top of page

TANESCO Wakatwa Mishahara



Maelfu ya wafanyakazi wa shirika la usambazaji umeme nchini (TANESCO) wamejikuta wakibubujikwa machozi baada ya mishahara yao kupunguzwa kwa asilimia kumi na nane (18%) badala ya kuongezeka kama walivyokuwa wakitarajia. Kufuatia kupunguzwa huko, mfanyakazi aliyekuwa akilipwa shilingi milioni mbili na laki tatu (Tshs. 2,300,000) kwa mwezi, sasa atakuwa akilipwa shilingi milioni moja na laki tisa (Tshs.1,900,000) tu, kiwango ambacho ni pungufu kwa shilingi laki nne (Tshs. 400,000) kwa mwezi sawa na shilingi milioni nne na laki nane (Tshs. 4,800,000) kwa mwaka. Hali iliyowaongezea ugumu wa maisha.


Kupunguzwa kwa mishahara hiyo kumetokana na matatizo ya kiufundi yaliyojitokeza wakati wa uingizaji taarifa za wafanyakazi wa shirika hilo kwenye mpango mpya wa huduma za wafanyakazi (new scheme of service). Ieleweke kwamba kwa muda wa miaka zaidi ya ishirini (20) TANESCO ilikuwa haina muundo bora wa huduma za watumishi. Hali hiyo ilisababisha matatizo makubwa katika ajira za wafanyakazi hususan masuala ya mishahara, upandishaji vyeo, marupurupu na stahiki nyinginezo. Hivi karibuni uongozi ulilivalia njuga suala hilo na hatimaye mwaka huu shirika lilifanikiwa kukamilisha muundo mpya wa huduma za watumishi wake (new scheme of service).


Tatizo la kupunguzwa kwa mishahara lilijitokeza wakati wa kuingiza taarifa za wafanyakazi kwenye mfumo mpya kwa sababu mfumo huo haukuandaliwa kwa ajili ya kuhamisha wafanyakazi, bali kwa ajira mpya. Kwa sababu hiyo taarifa zilizoingizwa hazikubaki kama zilivyotakiwa, badala yake mfumo ulibadilisha data kutegemea maswali na majibu yaliyojitokeza. Kwa mfano, mfanyakazi aliyeajiliwa kama fundi (technician) miaka kadhaa iliyopita na kufikia cheo cha fundi mwandamizi (senior technician) mfumo huo uliweza kusoma na kuingiza taarifa zake kwa usahihi na hivyo kulipwa mshahara sahihi. Lakini kama fundi huyohuyo alijiendeleza (shule) na kufanikiwa kupata shahada ya uhandisi (BsC. Engineering) mwaka mmoja uliopita, na hivyo kupandishwa cheo toka fundi (technician) kuwa mhandisi (Engineer) mfumo huo ulikataa kumtambua na hivyo kumuhesabu kama mfanyakazi mpya, hali iliyopelekea kupunguzwa kwa mshahara wake.


Hali hii imesababisha utata mkubwa katika shirika hilo ukizingatia kuwa asilimia kubwa ya watumishi wa TANESCO huajiriwa kama mafundi (technicians) na kujiendeleza kielimu miaka mingi baadae. Inakatisha tamaa fundi (technician) aliyejiendeleza na kupandishwa kuwa wahandisi anapooona analipwa mshahara midogo kuliko mwenzake ambaye hakuona umuhimu wa kwenda shule. Hii si sahihi ki utu wala kitaaluma.


Baadhi ya wafanyakazi walioulalamikia uongozi wa TANESCO waliambiwa kuwa mishahara yao itajirekebisha yenyewe baada ya miaka mitatu au minne, hivyo wasiwe na wasiwasi. Hata hivyo jibu hilo halikuwaridhisha wafanyakazi hao kwani kitendo cha kusubiri miaka minne kitawaweka katika hali ngumu na kuwarudisha nyuma kimaendeleo. Wapo pia wafanyakazi ambao hawakwenda kusoma, lakini mishahara yao imepunguzwa kwa sababu zisizoeleweka.


Tatizo hili linaweza kuonekana kama dogo, lakini athari zake zinaweza kuwa kubwa sana kwa shirika na kwa jamii. Tukumbuke kuwa wafanyakazi hawa wana familia zao, na watu lukuki wanaowategemea. Kitendo cha kuwaondolea shilingi milioni nne na laki nane (Tshs 4,800,000) katika kipato chao cha mwaka ni kuwatia umaskini. Hii ni pesa ambayo ingemsaidia mfanyakazi huyu katika kipindi hiki cha hali ngumu ya maisha. Inaeleweka kuwa tatizo hili limejitokeza wakati shirika likijitahidi kuboresha muundo wake wa utumishi kwa faida ya wafanyakazi. Hata hivyo bado si sahihi kwa mfanyakazi kubeba gharama za makosa ya shirika au ya mfumo wowote wa uendeshaji.


Ni muhimu pia kuzingatia kuwa wafanyakazi hawa ndiyo hasa wanaofanya kazi za kiufundi zinazoliwezesha shirika hilo kujitegemea, na kupiga hatua za kimaendeleo. Wako wanaofanya kazi zinazowakutanisha moja kwa moja na wateja, na wengine kazi zinazodhibiti mifumo mikubwa ya umeme nchini. Kutowapa stahiki zao kunaweza kuwapunguzia ari ya kufanya kazi na kuwachochea kuomba rushwa, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. Ikumbukwe hawa ndiyo wanaoweza kuwasha na kuzima umeme wa nchi nzima kwa sababu wanazozijua wenyewe. Ni vyema serikali iushauri uongozi wa TANESCO kuhakikisha wanyonge hao wanalipwa kama inavyostahili.Tusipoziba ufa tutajenga ukuta.


Ustawi wa Tanzania - Jukumu letu sote

Uwe na amani.

Rev. Godwin Chilewa

Comments


bottom of page