Watanzania Kubadilishwa Vinasaba?
- Rev. Godwin Chilewa
- Mar 18, 2024
- 10 min read
Updated: Mar 20, 2024

Hivi karibuni kulizuka gumzo kubwa kuhusu usalama wa vyakula vinavyoingizwa nchini kutoka nje. Watanzania wengi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii wamehoji uwajibikaji wa serikali na hasa shirika la viwango nchini (TBS) katika kupima na kuhakikisha watanzania hawalishwi sumu au vitu vinavyoweza kuwaletea madhara baadae. Haya yametokea baada ya kusambaa kwa taarifa za kuingizwa kwa msaada mkubwa wa mchele na mafuta ya kula kutoka nchini Marekani. Msaada unaolenga kufaidisha shule zaidi ya 350 chini ya mapango wa "Pamoja Tuwalishe" ("Together Let's Feed Them").
Binafsi nimeshangazwa mno kwa kelele nyingi zilizopigwa kuhusiana na suala hilo. Si kwa sababu nina hakika chakula kilichoingizwa ni salama la! Bali kwa kuwa yako mambo mengine mazito na ya kutisha zaidi ambayo watanzania walipaswa kuyapigia kelele kwa nguvu kuliko chakula hicho. Yamkini ubaguzi wa kisiasa na uchawa uliokithiri umewafanya wengi kufuatilia mambo wanayoona yanaweza kuwapa mtaji wa kisiasa au kupata teuzi na si vinginevyo. Ndiyo maana jambo jema linaweza kupigiwa kelele na la hovyo likapigiwa makofi kwa kuwa limefanywa na mtu anayeungwa mkono kisiasa tu. Hovyo kabisa!
Ninachoshukuru ni kuwa kelele hizo zimenihamasisha na mie kuchungulia miradi mbalimbali yenye ufadhili wa kigeni nchini mwetu. Uchunguzi nilioufanya kwa muda mfupi tu umeniwezesha kuona mengi ya kutisha ambayo sina hakika kama wananchi wanayajua lakini wameamua kuyakalia kimya tu, na pia kama mheshimiwa Rais, mama Samia Suluhu Hassan na serikali yake wameruhusu mambo hayo yaendelee kufanyika bila maswali. Yapo mengi lakini leo ngoja nianze na haya mawili: Mradi wa uzalishaji mbu wa vinasaba, na mradi wa uzalishaji mahindi ya GMO nchini.
MRADI/UTAFITI WA KUZALISHA MBU WA VINASABA (KI BAIOLOJIA) TANZANIA
Mradi huu unaojulikana kama "Transmission Zero" ulianzishwa na mpango wa utafiti wa ugonjwa wa malaria duniani (Global Malaria Research Programe) kwa lengo la kupambana na ugonjwa huo kusini mwa jangwa la sahara. Nchini Tanzania mradi huu unasimamiwa na Chuo cha Afya Ifakara (Ifakara Health Institute) kupitia idara yake ya afya ya mazingira na sayansi ya ikolojia (Environmental Health and Ecological Sciences Department) inayoongozwa na Dr. Lina Finda. Viongozi wengine ni Dr. Maganga Sambo na Dr. Fredros Okumu.
Kinachofanyika katika mradi huu ni kutengeneza mbu wa kibaiolojia kwa kubadilisha vinasaba vyao toka hali ya sasa kwenda hali mpya kwa kufanya gene drive. Kwa kawaida vinasaba vya kiumbe hai huwa na asilimia 50% ya kuweza kurithiwa na watoto, lakini kwa kufanya gene drive uwezekano huo hupanda kufikia 99% Hii ina maana wajukuu wa mbu watakaozalishwa chini ya mpango huu watakuwa na vinasaba vipya kabisa.
