maisha ya wananchi. Ufumbuzi wa kudumu ni kubuni vyanzo vitakavyotengeneza ajira na kuingiza mapato bila kelele.

Ustawi wa Tanzania - Jukumu Letu Sote

Uwe na Amani.

Godwin Chilewa

Comments


bottom of page