top of page

Waraka wa Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) Kumyima Usingizi Rais Samia Suluhu?

Updated: Aug 21, 2023

Hivi karibuni Baraza la maaskofu katoliki nchini Tanzania (TEC) lilitoa waraka maalum kuelezea kutoridhishwa kwake na makataba kati ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na falme za kiarabu (Dubai) kuhusu uwekezaji katika bandari za Tanzania. Waraka huo uliosainiwa na maaskofu 37 na kusambazwa kwenye makanisa ya kikatoliki, umechambua kwa kina vipengele vyenye utata katika mkataba huo na vinavyoelekea kuitia Tanzania kwenye matatizo makubwa kiuchumi, kiutawala na kijamii. TEC pia imeishauri serikali hatua za kuchukua ili kuondoa mgawanyiko katika taifa na kulinda rasilimali zetu.


Kufuatia waraka huo watu wengi wamekuwa wakijiuliza maswali kadhaa. Kwanza hawa TEC wana nguvu kiasi gani? Waraka wao una jipya gani? na je! unaweza kuitikisa serikali kiasi cha kukubali kufanya mabadiliko muhimu katika mkataba huo japo kwa kuondoa yale yanayolalamikiwa tu? Kujibu maswali haya inabidi tujiulize kama kweli TEC wanaweza kumnyima usingizi Rais Samia Suluhu Hassan japo kwa usiku mmoja, au kama rais huyo anaweza kuwadhibiti kirahisi tu.


Tuanze kwa kukumbushana kuwa baraza la maaskofu katoliki si chombo cha kwanza kutoa tamko la kupinga mkataba wa bandari. Viongozi mbalimbali wa kisiasa ikiwa pamoja na mwenyekiti wa CHADEMA Bw. Freeman Mbowe, makamu wake mhe. Tundu Antipasi Lisu, Dr. Wilbroad Slaa na wengine wengi walishatoa kauli zinazofanana na tamko la TEC. Nao viongozi wastaafu wanaoheshimika kama profesa Tibaijuka, mzee Joseph Butiku, na hata makamu mwenyekiti wa CCM Luteni Kanali Abraham kinana nao kwa namna tofauti wamethubutu kusimama hadharani kuelezea wasiwasi wao kuhusu mkataba huo na haja ya kuufanyia marekebisho.


Balozi, Dr. Wilbrod Slaa

Kubwa zaidi ni hili la wanasheria wakongwe nchini ikiwa pamoja na profesa Issa Shivji, Fatuma Karume, wakili Mwabukusi na wengine wengi ambao wameuchambua waraka huo kifungu kimoja baada ya kingine kubainisha udhaifu na hatari ya kuendelea na mkataba huo bila ya kuufanyia marekebisho. Wakili Mwabukusi yeye na wenzake walienda mbali zaidi hata kufungua kesi katika mahakama kuu ya Tanzania, Mbeya kujaribu kuizuia serikali kuendelea na mkataba huo jambo ambalo halikufanikiwa.


Nao wanaharakati wa mitandaoni akina Maria Sarungi, Mdude Nyangali na wengine wengi wamefanya kazi kubwa ya kupiga kelele na hata kuhamasisha maandamano ya wananchi kupinga mkataba huo. Harakati hizo zimeelekea kupigwa stop baada ya jeshi la polisi kuonya kuhusu watu wanaohamasisha mipango ya kuipindua serikali ya rais Samia, na kuwakamata Dr. Wilbroad Slaa, Mdude Nyangali na wakili Mwabukusi kwa tuhuma za uhaini japo baadae wakaachiliwa huru.


Hata kwa makundi na mashirika ya kidini, TEC si wa kwanza kutoa tamko. Wako maaskofu, wachungaji, mitume na manabii wa makanisa mbalimbali, na pia mashekhe na maulamaa wa kiislam walioeleza hadharani misimamo yao kuhusu mkataba huu bila woga. Kwa ujumla ilichofanya TEC si jambo jipya, bali marudio tu ya yale yaliyokwishafanywa na makundi mengine. Sasa kwanini waraka huu umkoseshe usingizi rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?


Ieleweke kwamba kanisa Katoliki Tanzania ni sehemu ya mtandao mzima wa kanisa katoliki duniani chini ya uongozi wa pontifex (Baba mtakatifu) mwenye makao yake nchini Vatican. Inakadiliwa kanisa hili lina waumini zaidi ya bilioni moja na ushee ulimwenguni, na hapa Tanzania zaidi ya waumini milioni 12 . Idadi ambayo ni karibu ya moja ya tano ya watanzania wote.


Tofauti na makanisa mengi ya kisasa (ya uamsho) ambayo hayana misingi imara ya mifumo ya uongozi na uchumi, kanisa katoliki limejengwa chini ya mwamba imara. Viongozi wa makanisa yote (mapadre) ni wasomi wa hali ya juu, waliohitimu masomo ya theolojia, filosofia, uungu, historia, siasa, sheria za kanisa, sayansi jamii na kadhalika. Hakuna padre wa kanisa hili anayepatikana kwa ubabaishaji, Kila anayepewa daraja hili takatifu huwa amepitia mchakato kamili, kufuzu masomo, na kuidhinishwa kupewa daraja takatifu la ukuhani.