Pengine utajiuliza kwa nini wazalishwe mbu wenye vinasaba vipya ? Kwa mujibu wa taarifa za waandaaji wa mpango huu mbu wapya watakaozalishwa (transgenic mosquito) watakuwa na uwezo wa kuwala au kuwaua mbu aina ya anopheles wanaoambukiza ugonjwa wa malaria. Kwa hiyo baada ya miezi au miaka kadhaa ya kusambazwa kwa transgenic mosquito mbu wanaoishi sasa (Anopheles, Qulex na Edes watakuwa wameangamizwa na badala yake mbu wapya - transgenic mosquito watakuwa wamechukua nafasi yao.
Ukiangalia kwa haraka haraka utaona mradi huu kama mzuri na wenye manufaa makubwa kwani utamaliza ugonjwa wa malaria unaoua mamilioni ya watu kila mwaka. Hata hivyo yapo maswali ya msingi ambayo serikali yetu inapaswa kujiuliza kuhusiana na mradi huu. Hapa nimeorodhesha machache tu.

(i) Mradi Huu ni Kificho kwa Mradi Mwingine?
Mojawapo ya sifa kubwa ya nchi zilizoendelea hasa Marekani, Uingereza na China ni kutumia hadaa na ulaghai wa kijasusi katika kufanikisha mipango yao. Si ajabu katika kutafuta makoloni wazungu hao walitumia wamisionari na wavumbuzi kuwahadaa waafrika. Sina hakika kama tabia na mtazamo wa wazungu hao umebadilika. Ndiyo maana inapaswa tujiulize mara mbili mbili kama lengo la mradi huu ni kupambana na malaria kweli au kuna lingine? Je serikali yetu ina uwezo na utaalam wa kubaini mbinu, hujuma au uharibifu wowote (kama upo) au unaoweza kutengenezwa kupitia mradi huo?
(ii) Nchi Zilizoingizwa Kwenye Mradi Huu
Kwa mujibu wa taarifa za Active Gene Drive Project in Africa kundi la kwanza liitwalo Target Malaria linahusisha nchi za Burkina Farso, Uganda, Ghana na Cape Verde ambazo zinafanya majaribio ya suppression drives. Kundi la pili liitwalo Transmission Zero lina nchi moja tu ambayo ni Tanzania, inayofanya majaribio ya Integral Gene Drive, Kundi la tatu liitwalo UMCI Stop Malaria Program linahusisha visiwa vya Sao Tome and Principe ambalo linafanya majaribio ya Replacement Drive. Kundi la mwisho linahusisha nchi ya Djibout lakini lenyewe linashughulika na Anopheles Stephensi ambayo si gene drives.
Swali la msingi wanalojiuliza wataalam ni hili: Kwanini nchi ya Cape Verde imeingizwa kwenye mpango huu wakati nchi hiyo ilishatokomeza ugonjwa wa malaria? Kama kweli lengo ni kuwamaliza mbu wa malaria tu kwanini nchi isiyo na ugonjwa huo ipelekewe transgenic mosquito? Ukweli huu umewatia wasiwasi baadhi ya wataalam kwamba mradi huu ni mojawapo ya mipango inayofanywa kujaribu kupandikiza vinasaba vipya kwa waafrika kwa malengo yasiyofahamika, au kutengeneza ugonjwa utakaoua mamilioni ya watu baadae (extermination vector).
Wanaotetea mradi huu wanasema haya ni majaribio ya kawaida na kwamba sehemu ya kwanza ya majaribio kama hayo ilifanyika nchini Marekani ambapo mbu hao walisambazwa kwenye majimbo (states) ishirini. Swali wanalojiuliza wataalam ni kama mbu waliosambazwa marekani ndio haohao watakaosambazwa Tanzania au hawa wana malengo mengine? Kumbuka mmoja wa wafadhili wakubwa wa mradi huu ni Bill and Melinda Gates Foundation. Kama hujui Bill Gates anatuhumiwa (bila kuwepo uthibitisho) kwa kuipigia debe sera ya kupunguza watu duniani (depopulation).
