SIASA ZA HOFU DHIDI YA UKWELI: Kwa Nini Kauli ya Nchimbi Inatikisa Mfumo?
Na Rev. Godwin Chilewa

Hivi sasa kuna wimbi kubwa la mashambulizi ya maneno dhidi ya Makamu wa Rais, mheshimiwa Emmanuel Nchimbi. Wimbi hilo limeibuka kufuatia hotuba yake kwa watetezi wa haki za binadamu. Katika hotuba hiyo, Mhe. Nchimbi alisisitiza umuhimu wa Watanzania kupambania Katiba mpya, kauli ambayo kimsingi si ngeni ndani ya mjadala wa kitaifa, bali imekuwa sehemu ya ajenda ya muda mrefu ya mageuzi ya kisiasa nchini.
Hata hivyo, kilichozua mjadala mkali si wito wa Katiba mpya wenyewe, bali tafsiri iliyopotoshwa ya baadhi ya kauli zake, hasa pale aliposema kuwa “Katiba ya sasa inampa Rais madaraka yasiyo na maana.” Kauli hii imechukuliwa na baadhi ya wadau kama ishara ya kumkosoa au hata kumsaliti Rais, Samia Suluhu Hassan. Lakini je, huo ndio ukweli?
NCHIMBI ALIMAANISHA NINI HASA?
Kwa mtazamo wa kiintelijensia, ni muhimu kuchambua kauli katika muktadha wake halisi. Nchimbi hakuwa akimdhalilisha Rais wala kupunguza mamlaka ya kikatiba ya urais, bali alikuwa akitoa hoja ya kitaasisi: kwamba Katiba ya sasa imejikita katika mfumo unaokusanya madaraka makubwa mno kwa mtu mmoja.
Hii si hoja mpya, ni mjadala uliowahi kujitokeza mara nyingi katika historia ya siasa za Tanzania.
Kwa kusema “madaraka yasiyo na maana,” tafsiri sahihi si kwamba madaraka hayo hayana thamani, bali yanaweza kuwa yasiyodhibitiwa ipasavyo (unchecked powers), jambo linaloweza kuleta hatari kwa utawala bora na uwajibikaji wa taasisi. Kwa lugha nyingine, Nchimbi alikuwa akisisitiza haja ya kuweka mizani ya madaraka (checks and balances) ili kuimarisha demokrasia na kuondoa uwezekano wa matumizi mabaya ya mamlaka.
JE, HII NI KINYUME NA RAIS SAMIA?
Kinyume chake, Nchimbi alieleza wazi kuwa wazo la Katiba mpya ni sehemu ya maono ya Rais Samia mwenyewe. Hii ina maana kuwa hotuba yake haikuwa ya kupingana na Rais, bali ya kuunga mkono ajenda ya mageuzi ambayo tayari imeashiriwa na uongozi wa juu wa nchi.
Kumshtumu Nchimbi kwa “usaliti” ni ama kutokuelewa kwa kina hoja yake, au ni jitihada za makusudi za kupotosha umma. Kiintelijensia, hali hii huashiria uwepo wa makundi yenye hofu ya mabadiliko hasa wale wanaonufaika na mfumo uliopo wa madaraka usio na mizania.
NAFASI YA NCHIMBI KIKATIBA
Ni muhimu pia kuzingatia kwamba Nchimbi yuko hatua moja tu kutoka kushika madaraka ya juu kabisa ya nchi endapo kutatokea dharura. Hivyo basi, kauli yake ina uzito wa kipekee kwani ni mtu anayeelewa uzito wa madaraka hayo na athari zake kwa taifa. Kwa mantiki hiyo, kauli yake inaweza kutafsiriwa kama tahadhari ya kiuongozi na sauti ya mtu anayejua hatari ya mfumo usio na uwiano wa madaraka. Hii ni ishara ya ukomavu wa kisiasa, si udhaifu.
NANI ANAPOTOSHA NA KWA AJENDA GANI?
Swali ambalo kila mtu anapaswa kujiuliza ni hili, “ni nani wanaopotosha kauli za Nchimbi, na kwa faida ya nani?” Uchambuzi unaonesha uwezekano wa makundi matatu. Kwanza ni kundi la Wanaonufaika na mfumo uliopo ambao wanaona Katiba mpya kama tishio kwa maslahi yao binafsi au ya kisiasa. Pili ni Wanasiasa wa taharuki, wanaotumia propaganda ili kujijengea mtaji wa kisiasa kwa kuibua migogoro isiyokuwepo. Kundi la tatu ni “CHAWA” wa kisiasa: kundi la watu wanaotafuta kujipendekeza kwa viongozi kwa kupotosha ukweli na kueneza hofu. Makundi haya yanaweza kuwa na lengo la kuzima mjadala wa Katiba mpya kwa kugeuza hoja ya msingi kuwa mgogoro wa kisiasa binafsi.
Katika mazingira haya, ni wazi kuwa Mhe. Nchimbi hajafanya kosa la kisiasa, bali ameibua mjadala wa msingi kuhusu mustakabali wa taifa. Huu ni mjadala unaohitaji ujasiri, si lawama.
Ni muhimu kwa viongozi wenye maono kama Nchimbi kutotikiswa na kelele za upotoshaji. Taifa linahitaji mjadala wa wazi, wa kina, na wa ujenzi, sio propaganda.
Kwa hiyo, ujumbe wa mwisho ni huu, Makamu wa Rais Nchimbi asitikiswe na “chawa” wa kisiasa wasioitakia mema Tanzania. Historia inaonesha kuwa mageuzi ya kweli huanza kwa sauti chache jasiri zinazothubutu kusema ukweli, hata pale ambapo ukweli huo haupendwi na wengi. Na mara nyingi, sauti hizo ndizo huandika mustakabali wa taifa.
Uwe na amani






Comments