top of page

TISS, Uwajibikaji na Hatari ya Ujumlishaji Usio na Msingi


Na. Rev. Godwin Chilewa


Katika wiki za hivi karibuni, kumekuwa na wito wa kutaka kuitangaza Idara ya Usalama wa Taifa Tanzania (TISS) kama kundi la kigaidi. Wito huu, unaochochewa na ripoti za vurugu na matukio ya baada ya uchaguzi, madai ya utekaji, na ukiukwaji wa haki za binadamu, unaonyesha hofu halisi ya wananchi. Hata hivyo, madai ya kutaka kuitangaza taasisi hii kuwa “kundi la kigaidi” ni jambo lisilofaa kisheria na kimaadili.


Ukiangalia kwa kina utagundua kuwa chanzo cha mjadala huu ni tatizo kubwa zaidi, lisilozungumzwa: kukomaa kwa tabia ya kuchukulia mambo ki ujumla bila uchambuzi makini katika siasa za Tanzania.


Ieleweke kwamba TISS si kundi la wahuni wala mtandao wa siri usio rasmi. Ni taasisi ya serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania, ikiwa na majukumu yaliyoainishwa wazi: kulinda usalama wa taifa, kukusanya taarifa za kiintelijensia, na kuishauri serikali kuhusu matishio au viashiria vya vitendo vya kiadui vinavyoweza kuhatarisha taifa. Maafisa wa TISS hufanyiwa upekuzi wa kina, hupatiwa mafunzo, na hudhibitiwa kwa kanuni na mifumo ya kisheria. Kwahiyo kuifananisha taasisi hii na kundi la ugaidi ni kupuuza misingi ya utawala wa sheria na muundo wa taasisi za dola.


Tatizo hili la kuchukulia mambo ki ujumla si jipya. Vyama vya upinzani kama CHADEMA, licha ya kuwa na uhalali kisheria, mara nyingi vimekuwa vikibandikwa lebo ya “wasaliti” na baadhi ya wanasiasa. Wanaofanya hivi huwa hawawatofautishi watu binafsi, matendo yao, wala kutoa ushahidi, bali huhukumu kundi zima. Matokeo yake jamii huanza kuwaona wanachama wote wa upinzani kama maadui wa taifa, jambo ambalo si la kweli wala la haki.


Mantiki hiyo hiyo isiyo sahihi ndiyo inatumika dhidi ya TISS. Madai yanayotolewa na baadhi ya watu hata kama ni mazito kiasi gani, yanatumika kulaani taasisi nzima. Lakini taasisi, kama ilivyo kwa vyama vya siasa, zinaundwa na watu wenye majukumu tofauti, viwango tofauti vya mamlaka, na mitazamo tofauti. Kudhani kuwa wote wana hatia sawa ni kupotosha haki na mantiki.


Hii haimaanishi kuwa TISS au chombo chochote cha usalama hakipaswi kuchunguzwa. Kinyume chake, uzito wa madai yaliyotolewa unahitaji uchunguzi makini na wa kisheria. Madai ya mauaji, utekaji, na matumizi mabaya ya madaraka iwe Dar es Salaam, Mwanza au mahali pengine yanapaswa kuchunguzwa kwa uhuru na umakini. Iwapo maafisa binafsi, kutoka TISS au vyombo vingine, watabainika kuhusika na uhalifu, basi watapaswa kufikishwa mahakamani na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.


Lakini pia tunapotafakari matukio ya Oktoba 29 ni muhimu kujiuliza swali ambalo mara nyingi halizingatiwi katika mjadala wenye hisia kali: je, inawezekana kwamba ndani ya TISS au mfumo unaolalamikiwa kulikuwa na watu waliopinga vitendo hivyo? Je, inawezekana kwamba viongozi wa juu wa ujasusi, wakiwemo wakuu wa taasisi, hususani DGIS waliwahi kutoa ushauri wa kupinga au kuonya dhidi ya matumizi ya nguvu kupita kiasi na mauaji raia wasio na hatia?


Zingatia kwamba Taasisi si kitu kimoja kisichobadilika; ndani yake kunaweza kuwepo utiifu na pia upinzani, udhaifu na pia uadilifu.

Ripoti inayojadiliwa inaruka hatua muhimu kutoka madai kwenda hitimisho la jumla, tena Inategemea maneno kama “madai ya uhusiano,” “taarifa zilizovuja,” na “tuhuma za uhusika,” lakini bado inadai hatua kali zaidi ya kisheria kimataifa. Kuruka huku kunadhoofisha hoja yenyewe.


Aidha, kuunganisha masuala tofauti kama vurugu za uchaguzi, mgogoro wa ardhi wa Wamaasai, na madai ya matukio ya kuvuka mipaka katika shtaka moja dhidi ya TISS kunachanganya badala ya kufafanua uwajibikaji. Kila suala linahitaji kuchunguzwa kivyake kwa umakini na ushahidi wake.


Pia kuna athari pana zaidi. Kuitangaza Idara ya Usalama wa Taifa, ambayo ni taasisi ya kitaifa ya ujasusi kuwa kundi la kigaidi kuna madhara makubwa ya kidiplomasia na kisheria. Hii si lebo ya kutumia kwa hasira au shinikizo la kisiasa; ni hatua inayohitaji ushahidi usio na shaka na viwango vya juu vya kisheria kimataifa.


Maelezo haya si kwamba yanapunguza maumivu ya waathirika au umuhimu wa haki. Ni ukweli usiopingika kuwa maelfu ya raia waliuawa au kujeruhiwa isivyo halali, hivyo yafaa wahusika wawajibishwe kikamilifu. Heshima ya Tanzania inategemea uwazi, uhuru wa mahakama, na uwajibikaji wa kweli katika kutoa haki. Hata hivyo, haki haiwezi kujengwa juu ya hisia au mawazo ya jumla bila ushahidi. Kanuni ile ile inayotukataza kuwachukulia wanachama wote wa CHADEMA kama wasaliti inapaswa pia kutuzuia kuwachukulia maafisa wote wa TISS kama wahusika wa uhalifu au magaidi.


Kwa hapa tulipofika Tanzania inahitaji ukweli wenye nidhamu. inayoweza kutofautisha kati ya mtu na taasisi, kati ya tuhuma na ushahidi, na kati ya hasira, hisia, na haki. Hapo ndipo taifa linaweza kusonga mbele kwa uadilifu na umoja.


Uwe na Amani

 
 
 

Comments


bottom of page