(ii) . Udhibiti wa Mbu (transgenic mosquito) Watakaoachiliwa
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, Tanzania hivi sasa iko katika hatua ya pili ya majaribio ya kimaabara ambapo mbu waliotengenezwa wanahifadhiwa kwenye matundu makubwa kupima matokeo ya awali. Baadae katika hatua ya tatu (phase III) mbu hao wataachiliwa huru kwa kiasi fulani, kabla ya kuachiliwa kwa wingi kwenye hatua ya nne (phase iv) ili wafanye kazi yao. Hata hivyo si waendeshaji wa mradi huo (Ifakara Health Institute) wala serikali ya Tanzania iliyochukua hatua zotote kwa :
(a) Kufanya upembuzi yakinifu kabla ya kuendelea na hatua ya sasa. Taarifa zilizoandikwa na gazeti moja la Marekani mwaka 2023 zilisema majaribio yaliyofanyika awali yameonesha gene drive iliyofanyika ilileta haikuleta matokeo yaliyotarajiwa na au transgenic mosquito wanaotengenezwa hawatakuwa na uwezo wa kudhibiti vijidudu vya malaria (parasites) kama inavyodaiwa. Mpaka sasa watafiti wa mradi huo wameshindwa kutoa maelezo ya namna jeni zinazotengenezwa zitakavyoweka shinikizo maalum kwa vimelea vya malaria kubadilika na kubadilisha uwezekano wake wa kusababisha magonjwa. Aidha wameshindwa kueleza jinsi wanavyoweza kujua ikiwa upinzani dhidi ya jeni hizo unafanyika
(b) Kutoa taarifa ya maeneo yaliyochaguliwa kwa ajili ya kusambaza mbu hao, na Kuthibitisha kwamba transgenic mosquito watakapoachiliwa hawatakua chanzo cha ugonjwa mpya utokanao na vinasaba vipya.
(c) Kuwaasa wananchi mahali pa kutoa taarifa kama ikitokea wamepata ugonjwa usiojulikana baada ya kuumwa na mbu hao.
(d) kuandaa matibabu ya dharula au uangalizi maalum kwa wananchi watakaopata ugonjwa usiojulikana baada ya kuumwa na mbu hao.
(e)Utaratibu wa kuwadhibiti mbu hao baada ya kuwaachia huru na kusambaa maeneo mengine endapo watabainika kusambaza ugonjwa mpya.
(f) Kujua kama kweli mbu hao wanafanya kazi wanayotakiwa (kuua mbu wa malaria tu) na si kudhuru mifugo au viumbe hai vingine.
(g).Kuhakikisha transgenic mosquito hawabadiliki kuwa viumbe vingine visivyotarajiwa hata baada ya miaka mingi na kama hawatatumika kama silaha za maangamizi (extermination vector)
(h) Uhakika wa kuwamaliza mbu hao mara tu watakapomaliza kuwaangamiza wenzao ili wasidhuru viumbe vingine kwa sababu ya ukosefu wa chakula.
Yako maswali mengine mengi ya kitaalam ambayo hayajatolewa majibu na au majibu yake yanaelekea kuwa ya ubabaishaji. Ni muhimu sana serikali ya Tanzania ichunguze mradi huu kwa undani na ikibidi hata kutumia wataalam wengine wa nje (3rd party) wenye utaalam na vifaa vinavyoweza kubaini ajenda zilizo nyuma ya pazia.

2. MRADI WA MAHINDI YANAYOHIMILI UKAME (Water Efficient Maize for Africa - WEMA)
Mradi huu ulianzishwa mwaka 2008 lakini ulipata nguvu zaidi kati ya mwaka 2013 - 2017. Mradi unaongozwa na Christopher Ochieng Ojiewo, Paswel Marenya na Pieter Rutsaert wenye ofisi yao Icraft House, United Nations Avenue, Gigiri Village Market 00621 Nairobi Kenya. Wafadhili wakubwa ni Bill and Melinda Gates Foundation, Howard and Buffet Foundation na Agency for International Development.
