Siasa za Alama na Shahada za Heshima: Dalili ya Udhaifu wa Taasisi au Utamaduni Mpya?
Na Rev. Godwin Chilewa

Katika mifumo ya kisasa ya utawala, heshima ya kiongozi hujengwa kwa uzito wa matokeo ya utendaji wake. Kwahiyo, maneno mazuri, nyimbo za sifa, majina matukufu na vyeo vya sifa haviwezi kumuongezea kiongozi heshima hata kidogo kama utendaji wake ni mbovu. Uongozi hupimwa kwa matokeo.
Katika muktadha wa siasa za Tanzania mambo ni tofauti kidogo. Kwa miaka mingi sasa kumekuwa na mwenendo uliokomaa wa viongozi kulundikiwa vyeo na sifa zisizo na msingi thabiti wa kitaaluma, hususan matumizi ya majina kama “Daktari” yanayotokana na shahada za heshima (honorary degrees) badala ya taaluma iliyosomwa na kuthibitishwa.
Mwenendo huu unazidi kukithiri kutokana na ongezeko kubwa la tabia ya uchawa unaoelekea kukubalika na kupewa nafasi kubwa katika siasa za nchi. Tatizo hili linapaswa kuchambuliwa kwa kina na, zaidi ya yote, kuwekewa tahadhari ya kitaifa.
Ni kweli kwamba katika jamii nyingi za Kiafrika, heshima huonyeshwa kwa kutumia majina na vyeo. Hata hivyo, pale utamaduni unapochanganywa na siasa za mamlaka bila mipaka, hutengeneza mazingira ya kupotosha dhana ya uhalali (legitimacy). Kiongozi anapoanza kujengwa kupitia alama (symbols) badala ya matokeo, mfumo mzima wa utawala huanza kupoteza mwelekeo.
Katika diplomasia ya kimataifa, nchi nyingi zilizoendelea hutumia mfumo wa utambulisho ulio rahisi na wa kitaasisi zaidi hususan “Rais,” “Waziri Mkuu,” au “Mheshimiwa” bila kuingiza sifa za ziada zisizo na uhusiano wa moja kwa moja na majukumu ya kiongozi. Hii ni kwa sababu heshima ya kiongozi hutokana na taasisi anayoiwakilisha na utendaji wake, si mapambo ya majina.
Udaktari wa Heshima: Tuzo au Zana ya Kujipamba?
Shahada za heshima zilitengenezwa kwa lengo la kutambua mchango wa mtu katika jamii. Hazikulenga kubadili utambulisho wa kitaaluma wa mhusika. Hata hivyo, baadhi ya viongozi na wanasiasa wamekua wakizitumia kama nyenzo ya kujijengea hadhi ya kitaaluma isiyo halisi.
Matukio ya baadhi ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwemo Joseph Kasheku Musukuma (Mhe. Msukuma) na mbunge wa Morogoro Mashariki Mhe. Babu Tale kununua au kutafuta shahada za udaktari wa heshima kutoka vyuo vya nje kwa lengo la kuitwa “Daktari,” yamezua maswali mazito ya kimaadili na kitaaluma. Hata hivyo hakuna hatua zilizochukuliwa kukemea. Hii inaonesha hili si suala la mtu mmoja mmoja ni dalili ya mfumo unaoruhusu na, kimyakimya, kuhalalisha tabia hii.
Athari kwa Heshima ya Taaluma
Taaluma yoyote ina thamani yake kwa sababu ya juhudi, utafiti, na uthibitisho wa uwezo wa mhusika. Pale ambapo jina “Daktari” linapotumika bila kuzingatia msingi huua heshima ya taaluma. Aidha wanataaluma halisi huonekana sawa na wale wasio na sifa hizo, na jamii hupoteza uwezo wa kutofautisha kati ya uhalali na mapambo
Kwa maneno mengine, matumizi holela ya vyeo vya kitaaluma ni aina ya inflation ya heshima (honor inflation) ambayo huishia kudhoofisha mfumo mzima.
Saikolojia ya Mamlaka: Kujaza Pengo la Uhalali
Kwa mtazamo wa kiintelijensia, tabia ya kujilundikia vyeo inaweza kuashiria mambo mawili: Kwanza ni jaribio la kuongeza uzito wa mamlaka kwa njia ya alama, na pili fidia (compensation) ya upungufu wa uhalali unaotokana na utendaji au taasisi dhaifu
Kadri taasisi zinavyokuwa imara, ndivyo hitaji la kujipamba kwa vyeo linavyopungua. Kinyume chake, kadri taasisi zinavyokuwa dhaifu, ndivyo utegemezi wa alama za mamlaka unavyoongezeka.
