top of page

Maandamano ya 7 Julai: Serikali Isipange Kufanya Makosa ya 29 Oktoba 2025

Na Godwin Chilewa




Tarehe 7 Julai 2026 si siku ambayo inaweza kuamua mwelekeo wa taifa kwa miaka mingi ijayo. Vijana hasa kizazi cha Gen Z wamekusudia kuingia mitaani tena kuandamana kwa amani kudai haki zao za kikatiba. Watanzania wamefikia uamuzi huo licha ya kumbukumbu mbaya ya Oktoba 29 mwaka jana, siku iliyotikisa misingi ya taifa na kubadili historia ya nchi.


Kwa jinsi mambo yalivyo, na morali walionao vijana inaonekana kwamba uwepo wa maandamano hayo ni suala lisilo na mjadala. Hivyo swali pekee wanalojiuliza wengi ni kuwa serikali itachagua njia gani kuhakikisha amani na utulivu unakuwepo siku hiyo. Je, itakuwa tayari kujishusha ili kusikiliza raia wake, au itaamua kutumia kutumia mbinu zilezile za Oktoba mwaka jana?


Matukio ya Oktoba 29 hayakuwa ya kawaida kiusalama. Yalikuwa matukio mabaya, yaliyoacha athari nzito katika nafsi ya taifa. Matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya raia yalisababisha umwagaji damu wa kutisha, huku wengi wa waliouawa wakiwa vijana wadogo.


Nguvu hiyo badala ya kutuliza ghasia imechochea kuporomoka kwa imani ya wananchi kwa serikali, imejenga hofu iliyochanganyika na hasira ya kimya kimya, na mbaya zaidi imetia chachu kuibuka kwa kizazi kipya kisichoogopa tena mamlaka


Kwa ujumla badala ya kuzima sauti, tukio hilo limetengeneza kile kinachoweza kuitwa “kizazi cha upinzani” kizazi kinachohoji, kinachorekodi, na kinachokataa kunyamaza.


Swali kuu ambalo serikali haijawahi kujibu ni sababu hasa iliyofanya askari watumie risasi za moto kwa raia wasiokuwa na silaha. Nini hasa kilitokea? Kulikuwa na ulazima gani? Ni kweli kwamba kulikua na jaribio la mapinduzi? Kuna ushahidi gani?


Kutojibiwa kwa maswali hayo kunatoa taswira kwamba serikali inaogopa kusema ukweli, haijui makosa ya kimkakati iliyofanya, na au uongozi ulifanya maamuzi kwa hisia na mihemko badala ya taarifa sahihi za kiintelijensia.


Baadhi ya makosa ya kimkakati yanayoonekana wazi ni pamoja na kutafsiri tatizo la kisiasa kama tishio la kiusalama. Hili liliipa mamlaka ya juu sababu ya kutumia nguvu na mbinu za kijeshi badala ya hoja na kauli za kisiasa. Ukweli ni kwamba maandamano ni mgogoro wa kisiasa na si vita. Lakini kwa sababu serikali ilishaona mifano ya tawala zilizong’olewa madarakani kwa maandamano, basi maamuzi ya haraka na pengine ya kimhemko yakawa kutumia risasi badala ya hoja, na ikibidi mabomu ya machozi na maji ya washawasha. Hapa ndipo kosa la msingi lilipo. Tatizo halikutatuliwa, lilipanuliwa.


Kosa la pili lilikuwa kupuuza muktadha wa dunia ya leo. Katika hizi zama za simu janja na mitandao kila tukio linarekodiwa, kila habari inasambazwa, na kila hatua inachunguzwa kimataifa. Matumizi ya nguvu yawe makubwa au madogo hayabaki siri, hugeuka ushahidi.


Mfano mzuri ni tukio lililotokea Marekani ambapo polisi mmoja alimuua kwa kumkandamiza shingo mtu aitwae George Floyd huku wenzake wakiangalia. Tukio hilo lilipigiwa kelele dinia nzima na kusababisha maandamano makubwa nchini Marekani. Serikali ya nchi hiyo licha ya kuwafungulia mashitaka askari hao, ililazimika kuilipa fidia familia ya marehemu, na kutunga sheria na kanuni kadhaa za kuhakikisha tukio kama hilo halijirudii tena. Kifo cha mtu mmoja kilitingisha dunia sembuse mamia ya watu?