Lengo la wazi la mradi huu ni kuzisaidia nchi maskini kuzalisha mahindi zaidi ili kujitosheleza kwa chakula. Tofauti na miradi mingine ya kilimo cha kawaida mradi huu unahimiza matumizi ya njia za kitaalam (Bleeding - Biotechnology) kuzalisha mahindi ya GMO. Wataalam wa WEMA wanadai mkulima anayetumia mbegu na utaalam huu hupata ongezeko la 24% hadi 35% zaidi kulinganisha na mkulima wa kawaida.

Kufikia wakati huu WEMA inaendelea kufanya utafiti wa mbegu bora zinazohimili ukame, kufanya makongamano ya kutoa elimu na kuhimiza matumizi ya mbegu za kisasa pamoja na viwatilifu vinavyokwenda sambamba.
WEMA pia inafanya jitihada za kuwawezesha wakulima wadogo kupata masoko ya mazao yao, kujipanua kwa kuongeza uzalishaji ki hekali, kushirikiana na asasi nyingine kuwawezesha wakulima kwa kuwapa mtaji. Ki msingi mradi huu unaendeshwa sambamba na ule wa "Pamoja Tuwalishe" uliotoa msaada mkubwa wa mchele na mafuta ya kula kwa mashule zaidi ya 350 nchini.
Ukiangalia kwa haraka haraka utasema miradi hii nayo ni mizuri na yenye tija kubwa kwa watanzania, na waafrika kwa ujumla. Hata hivyo si kweli hata kidogo. Miradi hii imelenga kuzidumbukiza nchi za kiafrika kwenye utegemezi wa mbegu na viwatilifu kutoka nje, na pia kutuingiza kwenye ulaji wa vyakula vilivyotengenezwa kwa Genetic Modified Organisms (GMO) ambavyo vimethibitika kuweza kupandikizwa vimelea vya kuharibu vinasaba kwa kutumia NRA effect technology.
(a) Kuwa Tegemezi kwa Mbegu na Viwatilifu
Aina ya mazao ya chakula na biashara yanayozalishwa nchini hivi sasa yanawezesha uendelevu wa uzalishaji. Mkulima akivuna mahindi au mpunga wake anaweza kutenga sehemu ya mavuno hayo kwa ajili ya mbegu atakazozitumia msimu wa kilimo unaofuata. Kwa hiyo hivi sasa nchi haina sababu ya kuagiza mbegu kutoka nje. Lakini mazao yanayopigiwa debe na wafadhili hawa kwa kuwa ni GMO hayamuwezeshi mkulima kujitunzia mbegu zake kwahiyo analazimika kununua toka kwa makampuni yanayozalisha mbegu kila msimu kilimo. Hii haijalishi kama mkulima huyo anao mpunga au mahindi ya kutosha ghalani mwake. Hili ni jambo la hatari sana kwani linampa nguvu mzalisha mbegu kumtawala mkulima.
Ki msingi kilimo cha mazao ya GMO ndicho kilichowezesha nchi zilizoendelea kama Marekani na Uingereza kudhibiti uzalishaji na matumizi ya vyakula nchini mwao. Mtu anayeishi Marekani akitaka kulima bustani analazimika kununua mbegu, viwatilifu, na hata udongo wa kupandia mimea anayoitaka toka kwa wauzaji wakubwa. Hili limewafanya wananchi wa kawaida kuwa wanunuzi wa vyakula na hata mboga ambazo wangeweza kujipandia wenyewe huku wakulima matajiri (makabaila) wakiendelea kuwa na soko la uhakika wa mazao yao. Utaratibu huu umewafanya raia kuishi kwa kutegemea mshahara.
(b) Kula Vyakula Vilivyobadilishwa.