Kwa juujuu tatizo hili linaweza kuonekana si kitu. Lakini kiundani lina athari kubwa kitaifa na kimataifa. Ndani ya nchi jambo hili huongeza umbali kati ya viongozi na wananchi, huimarishs utamaduni wa kuabudu watu (personality cult), na kudhoofisha uwajibikaji kwa sababu mjadala huhama kutoka utendaji kwenda hadhi. Si ajabu kwamba hata watumishi wa Mungu ikiwa pamoja na maaskofu, wachungaji na mashekhe nao hivi sasa hujitambulisha kama “Daktari” fulani.
Kimataifa tabia hii huibua taswira ya kutokukomaa kwa itifaki na kudhihirisha dhana ya fidia (compansation) ya udhaifu. Huleta mkanganyiko wa kitaaluma, na huashiria mfumo unaotegemea zaidi ishara kuliko ufanisi. Ingawa diplomasia inaheshimu tofauti za kitamaduni, ulimwengu wa kisasa unathamini zaidi uwazi na uhalisi kuliko majina marefu na sifa za ki-kalubandika.
Kimsingi kiongozi anaweza kuheshimika kwa utendaji na misimamo yake kuliko mavyeo yasiyo na maana. Mfano bora zaidi wa uongozi unaojenga heshima kupitia matokeo ni Julius Nyerere ambaye ya kutunukiwa shahada nyingi za udaktari wa heshima kutoka vyuo vikuu mbalimbali duniani, hakuwahi kujitambulisha kama “Doctor Nyerere,” wala kusisitiza kuitwa hivyo. Badala yake alijulikana zaidi kama “Mwalimu” jina lililotokana na kazi yake, si cheti. Hii ni ishara ya uongozi uliokomaa, unaotambua kwamba heshima ya kweli haitokani na kile unachoitwa, bali kile unachofanya.
Kinyume chake, kiongozi aliyejipachika mivyeo na sifa nyingi za hovyo alikuwa rais wa Uganda, jenerali Iddi Amin Dada. Rais huyu alijiita Mheshimiwa Sana (His Excellency), Rais wa Maisha (President for Life), Field Marshal Alhaji Daktari Idi Amin Dada, VC, DSO, MC, CBE, Bwana wa Wanyama wote wa nchi kavu na Samaki wote wa baharini, na Mshindi wa Dola ya Uingereza barani Afrika kwa ujumla na Uganda kwa pekee.” Pamoja na misifa hii yote, Amini alikuwa rais wa hovyo aliyeharibu kabisa uchumi na amani ya Uganda.
Ushauri kwa Serikali
Ni wakati sasa kwa serikali kuchukua hatua za kimfumo ili kuondoa janga hili la kitaaluma. Ni vyema vyombo husika viweke miongozo ya wazi kuhusu matumizi ya vyeo vya heshima na kutenganisha wazi kati ya shahada za kitaaluma na za heshima. Ni muhimu pia serikali ipige marufuku matumizi ya majina yanayoweza kupotosha umma kuhusu sifa za mtu. Ni aibu kwa taifa kuwa na wabunge au viongozi wa kitaifa walionunua udaktari wa heshima, na bado wakarihusiwa kutumia utambulisho huo.
Pamoja na hayo serikali inapaswa kuhimiza utamaduni wa kuthamini utendaji kuliko majina
Bila hatua hizi, taifa lina hatari ya kudhofisha mifumo yake ya kitaaluma, kupoteza uaminifu wa wananchi, na kujenga kizazi cha viongozi wanaotafuta hadhi badala ya kuwatumikia wananchi.
Ni muhimu sana ieleweke kwamba heshima ya Rais au Makamu wa Rais haiongezeki kwa kuitwa “Daktari.” Inaongezeka kwa imani aliyopewa na wananchi kwa kumpigia kura, kwa maamuzi sahihi, uongozi thabiti, na matokeo yanayoonekana kwa wananchi. Vyeo vinaweza kupamba jina, lakini haviwezi kuficha ukweli wa utendaji.
Zaidi ya yote, serikali inapaswa kulichukulia suala hili kama ishara ya tahadhari. Kwamba pale ambapo wanasiasa au viongozi wenye nyadhifa nyingine majina yao yanakuwa makubwa kuliko matokeo ya kazi zao, basi msingi wa uongozi huanza kuyumba.
Ni wakati wa kurejesha mizani: kutoka kwenye siasa za majina kwenda kwenye siasa za matokeo.
Uwe na amani.






Comments