Askofu Flavian Kassala Matindi

Maaskofu wa kanisa katoliki hawa ndiyo usiseme. Huteuliwa na pontifex (baba mtakatifu) mwenyewe toka kwenye orodha ndefu ya mapadre wasomi wenye PhD waliopendekezwa. Kwenye kanisa hili hakuna PhD za kupeana wala za heshima, Padre ni lazima aoneshe sifa zinazomstahilisha kupewa uaskofu ikiwa pamoja na uwezo mkubwa wa akili, uongozi, utii, ucha Mungu, na uwezo wa kuzungumza lugha za Biblia - kiebrania, kigiriki na pia kilatini.


Ufahamu na lugha ni muhimu sana kwani kila askofu wa kikatoliki hupewa nafasi ya kukukutana, kuzungumza na kufanya maombi ya kipekee (private) na baba mtakatifu mara moja katika kipindi cha miaka mitano kwenye Ad limina. Kwahiyo ni lazima askofu ajue kuzungumza lugha ya nyumbani (Vatican).


Kanisa katoliki huendeshwa kwa mfumo unaofanana na jeshi, hivyo amri ikitoka juu hakuna anayeweza kuipinga. Wenyewe husema "Roma locuta causa finita" Kwahiyo maaskofu wakiagiza, mapadre hufanya utekelezaji tu, kadhalika na waumini hivyo hivyo. Kanisa halina ile demokrasia ya makanisa ya uamsho. Viongozi na walei wote hujifunza utii kutoka juu. Hili ni jambo muhimu sana la kutafakari hasa yanapotokea malumbano kati ya serikali na kanisa katoliki. Serikali inapaswa kujiuliza, waumini wanaweza kuchagua kumtii nani?


Kwa kuwa kanisa katoliki Tanzania ni sehemu ya kanisa katoliki duniani viongozi wake (maaskofu) hujiamini na hawatishiki kirahisi kwa sababu ya nguvu iliyo nyuma yao. Makadinali hao ndiyo zaidi, maana wao huitwa "princes of church" hawagusiki kirahisi. Kumkamata na kumuweka ndani kiongozi wa kanisa katoliki kunaweza kusababisha mlipuko mkubwa wa kidiplomasia duniani. Zingatia pontifex ni mmoja wa viongozi wenye nguvu na ushawishi mkubwa duniani.

Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Bugando

Nchini Tanzania kanisa Katoliki lina historia ya kipekee kuanzia kipindi cha kudai uhuru. Wasomi wengi wa kipindi cha kina mwalimu Nyerere walitokana na shule za kanisa hilo. Kanisa katoliki lilijenga shule na hospitali katika maeneo mengi yaliyowasaidia watu wa dini zote kupata elimu ingawa wazazi wengine (kwa kutojua) waliwazuia watoto wao kwenda shule kwa hofu ya kubadilishwa dini. Ni msingi huo uliotupa wasomi wa mwanzo waliojenga serikali ya Tanganyika. Hili baadae lilileta malalamiko yasiyo na tija kuwa serikali ya Tanzania ilikuwa ya kikatoliki hususan kwa kuwa mwalimu Nyerere alikuwa mkatoliki.


Kanisa katoliki lina mchango mkubwa mno katika ustawi wa taifa la Tanzania. Leo hii kanisa hili linamiliki hospitali kubwa za rufaa ikiwa pamoja na ile ya Bugando Mwanza, vituo vya afya na zahanati lukuki zilizotapakaa nchi nzima. Pia inamiliki maelfu ya shule za chekechea, msingi, na sekondari zinazofanya vizuri zaidi kitaifa; na vyuo vikuu kadhaa vinavyoheshimika kimataifa. Hii ni taasisi iliyojijenga vyema na yenye misingi imara.


Kama mpaka hapo hakuna jambo linaloweza kumfanya mheshimiwa rais asipate usingizi kwa waraka wa TEC basi kuna jambo haliko sawa. Viongozi wa waumini zaidi ya milioni 12 wanapowaambia waumini wao mkataba huu hauko sawa.... tuukatae si jambo la kupuuza hata kidogo. Hawa ni watu wanaoweza kuwaambia waumini wao "Msimchague huyu" na wakasikilizwa bila maswali.


Zaidi ya yote hoja walizotoa kwenye waraka huo si za kitoto. Ni hoja za nguvu, zilizoandaliwa kwa umakini mkubwa, na watu wenye elimu na maono ya hali ya juu. Watu wa Mungu wanaoongozwa kwa uvuvio wa roho mtakatifu. Yamkini mtu yeyote ambaye bado anaamini mkataba wa bandari ni mzuri na wa manufaa kwa watanzania kama akiusoma waraka huu hawezi kubaki kama alivyo. Atajitambua na kuelewa kiini cha yale yanayopigiwa kelele na wengi. Kwa ujumla waraka huu umetia muhuri yale yaliyokwisha elezwa kwa machozi na wengi waliotangulia. Kwa waumini, hii ni sauti ya Mungu anayenena kwa vinywa vya manabii wake.


Ni matumaini yangu mheshimiwa Rais atakuwa tayari kuyafanyia kazi maoni ya TEC na wengine wote waliojitokeza kuhoji mkataba wa bandari. Kufanya hivyo kutasaidia kurejesha umoja ulioanza kupata nyufa, lakini pia kujenga matumaini mapya ya wananchi kwa rais wao. Vinginevyo tutatarajia matamko mengine mengi kabla ya uchaguzi toka kwa viongozi hawa. Na kama wasemavyo wenyewe "Roma locuta causa finita"


Ustawi wa Tanzania - Jukumu letu sote.

Rev. Godwin Chilewa

Uwe na amani



Comments


bottom of page