Kwa kuwa mazao yanayozalishwa kwa mbegu bandia (GMO) huwa yamekufa (ndiyo maana hayaoti) ubora wa lishe yake huwa duni kulinganisha na mazao yaliyozalishwa kwa mbegu hai. Hili ndilo linalopelekea wataalam wa vyakula wa nchi zilizoendelea kuongeza virutubisho kwenye mazao yao ili kukidhi haja ya mahitaji ya mwili. Kwa hiyo endapo serikali ya Tanzania itaunga mkono jitihada za matumizi ya mbegu za GMO italazimika kujiandaa kununua virutubisho vya kuongeza katika vyakula hivyo ili viweze kufaa. Kufanya hivyo kunaweza kufungua mlango mkubwa zaidi wa kulishwa madawa mengine yenye madhara kimwili na kiakili kwa jina la virutubisho.
Mbaya zaidi ni kuwa vyakula vya GMO vinaweza kutumika kama silaha za maangamizi. Wakati wa uzalishaji wake wataalam wanaweza kutumia NRA effect technology kupandikiza vimelea vya sumu au vinavyoweza kubadilisha vinasaba vya mlaji kwa namna wanayotaka. Hii ina maana wanaweza kupandikiza vimelea vya kusababisha kansa, kupunguza nguvu za kiume, kuharibu mimba, au kuchochea ushoga. Kimsingi NRA effect technology inaweza kufanikisha chochote wanachokudia kufanya wataalam hao.
Naomba nieleweke hapa kwamba mpaka sasa hakuna uthibitisho wowote ule kwamba WEMA, Pamoja Tuwalishe au mradi mwingine wa wafadhili umethibitika au umeonesha haja ya kuua watanzania. Lakini hekima imetufundisha, kwamba ukimuona jirani yako ananoa panga ni vyema ujiulize anataka kufanya nini. Je! Anataka kufyeka msitu, kukata kuni, au kukushambulia? Kama hicho kipindi ni cha kilimo unaweza usiwe na wasiwasi sana, lakini kama ni kipindi cha vita utapaswa ujiulize mara mbili na ikibidi ujiandae kwa mapambano. Hapo ndipo ninapojiuliza kama serikali yetu inafuatilia kwa undani miradi hii ya vyakula vya GMO? Ina hakika na malengo yake?
Kumbe ni vyema viongozi wetu wajifunze kutokana na historia yetu. Miaka ya mwishoni mwa 1970 serikali yetu ilipewa maonyo kadhaa kuhusu ubaya wa matumizi ya mbolea ya chumvichumvi mashambani. Maneno hayo japokua yalikuwa na ukweli yalipingwa kwa kuonekanna ni propaganda za mabeberu ukizingatia wakati huo Tanzania ilikuwa na kiwanda chake cha mbolea mjini Tanga. Leo hii ardhi ya mikoa iliyotumia mbolea hiyo kwa wingi (kama Ruvuma) imeharibika vibaya kiasi cha kushindwa kuotesha chochote bila mbolea hiyo ambayo pia imebainika si salama kwa afya. Tuliambiwa tutumie samadi tukapuuza.
Hivi sasa nchi zilizoendelea hususan Marekani zinafanya kampeni kubwa za kuwahimiza wananchi wake kula vyakula vilivyozalishwa bila mbolea za kemikali wala madawa ya kuua wadudu (Organic Food) kwa afya na usalama wa miili yao. Vyakula hivyo huuzwa kwa bei ya juu na ndivyo vyenye soko kubwa zaidi nchini humo. Itakuwa ajabu mno kwa Tanzania kujiingiza kwenye kilimo kinachotupeleka kwenye uharibifu wakati tunayo ardhi inayofaa kuzalisha chakula bora na kukiuza ughaibuni.
