top of page

Tanzania Kwenye Kashfa ya Silaha Marekani

Updated: 1 day ago

Na Godwin Chilewa




Tanzania imeingia kwenye kashfa nyingine kubwa kufuatia kuhusishwa kwenye kesi ya usafirishaji haramu wa silaha inayosikilizwa katika Mahakama ya Shirikisho la Marekani, Eastern District of Virginia, moja ya mahakama zinazoshughulikia kesi nyeti za usalama wa taifa na uhalifu wa kimataifa.


Katika kesi hiyo, idara ya sheria ya Marekani (U.S. Department of Justice) imemshitaki raia wa Tanzania, Subiro Osmund Mwapinga, pamoja na washirika wake wa kimataifa, kwa tuhuma za kupanga kusambaza silaha za kivita kwa cartel ya Mexico, Jalisco New Generation Cartel. Silaha hizo ni machine guns, rocket launchers, na vifaa vya kivita vinavyoweza kuleta maafa makubwa.


Jambo linalofanya kesi hii kuwa mtego kwa Tanzania ni mbinu iliyodaiwa kutumiwa na watuhumiwa hao ambapo nyaraka za uongo (End-User Certificates) zinazoonyesha Tanzania kama mnunuzi halali wa silaha hizo. Zingatia hapa kwamba jina la taifa linaingia si kama mshtakiwa, bali kama mhusika wa mazingira ya tuhuma husika.


Kwa ujumla, kesi hii haiko kwenye kiwango cha uhalifu wa kawaida. Inagusa sheria nzito za Marekani zenye athari za kimataifa ikiwa pamoja na Arms Export Control Act (AECA)  sheria inayodhibiti usafirishaji wa silaha za Marekani nje ya nchi ambapo ukiukaji wake unaweza kusababisha hukumu ya vifungo virefu na vikwazo vya kimataifa.


Pia inahusisha International Traffic in Arms Regulations (ITAR)  Kanuni zinazosimamia nani anaruhusiwa kununua na kutumia silaha za Marekani. Aidha 18 U.S.C. § 371 (Conspiracy) inayohusu njama ya kufanya uhalifu dhidi ya Marekani, na pia Sheria za kupambana na ugaidi na makundi ya kihalifu ya kimataifa, hasa pale silaha zinapohusishwa na makundi kama cartel. Kwa maneno mengine, hii si kesi ya “biashara haramu” tu bali ni kesi inayoweza kutafsiriwa kama tishio kwa usalama wa kimataifa.


Kwa sasa serikali ya Tanzania haipo kizimbani. Lakini hilo haiko hatarini. Katika diplomasia, kuna kitu kinaitwa “association liability in perception” yaani “dhima ya taswira” jambo linalogusa taifa moja kwa moja. Aidha kesi hii inaibua maswali mengi kimataifa yanayohoji kama mifumo ya Tanzania ya kutoa vibali vya silaha ni salama? Nani anahakikisha uhalali wa End-User Certificates? Na inawezekanaje nchi itajwe mara kwa mara katika mpango wa uhalifu wa kimataifa bila udhaifu wowote wa ndani? Hapa ndipo serikali inapopaswa kutoa maelezo kwani kimya chake katika mazingira haya kinaweza kutafsiriwa kama kukwepa uwajibikaji.


Historia inatoa onyo wazi kwamba jumuia ya kimataifa huwa haifumbii macho tuhuma za aina hii. Iran imekuwa chini ya vikwazo vikubwa vya Marekani kwa miongo kadhaa kufuatia kesi na vikwazo vilivyotokana na ukiukwaji wa sheria za silaha (AECA na ITAR), Matokeo yake ni kutengwa kiuchumi na kidiplomasia.


Nayo Korea ya Kaskazini imekumbwa na mabalaa mengi kwa sababu ya tuhuma kadhaa za usafirishaji haramu wa silaha kupitia nyaraka za uongo na mitandao ya siri. Matokeo: vikwazo vya United Nations na kutengwa kabisa kimataifa.


Katika tukio lingine Mtandao wa nyuklia uliogunduliwa (Pakistan (A.Q. Khan Network) ulisababishia Pakistan presha kubwa ya kimataifa na kupoteza imani kwa washirika wake, licha ya serikali kudai haikuhusika moja kwa moja.


Nako nchini Mexico kuenea kwa cartel kama Jalisco New Generation Cartel kumeifanya Mexico kuwa chini ya shinikizo la kimataifa kuhusu udhibiti wa silaha na usalama wa ndani.


Mifano hii inaonyesha jambo moja muhimu: mara tu jina la nchi linapoingia kwenye mzunguko wa uhalifu wa kimataifa, athari zake hazibaki kwenye mahakama bali zinaingia kwenye uchumi, diplomasia, na siasa. Kwahiyo kama jumuiya ya kimataifa itaamua kuchukulia suala hili kwa uzito wake wote, Tanzania inaweza kukumbana na vikwazo vya moja kwa moja au vya siri. Marekani inaweza kuweka vikwazo kwa watu au taasisi, au hata kuanza kuzuia baadhi ya ushirikiano wa kifedha.


Pili, Tanzania inaweza kuwekwa kwenye orodha ya uangalizi wa Financial Action Task Force. Hii itafanya benki za kimataifa kuwa na tahadhari kubwa na Tanzania jambo linaloweza kusababisha kupungua kwa uwekezaji na kuongezeka kwa gharama za biashara.


Upo pia uwezekano wa kudorola kwa Mikataba ya Kijeshi na Usalama. Nchi washirika hususan Marekani, Jumuia ya Ulaya, Canada na nyinginezo zibaweza kusita kuuza silaha au kushirikiana kiusalama kwa hofu ya uvujaji wa silaha. Tanzania inaweza kuanza kuonekana kama “weak link” katika usalama wa kimataifa, jambo linaloweza kudumu kwa miaka mingi.


Kwa ujumla Tanzania iko kwenye mstari mwembamba kati ya ukweli na taswira. Ukweli unaweza kuwa kwamba serikali haijahusika. Lakini taswira inayojengwa kimataifa inaweza kusema vingine. Katika dunia ya leo, taswira hiyo ndiyo huamua nani anayewekeza nchini, nani anashirikiana nanyi, na nani anaiamini nchi. Kumbe swali la msingi si kama serikali ya Tanzania imehusika moja kwa moja, bali kama iko tayari kuthibitisha kwa vitendo kwamba haijahusika. Kwa sababu katika diplomasia ya kisasa, kutokujibu tuhuma ni sawa na kuziacha zikue. Na zikishakua, hazidhibitiwi tena na ukweli bali na imani ya dunia.


Uwe na amani.

 
 
 

Comments


bottom of page