Kosa lingine la kimkakati ilikuwa kusahau “Backfire Effect” ya nguvu ya udhibiti. Matokeo yake nguvu hiyo imezalisha upinzani mkubwa zaidi, kiu ya kulipiza kisasi, na uungwaji mkono wa kambi na vyama vya upinzani. Chama tawala kinaonekana sehemu ya wauaji na hivyo kuzidi kupoteza umaarufu. Hili linaweza kusukuma muongezeko wa matumizi ya nguvu ya mara kwa mara ili kulinda maslahi ya chama tawala.


Kwa lugha rahisi badala ya kuwatisha vijana matukio ya Oktoba 29 yamewapa sababu ya kuendelea. Mauaji yameunganisha makundi yaliyokuwa tofauti na kuimarisha harakati za kijamii. Hii ni kanuni ya kihistoria, ukandamizaji mkali huzalisha upinzani mkubwa zaidi.


Mbaya zaidi ni kuwa makosa yaliyofanyika yamefunga mlango wa mazungumzo. Hii ni kanuni nyingine ya kiasili. Baada ya damu kumwagika Imani hupotea, mazungumzo huwa magumu, msimamo mkali huongezeka. Hata wale waliokuwa wakihimiza mazungumzo hurudi nyuma kwa hofu ya kuonekana wasaliti. Kwa hiyo, hatua hiyo haikumaliza mgogoro wala kuvunja upinzani, iliufanya kuwa mgumu zaidi.


Je, mauaji yangeweza kuepukwa? Serikali inasema la! Nguvu iliyotumika ilikuwa sawasawa na uhalifu wenyewe! Lakini ukweli ni kwamba hali ile haikuwa lazima ifikie hapo. Njia mbadala kadhaa zilikuwepo, na zingeweza kutumika kuepusha mauaji. Mazungumzo ya mapema kati ya serikali na waandaaji au vyama vikuu vya upinzani yangeweza kuepusha hali hiyo. Ieleweke hapa kwamba tatizo la msingi lilikuwa linajulikana na kila mtu.


Pili serikali ilikuwa na uwezo wa kuruhusu na kuratibu maandamano kwa amani, badala ya kuyazuia. Historia imetufundisha kwamba unapowazuia watu kusema basi hata mabubu huona wamenyang’anywa haki. Kama serikali ingeruhusu maandamano na kufanya utaratibu wa kuyadhibiti upo uwezekano mkubwa kwamba wengi wasingetoka.


Pamoja na hayo, serikali ilipaswa kufanya mawasiliano ya wazi, badala ya vitisho. Hili lilikuwa muhimu sana kwani maandamano ni haki ya kikatiba na si uhaini au uvunjaji wa sheria yoyote ile. Uzoefu unaonesha kwamba mawasiliano bora ni njia nzuri ya kutuliza hasira kuliko vitisho.


Mfano mzuri ni matukio ya uchaguzi mkuu wa 1995 ambapo Augustino Mrema alikuwa mgombea urais kwa tiketi ya NCCR MAGEUZI. Mikutano ya mgombea huyo ilikuwa ikileta taflani kwani kila baada ya hotuba wananchi walimmnyanyua na kumbeba juu juu bwana Mrema hali iliyowafanya polisi kulazimika kuwatawanya kwa kuwapiga risasi. Hatua hiyo ilizusha chuki kubwa kati ya polisi na wanachama wa NCCR MAGEUZI.


Mgogoro huo ulimalizika baada ya Mwalimu Nyerere kuhoji sababu za polisi kuwashambulia wananchi kwa mabomu kwa sababu tu ya kumbeba Mrema. “Kama kuna mtu anapenda kubebwa, na wako watu walio tayari kumbeba kuna tatizo gani? Hata kama wakienda wanapokezanamaili tatu kama jeneza?” Alihoji mwalimu Nyerere.


Maneno hayo yalikomesha kabisa tabia ya polisi kushambulia kwa mabomu ya machozi mikutano ya Augustino Mrema, na mgombea huyo pia akawa hataki tena kubebwa kwa kukwepa kejeli ya kufananishwa na maiti. Maneno machache yaliepusha maafa mengi.


Kumbe viongozi wetu wanapaswa kutumia vyema ujuzi wa mawasiluano huku wakitambua haki za kikatiba kama msingi wa utulivu. Kwa maneno mengine katika matukio ya Oktoba 29

kulikuwa na chaguo la amani lakini halikuchaguliwa. Hakuna ajuae kwanini.


Lipo pia suala la uhusika wa mataifa ya nje (mabeberu) katika kuhamasisha maandamano. Serikali ya Tanzania imekuwa ikisema mara kwa mara kuwa maandamano ya Oktoba 29 na mengine yote ni njama za nje na ufadhili wa mabeberu wanaoionea gere nchi yetu. Hili linapingwa na Vijana wanaosema wanadai haki zao za msingi ikiwa pamoja na ajira, uhuru wa kuchagua viongozi, na kupinga ufisadi.