3. HITIMISHO
Kwa miaka mingi watanzania tumetumika kama panya wa majaribio (guinea pigs) kwa manufaa ya makampuni ya vyakula na madawa ya nchi za magharibi. Miaka ya mwishoni mwa 1970 kina mama wengi walipata matatizo ya kiafya na hata kupoteza maisha yao kwa kutumia madawa ya uzazi wa majira yaliyokuwa yakisambazwa chini ya mradi wa Uzazi na Malezi bora Tanzania (UMATI). Mpaka sasa hakuna kampuni wala nchi yoyote iliyoonesha kuwajibika na hakuna mhanga hata mmoja aliyelipwa fidia kwa madhara hayo,. Mbaya zaidi hakuna dalili yoyote inayoonesha kama serikali yetu imejifunza kitu kutokana na mradi huo maarufu.
Wakati sisi tunachekeana hivi karibuni serikali ya Marekani imeridhia kuwalipa fidia watu waliopata madhara (kuugua kansa) kufuatia majaribio ya bomu la Atomic (Manhattan Project Trinity test) yaliyofanyika New Mexico tarehe 16 Julai 1945. Vizazi vya wahanga hao wameahidiwa kulipwa mamilioni ya dola kwa sababu serikali imekiri kwamba ilifanya makosa. Hii inaonesha jinsi wenzetu wanavyojali thamani ya utu, wanavyotunza kumbukumbu, na walivyo tayari kusimamia haki zao kizazi na kizazi. Aidha kwa funzo hilo wenzetu wamefanya mabadiliko makubwa kwenye mifumo ya uendeshaji wa mambo yao hasa namna ya kulinda afya na usalama wa watu wao. Hawa ndio watu ambao tunawaita mabepali na mabeberu.
Cha ajabu ni kwamba sie tunaojiita wajamaa ndio tunaoongoza kwa kutothamini uhai hata wa watoto wetu wenyewe. Hebu fikiria mpaka sasa nchi yetu haina mfumo wa kuaminika wa kudhibiti majaribio hatari yanayofanywa kwenye maabara zetu. Yawe majaribio ya madawa, vyakula, au mbu kama waliotajwa katika taarifa hii. Serikali imewapa uhuru mkubwa maprofesa, wasimamizi wa miradi na wafadhili kufanya wanavyoona inafaa kwa faida yao.
Uchunguzi nilioufanya umebainisha kwamba wasimamizi wa miradi mingi nchini hufanya jitihada kubwa kufanikisha miradi yao ili kujipatia heshima, na kuendelea kupokea fedha za wafadhili, lakini hawaweki kipaumbele kwenye masuala ya usalama wa Taifa. Hii ni kwa sababu wanaopewa nafasi za kuwa waangalizi hulipwa fedha nyingi na wafadhili (Tshs kati ya Tshs. 250,000 na 400,000 kwa siku (PDM) Ukilinganisha na Tshs. 100,000 hadi 150,000 kwa siku zinazotolewa na serikali kwa kazi hiyohiyo. Hili ndilo linalosababisha miradi hatari iendelee kufanyika nchini mwetu kwa uhuru kwani hakuna anayethubutu kuilalamikia.
Katika nchi nyingine majaribio ya kisayansi husimamiwa kwa ukaribu na idara za usalama wa Taifa za nchi husika kupitia idara na vitengo vya kificho vilivyojipenyeza au kuundwa maalum kwa lengo hilo. Hili ndilo linalowezesha majaribio hayo kufanywa kwa ufanisi, usiri wa hali ya juu, na kwa usalama zaidi. Tanzania inazo asasi zisizo za kiserikali zenye malengo na muelekeo mzuri. Tatizo ninkuwa asasi hizo pia zinaendeshwa kwa misaada ya wafadhili jambo linalozipunguzia nguvu ya kufanya kazi. Baadhi ya asasi hizo ni Tanzania Alliance for Biodiversity (TABIO) African Center for Biodiversity (ACB) na Tanzania Organic Agriculture Movement (TOAM). Ni vyema serikali itupie macho suala hili kwa manufaa ya watanzania.
Ustawi wa Tanzania ni jukumu letu sote.
Rev. Godwin Chilewa.
Bình luận