Tundu Lisu Mhaini!? Hapana! CCM Hebu Jifunzeni Kuchutama…
- Rev. Godwin Chilewa
- Apr 11, 2025
- 3 min read

Uko msemo wa Kiswahili usemao “Ukivuliwa nguo chutama.” Msemo huu unaonesha hekima ya kutenda kwa akili baada ya kudharilishwa. Wanaoufafanua zaidi husema “kichaa akikupora taulo na kukimbia nalo, usimfukuze vinginevyo nyote mtaonekana vichaa. Kumbe iko hekima ya kutulia baada ya kudhalilishwa au kuaibishwa.
Ni jambo lisilopingika kwamba mwenyekiti wa CHADEMA mheshimiwa Tundu Antipas Lisu amekuwa akikivua nguo chama cha mapinduzi na serikali yake. Tundu lisu amekuwa akiyasema hadharani makosa na udhaifu wa viongozi wa serikali ya CCM na kuwataka wananchi kususia uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge ili kushinikiza mabadiliko ya sheria ya uongozi. “No Reform no election “ ndiyo kauli mbiu ambayo amekuwa akiitumia. Ni katika viguvugu hili la kuhubiri haki, kupigania demokrasia na kudai mabadiliko ndipo Tundulisu alipojikuta akiingia matatani.
Hata hivyo, Kitendo cha Jeshi la Polisi kumkamata Mwanasiasa huyu na kisha kumfungulia kesi ya uhaini kumefanya watu wa dunia nzima kujiuliza maswali mengi. Wapo wanaojiuliza kama uamuzi wa jeshi la polisi umezingatia hatima na muelekeo wa uhuru na demokrasia nchini. Wengine wanajiuliza kama hatua ya Polisi ni njama za kuisaidia CCM kushinda uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge (2025) na wengine wanajiuliza kama hivi sasa ni salama kuishi Tanzania kama wewe si mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi? Mimi najiuliza kama Watanzania tumerogwa au tumelaaniwa?
Ni ukweli usiopingika kuwa vyama vya upinzani ni muhimu kwa ustawi wa demokrasia ya Taifa letu . Kazi ya vyama hivi ni kuikosoa serikali, kuionya na kuishinikiza kujenga jamii ya haki, uhuru na yenye kuheshimu misingi ya utawala wa sheria. Katika kutekeleza wajibu huu viongozi wa vyama vya upinzani hawapaswi kusifia wala kujikombakomba kwa serikali au chama tawala. Wanapaswa kuongea kwa ukali, kukemea, kushawishi wananchi kuwaunga mkono na hata kutishia kuitisha maandamano kwa mujibu wa sheria. Naam, wapinzani wanapaswa kuonesha wana nguvu, na wanaweza kuitikisa serikali. Huo ni wajibu wao.
Kitendo cha kuwakamata viongozi hao kwa mambo wanayoyafanya kwa mujibu wa katiba, kwa tuhuma zisizoeleweka, au zinazotokana na kauli za kisiasa, ni tishio la wazi kwa uhuru wa kujieleza, uhuru wa kisiasa, na hatimaye kwa demokrasia yenyewe. Vyombo vya dola vinapotumika kukandamiza upinzani vinapora haki ya kikatiba ya wananchi kujieleza na kuonesha udhaifu wa kiutendaji, na tishio kwa demokrasia.
Mbaya zaidi ni kwamba dunia nzima inatushangaa kuona Vyombo vya dola, ambavyo kikatiba vinatakiwa kuwa huru na kutenda haki, vimegeuzwa kuwa vyombo vya mamlaka, vikitumika kuwanyanyasa wapinzani wa kisiasa kwa kisingizio cha kulinda amani na usalama. Matumizi mabaya ya sheria za uhaini, uchochezi na ugaidi dhidi ya wanasiasa na wanaharakati wa haki za binadamu ni dalili za wazi za serikali iliyo na hofu ya kushindwa katika uwanja wa hoja na siasa safi.
Tunapokaribia Uchaguzi Mkuu wa 2025, dalili hizi za uonevu wa kisiasa ni hatari kwa mustakabali wa Taifa letu. Demokrasia haiwezi kustawi mahali ambapo hofu imetawala, maoni yanazimwa kwa vitisho, na taasisi huru zimewekwa mfukoni mwa watawala.
Kumbe ni muhimu sana Jeshi la Polisi lionyeshe weledi na uzalendo wa kweli kwa kusimama upande wa haki, si upande wa mamlaka za kisiasa. Polisi ni chombo cha wananchi, si silaha ya serikali dhidi ya wapinzani wake. Ni muhimu pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ajiulize: kama Taifa linanufaika kwa vitendo hivi vya kubinya demokrasia, au linaelekea kusambaratika kwa mshikamano wa kitaifa?
Ili kuondokana na aibu hii ni muhimu Vyombo vya sheria vitumike kwa haki, si kwa hila. Sheria ya uhaini isiwe kisingizio cha kuminywa kwa haki ya kutoa maoni na kushiriki siasa. Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Asasi za kiraia zisimamie mchakato huru na wa haki kuelekea uchaguzi, bila hofu ya kuingiliwa na dola. Zaidi ya yote Wananchi waendelee kuwa macho na kusema kwa sauti kuhusu mustakabali wa Taifa lao. Kukaa kimya ni kuruhusu uonevu kuota mizizi.
Kwa kumalizia tunatoa wito kwa Serikali ya Tanzania kuachana na mkakati wa kuendesha nchi kwa hofu na mabavu. Njia hiyo haijawahi kuleta mshikamano wala maendeleo ya kweli. Badala yake, ijikite katika kuimarisha taasisi huru, kuheshimu haki za binadamu, na kujenga mazingira ambayo kila Mtanzania — awe chama tawala au upinzani — anahisi kulindwa na Taifa lake. Demokrasia si zawadi ya watawala, ni haki ya kila raia. Tusikubali iendelee kubakwa mbele ya macho yetu. Viongozi wa vyombo vyama vya upinzani dola muwe wa kwanza kulinda haki, demokrasia na amani ya Tanzania. Tusisahau kwamba kila kiongozi, kila askari na kila mtumishi ni mwananchi kwanza.
Rev. Godwin Chilewa






Comments