Ukweli ni kwamba hakuna harakati inayodumu bila sababu ya ndani. Hasira ya kijamii haiwezi kuundwa nje bila msingi wa ndani. Hivyo basi, hata kama kuna ushawishi wa nje bado chanzo kikuu ni mgogoro wa ndani ambao haujapatiwa suluhisho.


Isitoshe serikali imekuwa ikitoa madai hayo bila kutoa ushahidi wa wazi. Waziri mkuu mhe. Mwiguru Nchemba amekuwa akisema “Watu wamelipwa mamilioni” bila kutaja watu au mataifa waliolipa fedha hizo, kiasi cha fedha kilicholipwa, wanufaika wa malipo hayo, benki zilizopitisha miamala na watu waliohusika kuzisambaza.


Kitendo cha kutotoa ushahidi huo miezi zaidi ya saba baada ya maandamano kinafanya wengi waone kauli hizo ni propaganda, na blaa blaa zisizopangiliwa kitaalam. Hili pia linakwenda sambamba na tuhuma za uwepo wa waandamanaji kutoka nje ya nchi. Mpaka sasa hakuna raia yeyote wa kigeni aliyefikishwa mahakamani kwa tuhuma hizo.


Je, serikali itatumia nguvu tena kwenye maandamano ya tarehe 7 Jualai? Hili ndilo swali la Jackpot! Hata hivyo jibu lake linaweza kuwa rahisi. Kwa hali ya kisiasa, kiuchumi, kidiplomasia na kijamii iliyopo sasa serikali makini HAIWEZI kuthubutu kumwaga damu kwa mara ya pili.


Kama serikali itachagua matumizi ya nguvu tena, matokeo yanaweza kuwa mabaya zaidi kuliko yale ya Oktoba 29. Hii ni kwa sababu tayari serikali ina mgogoro mkubwa kisheria (Kimataifa) na mauaji mapya yanaweza kuharakisha njia ya uwajibikaji kupitia International Criminal Court:


Hii ina maana ICC itaharakishauchunguzi wa uhalifu dhidi ya ubinadamu. Itataka uwajibikaji wa haraka wa watu binafsi, sio taasisi tu. Nchi itakuwa imejiingiza kwa nguvu kwenye vikwazo vya kimataifa. Kwa lugha nyingine mauaji hata ya watu wachache tu yatamuweka rais wa nchi kwenye kundi moja na madikteta wengibe.


Ndani ya nchi hali itakuwa tete zaidi. Hasira ya wananchi itaongezeka, sio kupungua. Upinzani utakuwa zaidi kiasi cha kuchochea uasi wa moja kwa moja au wa siri kwenye najeshi. Uharali wa serikali utadhoofika zaidi. Mgawanyiko wa kitaifa utaongezeka hasa kati ya Watanzania bara na Wazanzibari.


Kidiplomasia Tanzania itapoteza hadhi yake ya muda mrefu ya utulivu. Wawekezaji wataanza kuondoka kwa kasi. Shinikizo la kimataifa litaongezeka. Tanzania haitabaki kama ilivyo.


NJIA PEKEE YA KUEPUKA MGOGORO MKUBWA ni kufungua milango ya mazungumzo ya kitaifa. Kuruhusu uhuru wa kukusanyika kwa amani chini ya uangalizi na ulinzi wa vyombo vya dola. Vijana wasikilizwe hoja zao, watoe madukuduku yao. Wanachotaka ni kusikilizwa.


Pamoja na hilo serikali ioneshe uwajibikaji kwa matukio yaliyopita. Matukio ya Oktoba 29 yanapaswa kuifindisha serikali umuhimu wa kukisokiliza kizazi kipya badala ya kukikandamiza.


Nisisitize hapa kwamba Tanzania iko katika wakati nyeti sana. Inaweza kuchagua njia ya nguvu na kuingia katika mzunguko wa migogoro au inaweza kuchagua njia ya haki na kujenga utulivu wa kudumu


Kwa hali ilivyo, kizazi cha Gen Z hakitarudi nyuma. Na kila hatua itakayochukuliwa dhidi yao itaamua mustakabali wa taifa kwa sababu ukweli huu hauwezi kubadilishwa:


Taifa haliwezi kujenga amani kwa risasi.

Na historia haisamehi makosa yanayoweza kuepukwa.


Uwe na Amani

 
 
 

Comments


bottom of page